24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

JPM APOKEA UJUMBE WA SULTAN QABOOS WA OMAN

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli jana alipokea ujumbe maalumu wa Sultan Sayyid Qaboos bin Said Al Said wa Oman.

Alimuhakikishia nchi hiyo ipo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda, uzalishaji wa nishati, kuongeza thamani ya madini.

Oman pia itaendeleza sekta ya gesi na mafuta na  ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo kukuza uchumi kwa kasi zaidi.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilieleza kuwa ujumbe huo wa Sultan Qaboos uliwasilishwa jana na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dk. Mohammed Hamad Al Rumhy.

Waziri huyo alifuatana  na Waziri wa Uwekezaji wa nchi hiyo, Salem Ben Nasser Al Ismaily   na Naibu Waziri wa Utalii, Maitha Saif Majid, Ikulu  Dar es Salaam.

Dk. Rumhy ambaye ameongoza watu zaidi 300 waliowasili  nchini kwa meli ya Sultan wa Oman, alisema ziara hiyo imelenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Oman hususan katika masuala ya uchumi, ambako nchi hiyo inabadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu biashara ya mafuta na gesi.

Pia itajenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea katika ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, itajenga viwanda vya mazao na kununua mazao ya wakulima na itawekeza katika uchakataji wa madini  kuyaongezea thamani.

“Mheshimiwa Rais tunataka kushirikiana nanyi kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, tunataka Bagamoyo isiwe eneo la bandari tu bali pia liwe ni eneo ambalo tutajenga viwanda mbalimbali.

“Tuzalishe mbolea na tununue mazao ya wakulima na kuyasafirisha, sisi tupo tayari na kesho tunakwenda kuangalia eneo hilo kazi ianze mara moja,” alisema Dk. Rumhy.

Rais Magufuli alimshukuru Sultan  wa Oman, Sayyid Qaboos bin Said Al Said kwa kutuma ujumbe huo na alimhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Oman.

Magufuli alimtaka Dk. Rumhy kufikisha ujumbe wake kwa Mfalme na wawekezaji wa Oman kuwa atafurahi kuona uwekezaji huo unaanza mara moja na Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Mheshimiwa Dk. Mohamed naomba ukamwambie Mfalme kuwa namshukuru kwa ujumbe huu na namkaribisha sana Tanzania.

“Nimefurahi kuona mpo tayari kushirikiana nasi kujenga viwanda, kuzalisha mazao na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo.

“Sisi tupo tayari hata leo, njooni tushirikiane kwa sababu nyinyi ni ndugu zetu na tutafanya uwekezaji kwa faida yetu sote,” alisema  Rais Magufuli.

Aliitaka Oman iongeze ushirikiano na Tanzania katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika usindikaji wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana wataalamu wa nyanja mbalimbali wakiwamo walimu wa Kiswahili na Kiarabu.

Alimshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada wa kujenga visima vya maji 100 nchini na amemuomba kuungana na Serikali katika safari yake ya kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu itakayoweka kumbukumbu ya ushirikiano wa undugu na historia kati ya nchi hizi mbili.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Suzan Alphonce Kolimba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles