24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM amtia ndani mtumishi, amtoa baada ya dakika tano

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, kumweka ndani mtoza ushuru aliyemtaja kwa jina moja la Pesha na baadaye ndani ya dakika tano akaagiza tena aachiwe.

Alitoa agizo hilo jana wakati aliposimama na kuzungumza na wananchi katika mji wa Kyaka mkoani Kagera akielelekea Karagwe.

Alichukua uamuzi huo baada ya baadhi ya wamachinga kulalamika kuwa pamoja na kwamba wana vitambulisho, lakini bado wanatozwa kodi na mtu anayeitwa Pesha.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli alimwita Mkurugenzi wa Wilaya, akimtaka aeleze kwanini wanawatoza wafanyabiashara waliopewa vitambulisho.  

“Mkurugenzi wa wilaya hapa uje hapa kwa sababu watendaji wanaokusanya kodi wanatumwa na wewe… uje ueleze kwanini mnawatoza tena watu. Je, uliwatuma wewe au walijituma wenyewe?” alihoji Rais Magufuli.

Kutokana na hilo, mkurugenzi huyo alisema; “Mheshimiwa Rais, kama ulivyotupa maagizo yako tuwape vitambulisho tulitekeleza, hakuna niliyemtuma na kama yupo nitamshughulikia.”

Rais Magufuli akahoji wananchi; “Ni nani anayekujaga kukusanya fedha hapa? Nimtaje? (wananchi wanamtaja Pesha)… yuko wapi huyo Pesha, njoo hapa tumalizane hapa hapa kwanini unawadai watu wenye vitambulisho.”

Baadaye Pesha naye alieleza; “Mheshimiwa Rais, sisi ofisini kwetu kuna utawala tofauti, mimi naagizwa na idara yangu ya mapato.”

Baada ya maelezo hayo ya Pesha, Rais Magufuli alimwita Kamanda wa Polisi wa mkoa huo; “RPC mchukue huyu akalale lock-up akaeleze hizo fedha alizokusanya kwa watu wenye vitambulisho kazipeleka wapi.

“Halafu mkurugenzi ufuatilie hizi fedha warudishiwe hawa wafanyabiashara ambao wana vitambulisho wakatozwa. Narudia tena leo (jana) kwa viongozi wote ndani ya Serikali, mwenye kitambulisho hatakiwi kuombwa hela yoyote kwa sababu wamelipia mwaka mzima, kuwatoza tena kodi wakati walishalipia kile kitambulisho huo ni wizi.

“Nikuombe mkurugenzi msiwabughudhi wenye vitambulisho, lakini ambao hawana wachape, wale wenye maduka msiwabane katika biashara zao, hawa na wao wanalipia.

“Kwa sababu huyu mwenye duka naye analipa kodi kubwa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania)… na ninyi machinga msiende mkaziba biashara ya mtu, huyu naye analipa kodi kubwa kuliko ninyi.”

Kutokana na hilo, aliwataka viongozi wa mikoa na halmashauri kufanya mawasiliano mazuri kati ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa.

“Pia mkurugenzi uwe unawa-monitor watu wako wasikuharibie kazi wewe,” alisema Rais Magufuli.

Baada ya maelezo hayo, Rais Magufuli aliagiza Pesha aachiwe na kwamba amemsamehe.

“Pesha toka huko ndani, ngoja nimsamehe, mleteni hapa… unajua naye ana watoto ila akirudia hiiiiiiiiii! au twende naye tu? Tumsamehe? Mwachieni atubu kwa wananchi na wale waliotozwa muangalie namna ya kurudisha, mtoeni ila asirudie.

“Mimi ninafahamu shida za wananchi hawa wanazozipata nikasema nitatoa vitambulisho. Kwa mwenye kitambulisho nilisema afanye biashara kokote na asihonge hata senti tano, akija Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya au Waziri mimi ndiye bosi wao mwenye kitambulisho afanye biashara kokote,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli alisema vijana wana wajibu wa kuitunza amani kwa sababu ikikosekana hata biashara hawawezi kufanya na wengine watakuwa wanaogopa kwenda kanisani au msikitini.

“Panapotokea amani hata mimi mtawala nitatawala vizuri kwa ajili ya maendeleo ya nchi, pasipokuwa na amani huwezi kununua ndege na badala yake utaenda kununua mabomu na mizinga,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimpigia simu Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, akimtaka kuhakikisha maji yanapatikana katika mji wa Kyaka mkoani Kagera.

“Kata pesa popote leta hapa, nataka wananchi wa hapa washerehekee Sikukuu ya Krismasi mwaka 2019 wakiwa na maji, sitaki mfanye upembuzi yakinifu kwa sababu ukiangalia hapa unaona kabisa maji yapo tu,” alisema Rais Magufuli.

Wakati akizungumza na Profesa Mbarawa kwa njia ya simu, aliiweka karibu na kipaza sauti na mazungumzo yake na waziri huyo kusikika kupitia spika kubwa.

Profesa Mbarawa akimjibu, alisema amepokea maagizo hayo na atafika Kyaka hivi karibuni kuanza kazi kama alivyoagizwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles