26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ashusha rungu mimba za utotoni

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amewataka wanaume mkoani Rukwa kuacha tabia ya kuwapa ujauzito wanafunzi wa kike na badala yake watafute wale ambao wameshamaliza shule.

Kutokana na hilo, ameutaka uongozi wa mkoa, wilaya na vyombo vya dola wawachukulie hatua wale wote waliohusika kuwapa mimba wanafunzi ili waweze kufungwa miaka 30 kwa mujibu wa sheria.

Kiongozi huyo wa nchi alitoa kauli hiyo jana wakati akiwahutubia wananchi wa Mkoa wa Rukwa, Uwanja wa Mandela baada ya kuzindua mradi wa maji safi na mazingira.

Alieleza kushangazwa kuona mkoa huo ambao ni wa pili kwa kuzalisha mazao nchini, ndio unaoongoza kwa kuwapa mimba watoto.

Vilevile aliwataka wazazi ambao wamekuwa wakiwaozesha watoto wakiwa wadogo waache mara moja na badala yake wawaache wamalize kwanza kusoma.

“Kwa takwimu nizilizonazo, Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwapa wanafunzi ujauzito, nimeambiwa kwa mwaka jana tu wanafunzi 229 walipata ujauzito.

“Tumeeleza tumekuwa tukitoa fedha kwa ajili ya elimu bure kwa watoto wetu kuanzia darasa la kwanza hadi sekondari, lakini ninyi mnatoa mimba bure, sasa tutakuwa tunatoa hela kumbe tunapata hasara.

 “Ninajua mnakula vyakula vyenye nguvu, mkatafute ambao wamemaliza muda wao, msiwaonee hawa wanafunzi, na ninyi watoto muache viherehere mtayakuta tu baadaye.

“Kwa hiyo hili ni lazima tulisimamie na ninyi wazazi tuwafundishe watoto wetu, yaani unamuona mtoto anaenda ‘tution’ hana hata daftari unamuacha tu.

“Hawa ni watoto masikini, tusiwarubuni kwa kuwa ni malaika na vyombo vya dola muanze kuwashughulikia hawa watu wanaowapa mimba kwani sheria inajulikana ni miaka 30, akishaenda gerezani ataelewa nini maana ya mimba, hii ni aibu kubwa katika mkoa wenu,” alisema Rais Magufuli.

Vilevile aliwataka viongozi wa dini kutumia muda wao kuwaasa watu wanaowapa mimba watoto, huku akiwataka wazazi kuwakanya watoto wao.

Hata hivyo, aliupongeza uongozi wa mkoa huo kwa maendeleo ambayo yanaonekana huku akisema Rukwa ya miaka mitano iliyopita ni tofauti na ya sasa.

“Huwezi ukaacha kujenga uwanja wa ndege ukitaka ‘ku-promote’ watalii, kuinua uchumi, mahali ambapo pamepatikana gesi na mengine mengi.

“Huwezi ukaacha kujenga uwanja wa ndege ukitaka kutangaza watalii, kuinua uchumi na mambo mengine mengi… kuna Sh bilioni 55.2 tunajenga uwanja mkubwa wa ndege hapa, tulianza na musuala ya kulipa fidia, tukaamua kwamba ni lazima tupange na tuamue ambapo ndege zitakuwa zinatua hata usiku, naomba hii ahadi muiamini.

“Kwa sababu huwezi kununua ndege halafu haziwezi kufika Rukwa, ukishaweka uwanja mkubwa hapa hata watu wa Tunduma, Zambia na DRC watakuja hapa.

“Naomba muamini, uwanja unakuja wala msiwe na wasiwasi ndugu zangu, ninafahamu pia changamoto ziko nyingi katika maeneo yetu, bonde la Rukwa kuna wafugaji na wakulima wengi na hatujatumia vizuri Ziwa Tanganyika,” alisema.

Aidha alitoa wito kwa Wizara ya Mifugo, uongozi wa mkoa,  wilaya na wananchi wenye uwezo wa kujenga viwanda vya samaki watumie fursa hiyo.

Alisema pamoja na hilo, anafahamu kuwa kuna changamoto katika manispaa hiyo kuhusu mabishano juu ya ujenzi wa soko na kwamba wapo watu waliochanga fedha kujenga mabanda, lakini baadaye wakuzuiwa kufanya biashara katika eneo hilo.

Baada ya kupata maelezo kutoka kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Rukwa na uongozi wa soko, Rais Magufuli aliahidi kuchangia Sh milioni 300 ili ziweze kusaidia ujenzi wa soko ambalo liliungua na moto mwaka juzi.

Kiongozi wa soko hilo ambaye hakujitaja jina, alisema tangu soko hilo lilipoungua, walichanga zaidi ya Sh milioni 15 na baadaye nje ya fedha hizo walichanga Sh 800,000 ambazo zote walizikabidhi kwa uongozi wa manispaa, lakini wamekuwa wakisumbuliwa kwa maelezo kwamba wanataka kujenga ghorofa.

“Baadaye tulijenga mabanda yetu, lakini tunasumbuliwa na manispaa wakisema lazima wajenge ghorofa, sasa nyanya na mchicha tutauza kwenye ghorofa?” alihoji mfanyabiashara huyo.

Kutokana na hilo, Rais Magufuli aliwataka viongozi hao wa manispaa kujifunza namna ya kutatua matatizo ya wananchi. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles