31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ataka waziri wa Mkapa anyang’anywe kiwanda

NORA DAMIAN Na FROLENCE SANAWA

-DAR/MTWARA

RAIS Dk. John Magufuli ameagiza wote waliobinafsishwa viwanda vya kubangua korosho, akiwamo aliyekuwa waziri wakati wa Serikali ya awamu ya tatu na sasa havifanyi kazi, wanyang’anywe mara moja.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Afya Mbonde kilichopo wilayani Masasi, alisema anayepewa kiwanda ni lazima azalishe kuliko kilivyokuwa kikizalisha.

“Kiwanda cha Newala ambacho hakifanyi kazi kabisa, Waziri wa Kilimo mnyang’anye hata kama ni leo, akikataa mpelekeni mahakamani.

“Kingine ni cha waziri wa awamu ya tatu, mnyang’anyeni na akikataa mpelekeni mahakamani, mimi nikishamaliza muda wangu ndio muwe mnabembelezana, kwa wakati wangu hakuna kubembelezana, ni lazima twende kwenye mstari unaonyooka.

“Kama amekaa nacho miaka 10 tumuulize Serikali ingepata kiasi gani, awalipe wafanyakazi ambao wangeajiriwa kwa miaka 10.

“Hatuwezi kuwahamasisha wananchi kulima korosho halafu hakuna mahali pa kuzipeleka, Nyerere (Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere) hakuwa mjinga, aliangalia mbele.

“Kubinafsisha si kosa, lakini kosa ni yule uliyempa halafu akashindwa kuendeleza kiwanda,” alisema Rais Magufuli.

Aliziagiza Wizara za Kilimo na Viwanda kukagua viwanda vyote vya korosho na kuvichukulia hatua vile ambavyo havizalishi. 

“Katibu Mkuu wa Viwanda mbaki huku mkashughulikie viwanda vyote, kuna cha Tunduru, Mtwara Mjini na hapa kipo (Masasi).

“Kuna mmoja nimempigia simu asubuhi anasema nimpe mwezi mmoja tu kitafanya kazi kwa asilimia 100, atakayeshindwa mnyang’anyeni hata akienda mahakamani nendeni, mnaogopa nini,” alisema.

VITUO VYA AFYA

Rais Magufuli alisema awali alikuwa anasita kuvifungua vituo vya afya kwa kuhofia kufungua vituo hewa. 

Alizindua Kituo cha Afya Mbonde kwa niaba ya vituo 352 vilivyojengwa nchi nzima ambavyo vimegharimu Sh bilioni 184.

“Ilibidi nihakikishe kwanza vituo vyote 352 viko kwenye hali gani nisije nikafungua kanyaboya, baada ya kupata taarifa ndiyo maana nimekuja kufungua,” alisema Rais Magufuli.

Alifafanua kuwa katika Mkoa wa Mtwara vituo vilivyokarabatiwa na kukamilika viko saba na vingine sita vinaendelea kukarabatiwa na kwamba watapata hospitali tatu mpya Masasi, Nanyamba na Mtwara.

Pia aliahidi kuleta gari la wagonjwa na akawatahadharisha watu kudhibiti hasira zao pindi kunapotokea vurugu.

MANGAKA

Akiwa katika ufunguzi wa barabara ya Mangaka – Nakapanya – Tunduru eneo la Mangaka wilayani Nanyumbu, Rais Magufuli alitoa siku tano kwa Wizara ya Mazingira na Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kutoa vibali kuwezesha makaa ya mawe kuweza kusafirishwa kutoka eneo la Mangaka. 

Pia aliahidi kutoa Sh milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya CCM wilayani Nanyumbu na Sh milioni 5 katika Shule ya Msingi Mkuti kusaidia kutatua changamoto mbalimbali shuleni hapo.

WABUNGE

Mbunge wa Masasi, Rashidi Chuachua (CCM), alimwomba Rais Magufuli kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara jimboni humo kwani kati ya kilomita 303.25 ni 3.8 pekee ndizo zenye lami.

Alisema pia kwa kutegemea mapato ya ndani wameanza tena kujenga vituo viwili vya afya katika kata za Napupa na Matalale.

Mbunge wa Lulindi, Jerome Bwanausi (CCM), alisema jimbo hilo lina kata 18, lakini kituo kinachofanya kazi ni kimoja tu cha Nagaga.

“Tuna tatizo kubwa sana la kuwasafirisha wagonjwa kutoka Kituo cha Afya Nagaga kwenda hospitali ya wilaya kwa sababu gari lililokuwepo liliungua miaka mitano iliyopita,” alisema Bwanausi.

Mbunge huyo pia aliomba katika bajeti ijayo waongezewe vituo vya afya viwili au vitatu kwani baadhi ya kata hazina zahanati wala kituo cha afya na ni maeneo ambayo yana mazingira magumu sana.

MAWAZIRI

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema hadi sasa Sh bilioni 593 zimelipwa kwa wakulima wa korosho na kwamba Sh bilioni 50 alizoagiza Rais Magufuli zilifika juzi na tayari wametumia Sh bilioni 10.8 kulipa wakulima mbalimbali. 

Alisema korosho zilizonunuliwa ni tani 222,824.6 na kati ya hizo 31,370.8 zimezalishwa kutoka Wilaya ya Masasi zenye thamani ya Sh bilioni 103.4.

“Pamoja na kwamba wamelima vizuri, lakini kwenye upande wa malipo hatujafanya vizuri upande wa Masasi kwa sababu walio wengi ni wale wakulima wakubwa, lakini wadogo wamelipwa wote,” alisema Hasunga.

Alisema pia juzi walianza jitihada za kulipa wakulima ambao akaunti zao zilikuwa na matatizo na wameweza kulipa Sh bilioni 4.3. 

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema Sh milioni 53 zimetolewa katika Shule ya Msingi Mbonde kuongeza madarasa mawili na matundu 10 ya choo.

Alisema pia shule za msingi Mkapandu na Kambarage nazo zimepatiwa Sh milioni 53 kila moja. 

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema kutokana na uwekezaji uliofanywa katika sekta ya afya, vifo vya wajawazito wilayani Masasi vimepungua kutoka 22 hadi sita.

Pia alisema vifo vitokanavyo na ugonjwa wa malaria vimepungua kutoka 67 hadi kufikia 47 na kwamba asilimia 111 ya watoto Masasi wanapata chanjo za kuwakinga na magonjwa mbalimbali.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema Kituo cha Afya Mbonde kimegharimu Sh milioni 500 na kwamba katika bajeti ya 2019/2020 watajenga hospitali nyingine kubwa 20.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, alisema Sh bilioni 5.8 zilitengwa kwa ujenzi wa vituo vya afya 13 kikiwemo Mbonde kilichopatiwa Sh milioni 500.

“Majengo unayoyaona hapa yamejengwa kwa mfumo wa Force Account, tumetumia mafundi wetu wa kawaida, mafundi wa hapa ndio wamefanya kazi na kipindi chote cha ujenzi wamepata ajira,” alisema Byakanwa.

Alisema pia wamepokea Sh bilioni 4.5 kwa ujenzi wa hospitali za wilaya ambazo ziko katika hatua mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles