25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM atoa onyo kali wanaowazungusha wawekezaji

ANDREW MSECHU

RAIS Dk. John Magufuli amewaweka kitanzini watendaji wa Serikali wanaokwamisha wawekezaji, huku akitaka mabalozi kuwapeleka kwake watendaji wanaowazungusha wawekezaji ili naye awazungushe kama tairi.

Alisema ili kuvutia wawekezaji, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), alikihamishia Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini akiona huko pia wanasuasua atairudisha Ofisi ya Rais ili mtu akifika leo akitaka kuwekeza, kesho apate anachotaka.

Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata majani ya chai cha Ruangu mkoani Njombe jana, Rais Magufuli alisema watendaji katika maeneo hayo muhimu wamekuwa kikwazo na kusababisha wawekezaji kukimbilia nchi jirani.

Alisema kwa upande mmoja, masharti magumu ya uwekezaji nchini yamekuwa kikwazo kwa uwekezaji hivyo ni vyema masharti hayo yapunguzwe.

“Kumekuwa na masharti magumu ya uwekezaji, wawekezaji wengi wanakimbilia nchi jirani kwa sababu ya urasimu na vi-masharti vya hovyo vimekuwa vingi. Tunajichelewesha wenyewe.

“Unakuta mwekezaji anakuja kuwekeza nchini, mara wanaanza kutokeza watu wa mazingira wanakuja na yao wakati mazingira ya Mungu yapi, mara wanakuja Osha sijui wanataka kuosha uso au nini. Mimi sasa ndiyo Rais na ninasema wawekezaji ukipata tu kiwanja anza kujenga hayo mambo mengine yatakuja baadaye,” alisema.

Alisema tatizo lililopo ni kwa watendaji kuwa na ‘vichwa kama kamongo’, hawafai na wamekuwa tatizo katika uwekezaji, kwa kuwafanya wawekezaji kuwa maadui zaidi ya kuwafanya marafiki.

Rais Magufuli aliwataka mabalozi wa nchi za nje kuwasiliana naye moja kwa moja iwapo kuna wawekezaji kutoka katika nchi zao ambao wanazungushwa wanapofika nchini, ili aweze kuwashughulikia watendaji wanaowasababishia urasimu.

“Ninawaambia mabalozi kama kuna wawekezaji wanataka kuwekeza nchini na wakazungushwa zungushwa, waleteni kwangu ili na mimi niwazungushe hao watumishi, nitajua nitawazungusha kama tairi au nini,” alisema.

Rais Magufuli pia alimshukuru Mkurugenzi wa Kampuni ya kimataifa ya Unilever ya Uingereza iliyojenga kiwanda hicho, Sir Iron Hood, akisisitiza kwamba hatua hiyo itasaidia kuongeza ushindani kwa viwanda vya ndani ambavyo vingi vimekuwa vikideka na vigine vimelala.

Alisema Uingereza ndiyo inayoongoza kwa wawekezaji wengi nchini, hivyo anaona fahari kubwa kuzindua kiwanda hicho katika ziara yake ya mikoa ya kusini mwa Tanzania, ambayo jana aliingia rasmi katika Mkoa wa Njombe.

KUSHIRIKIANA NA WAHISANI

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewashukuru wahisani kwa misaada yao na kusema uwepo wao katika uzinduzi wa Kituo cha Afya Madaba mkoani Ruvuma ni ishara ya kutambua juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwaletea maendeleo Watanzania.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa kituo hicho cha afya kilichopo katika Kata ya Madaba wilayani Songea, ikiwa ni siku ya mwisho katika ziara yake mkoani Ruvuma, Rais Magufuli alisema Serikali imehakikisha fedha zote kutoka kwa wafadhili zinatumiwa ipasavyo.

“Awali fedha zilikuwa zinakuja zinapelekwa kwenye halmashauri zinaliwa, tukaamua kubadilisha utaratibu, kwa hiyo sasa tunazipeleka moja kwa moja kwenye miradi na miradi yote imekuwa ikitekelezwa ipasavyo,” alisema.

Rais Magufuli alisema Serikali yake itaendelea kushirikiana na wahisani, ili kuhakikisha malengo ya pande zote mbili.

Alisema Serikali yake imeamua kuwekeza katika kulinda afya za watu kutokana na taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuonesha kuwa zaidi ya Dola za Marekani trilioni 2.4 hupotea katika nchi za Afrika kila mwaka kutokana na kushindwa kuwekeza katika sekta ya afya na kulinda afya za watu.

Rais Magufuli alisema fedha zilizotolewa katika ujenzi wa kituo hicho cha afya ni Sh milioni 400 ambazo zinatoka kwa wafadhili, hivyo ni suala la kusheshimiwa kwa kuwa fedha hizo ni za walipakodi kutoka katika nchi zao.

“Sasa hivi wafadhili wanatoa fedha zao kwa sababu hazipotei. La sivyo hawa wote msingewaona, wasingekuja hapa,” alisema.

Alisisitiza kwamba katika Serikali yake, anataka nchi ipasue anga katika maendeleo kwenye nyanja zote, ikiwemo miundombinu, afya, elimu na nishati.

Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema katika miaka mitatu ya Rais Magufuli, Serikali imesimamia vyema sekta ya afya hasa katika ujenzi wa miundombinu na kuboresha huduma za afya katika halmashauri.

Alisema pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya Madaba, katika Mkoa wa Ruvuma, bajeti ya dawa imeongezeka kutoka Sh milioni 845 hadi bilioni tatu katika miaka mitatu iliyopita.

Ummy alisema tayari Rais Magufuli alitoa agizo la kugawa vifaa vyenye thamani ya Sh bilioni tano yakiwamo magodoro 50, vitanda 50, mashuka 100 kwa kila halmashauri kwa mkupuo mmoja, ambalo tayari lilishatekelezwa.

Alisema tayari watumishi 8,000 wameajiriwa katika sekta ya afya, na kati ya hao 290 wamepelekwa Mkoa wa Ruvuma, huku Kituo cha Afya Madaba kimepata watumishi 22 wapya.

ATENGUA UTEUZI

Wakati huo huo Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Dk. Oscar Mbyuzi.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana, ilisema kufuatia uamuzi huo, Rais Magufuli amemteua Jimson Mhagama kuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo.

“Uteuzi wa Mhagama unaanza mara moja leo (jana),” inasema taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Gerson Msigwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles