27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

JPM awakuna wadau wa SAGCOT Nyanda za Juu

Mwandishi Wetu, Njombe

WADAU mbalimbali wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), wamepongeza hotuba ya kizalendo ya Rais Dk. John Magufuli hivi karibuni kuhusu uwekezaji na kuelezea kuwa dhamira hiyo itachochea ukuaji wa sekta ya viwanda  hapa nchini.

Akizindua Kiwanda kipya cha Kuchakata chai cha Kabambe kinachomilikiwa na Kampuni ya Unilever Tanzania, Dk. Magufuli aliwaonya watendaji katika ngazi zote serikalini kuachana na urasimu usio wa msingi kwa kukwamisha uwekezaji.

Mwenyekiti wa Wood Foundation, Sir Ian Wood, alisema kauli ya Rais Dk. Magufuli imeonyesha dhamira ya wazi kuwa anakerwa na watendaji wachache wanaokwamisha ukuaji  na maendeleo ya sekta za viwanda na uwekezaji.

Mbali ya kumpongeza Rais Magufuli, Sir Wood alisema taasisi yake itaendelea kufanya kazi kwa karibu na SAGCOT kwani kuwepo kwake kumechangia kuleta mageuzi mengi katika sekta ya kilimo katika ukanda huo.

“Maendeleo yanayopatikana hapa ni matokeo chanya ya kazi  na uratibu mzuri wa SAGCOT kama kiunganishi sahihi kwa wadau wote. Taasisi yangu kama mdau tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na SAGCOT,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Geoffrey Kirenga, alisema katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja, Rais Magufuli amefungua viwanda viwili muhimu katika eneo la SAGCOT.

“Kabla ya uzinduzi wa Kiwanda cha Kabambe ambacho kitawanufaisha sana wakulima wadogo wa chai katika vijiji vyote vinavyozunguka kiwanda hicho, rais pia alifungua kiwanda cha kuzalisha vifaranga vya kuku na chakula cha Silverlands kilichopo mkoani Iringa,” alisema Kirenga ambaye pia ni Bwana Shamba.

Alisema wakati umefika kwa wataalamu kutoka maeneo nje ya ukanda huo kutembelea maeneo ya ukanda huo kujifunza na kujionea jinsi sekta za umma na binafsi zinavyounganisha nguvu na kuleta maendeleo kwa wakulima.

“Ukitembelea eneo la SAGCOT utaona namna gani Serikali na sekta binafsi zinavyofanya kazi kwa pamoja. Miaka michache ijayo utashuhudia mabilionea wakitoka katika sekta ya kilimo. Unilever Tanzania  na Silverlands Tanzania ni wadau wa SAGCOT,” alisema.

Naye Mkulima wa chai na parachichi wilayani NJombe, Christom Mkole, aliishukuru SAGCOT kwa kuwa mstari wa mbele kuwajengea uwezo wakulima wadogo na kufanya kilimo biashara.

“Kwangu mimi SAGCOT ni kila kitu kwani uwepo wao hapa una maana kubwa sana kwa wakulima wadogo. Kiwanda cha Chai cha Kabambe ni mkombozi mkubwa kwa wakulima kwani watakuwa na uhakika wa soko,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles