29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM APIGA MARUFUKU MACHINGA KUNYANG’ANYWA BIDHAA

HUJAMBO?: Rais Dk. John Magufuli akiwa amembeba mtoto, Ikrama Mahadi (miezi-3) alipokuwa akiwasalimia abiria ndani ya ndege Boeing 787-8 Dream Liner ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) alipokuwa akielekea Mwanza ikiwa ni maraya kwanza kwake kusafiri kwa kutumia ndege hiyo mpya akiwa na abiria wengine. PICHA: IKULU

Na MWANDISHI WETU                  |             


RAIS Dk. John Magufuli amepiga marufuku viongozi wa halmashauri nchini kuwanyang’anya bidhaa wafanyabiashara wadogo – maarufu machinga, na badala yake amewaagiza kujielekeza kutatua kero zinazowakabili wananchi, ikiwamo ukosefu wa soko la mazao yao.

Alitoa agizo hilo baada ya wananchi wa Sengerema kudai halmashauri ya wilaya hiyo imekuwa ikiwanyang’anya matunda aina ya nanasi wakulima na wafanyabiashara wanaouza mjini hapo.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, imemkariri Rais Magufuli akimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, kufuatilia na kutatua kero hiyo.

“Nilishasema viongozi wote niliowateua mimi msisherehekee uteuzi, mtasherehekea siku mkimaliza uongozi, nataka mchape kazi, tatueni kero za wananchi na waleteeni maendeleo,” alisisitiza Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, aliwahakikishia Watanzania kuwa juhudi za kujenga Tanzania mpya zinakwenda vizuri kutokana na mafanikio makubwa yaliyoanza kupatikana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo wakati akisalimiana na wananchi waliokusanyika katika njiapanda ya Bugando jijini Mwanza na mjini Sengerema, akiwa njiani kuelekea Chato mkoani Geita kwa mapumziko.

Alisema utekelezaji wa ahadi za Serikali ya Awamu ya Tano unakwenda vizuri.

Kwamba katika kipindi kifupi cha miaka miwili na miezi minane, kumekuwa na kasi kubwa ya ujenzi wa viwanda vilivyofikia 3,060, Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) limefufuliwa, miundombinu ya barabara na madaraja inajengwa, watoto wanapata elimu bure na mengine mengi ambayo yamechangia kupanua wigo wa ajira na kukuza uchumi wa nchi.

“Nataka kuwahakikishia ndugu zangu tunakwenda vizuri, juhudi zetu za kujenga Tanzania mpya zinapata mafanikio makubwa, tumejenga viwanda vingi, nataka tuirudishe Tanzania ya Nyerere ambayo hapa Mwanza kulikuwa na viwanda vingi na vijana wengi walipata ajira,” alisema.

Kabla ya kukutana na wananchi wa Mwanza, Rais Magufuli aliwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya uangalizi maalumu (ICU) ya Hospitali ya Bugando jijini Mwanza ambapo dada yake Monica Joseph Magufuli alikuwa miongoni mwao.

Akiwa hospitalini hapo, Rais Magufuli aliwashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuwatibu wagonjwa.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na uongozi wa hospitali hiyo kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.

Mapema jana asubuhi, Rais Magufuli alisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyonunuliwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha shirika hilo.

Akiwa ndani ya ndege hiyo, abiria waliosafiri nae kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, walimshangilia na kumpongeza kwa juhudi zake za kuifufua ATCL na wamemwombea dua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles