27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JPM  ‘AMTOLEA UVIVU’ MBUNGE WA CCM

Mwandishi wetu


RAIS John Magufuli amemtolea uvivu Mbunge wa Morogoro mjini, Aziz Abood, akimtaka aendeleze viwanda alivyochukua vinginevyo avirudishe vigawiwe kwa watu wengine.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikuli, Gerson Msigwa, Rais Magufuli alisema hayo jana baada ya msafara wake uliokuwa ukitoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, kusimamishwa na wananchi wa Morogoro katika eneo la Msamvu.

Wananchi hao pia walizungumzia kunyanyaswa kwao na mgambo wa manispaa kwa kuwafukuza katika maeneo wanayofanyia biashara hasa baada kituo cha mabasi cha Msamvu kujengwa upya.

Rais Magufuli alisema kama mbunge wa eneo hilo ameshindwa kuendeleza viwanda alivyochukua wakati wa ubinafsishaji,  avirudishe wapewe watu na vijana wapate ajira.

 “Ninarudia wito wangu niliokwisha kuutoa huko nyuma  kwamba wenye viwanda hapa Morogoro ambao wameshindwa kuviendesha, na leo nataja akiwamo Mbunge wa hapa (Morogoro mjini) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)… narudia akiwamo Mbunge wa hapa wa CCM ambaye alibinafsishiwa viwanda vingi.

Kama ameshindwa kuviendesha avirudishe tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira, nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu, alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amewaagiza viongozi wa Manispaa ya Morogoro na viongozi wa mkoa wa huo  kuwaacha wafanyabiashara ndogondogo wa mji huo waendelee kufanya biashara zao katika eneo la kituo cha mabasi cha Msamvu.

Alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, kuhakikisha  mgambo hawawasumbui wafanyabiashara ndogondogo.

Amewataka pia wafanyabiashara hao kutofanya vurugu wakati utaratibu mzuri unaandaliwa kwa ajili yao.

Rais Magufuli pia amewapongeza wakulima mkoani Morogoro kwa kuongeza uzalishaji wa mazao.

Alisema wakulima wa Wilaya ya Kilosa wameongeza uzalishaji kutoka asilimia 42 msimu uliopita hadi asilimia 82 katika msimu huu.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi wa Morogoro kujitokeza kupata ajira wakati wa ujenzi.

Lakini amewataka waliojenga katika hifadhi ya reli kuondoa majengo yao kwa hiari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles