23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AIFUTA CDA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli ameivunja Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na kuagiza mali na shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na mamlaka hiyo zihamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.

Pamoja na mambo mengine, hatua hiyo inatokana na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma, kuwa CDA imekuwa ikitoa viwanja katika maeneo yenye mkondo wa maji na hivyo kusababisha mafuriko.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli amevunja bodi hiyo na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Paskasi Muragili atapangiwa kazi nyingine.

Mkuu huyo wa nchi, pia aliagiza wafanyakazi wote wa mamlaka hiyo wahamishiwe Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na ofisi nyingine za Serikali kadiri inavyofaa.

 “Rais Magufuli ameamua kuivunja CDA na kuhamishia majukumu yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji wa huduma kwa wananchi, uliokuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili na pia kuendana na mahitaji ya sasa ambayo yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya kuwepo kwa CDA,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Rais Magufuli aliagiza hati zote za kumiliki ardhi zilizokuwa zikitolewa na CDA kwa ukomo wa umiliki wa miaka 33, zibadilishwe na kufikia ukomo wa umiliki wa miaka 99 kama ilivyo katika maeneo mengine nchini ili kuwavutia wawekezaji hasa wa viwanda.

“Wananchi wa Dodoma wamelalamikia tatizo hili kwa muda mrefu sana, hata nilipokuwa kwenye kampeni zangu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 walilalamika sana.

“Sasa nimetekeleza niliyowaahidi, naamini kwa uamuzi huu malalamiko ya wananchi yatapata utatuzi na pia tutakuwa tumeondoa kikwazo cha umiliki wa muda mfupi wa ardhi uliosababisha wawekezaji kushindwa kujenga viwanda Dodoma.

“Sasa majukumu yote yanahamishiwa Manispaa ya Dodoma, sitaki kuendelea kusikia visingizio, mkajipange mambo yaende vizuri,” alisisitiza Rais Magufuli.

Kutokana na hilo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wamemshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi huo, huku wakiahidi kusimamia mchakato wa kuhamisha majukumu ya CDA kwenda Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.

Utiaji saini hati hiyo ulifanyika Ikulu, Dar es Salaam jana, pia ilishuhudiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Wengine walioshuhudia, ni Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana na viongozi mbalimbali wa wizara.

CDA ilianzishwa kwa amri ya Rais, Aprili mosi, mwaka 1973 na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230 na kuvunjwa jana Mei 15, 2017 kwa Amri ya Rais na kuchapishwa katika gazeti la Serikali.

 

WABUNGE

Katika hatua nyingine, wabunge wamefurahishwa na uamuzi wa Rais Magufuli kuifuta mamlaka hiyo.

Wakizungumza na MTANZANIA mjini hapa, wabunge walidai uamuzi huo ni sahihi kutokana na wakazi wa Dodoma kutojua waende wapi – CDA au Manispaa kufuata huduma za viwanja.

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), alisema kuwa alichofanya Rais anatakiwa apongezwe kwani ni kilio cha wananchi wengi kuhusu madudu yaliyokuwa yakifanywa.

Alisema hiyo ilikuwa hoja ya muda mrefu, huku akidai yalikuwa ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma kutokana na kazi moja kufanywa na watu wawili.

“Kazi za CDA ndiyo zilikuwa zinafanywa na manispaa, yalikuwa ni matumizi mabaya ya rasilimali fedha, watu wawili walikuwa wanalipwa mshahara kwa kazi moja,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, amemtaka Rais Magufuli kuzigeukia halmashauri kwa sababu kazi anazofanya mwenyekiti wa halmashauri, ndizo zinazofanywa na mkurugenzi.

“Asichoke, hili limekuwa tatizo kubwa, kuna Mamlaka ya Mto Rufiji imejaa madudu mengi kweli kweli, haipaswi kuwapo,” alisema.

Mbunge wa Makete, Profesa Norman Sigalla (CCM) alisema alichofanya Rais Magufuli ni sawa kwani  amesikiliza kilio cha watu wengi.

“Hoja yoyote inayoletwa na Rais ni matokeo ya mlengo wa kusikiliza kero za wananchi, siwezi kupingana naye kwa sababu anasikiliza wananchi wanataka nini,” alisema.

Naye Mbunge wa Kilombero, Joseph Lijualikali (Chadema), alisema uamuzi huo ni sahihi.

 

WANANCHI

Kwa upande wa wanachi, nao walionekana kupokea uamuzi huo kwa furaha, wakisema Rais Magufuli amekuwa msikivu, kwa sababu ni ahadi aliyoahidi wakati wa kampeni.

Mkazi wa Nkuhungu, Juma Issa, alisema CDA ilikuwa ni zaidi ya mzigo kutokana na kuwacheleweshea viwanja wananchi.

“Ilikuwa ukiwa na safari ya kwenda pale, unawaza mara mbilimbili, yaani walikuwa na ukiritimba wa ajabu, walifanya ofisi kama ya kwao,” alisema.

Lakini Rehema Musa, Mkazi wa Chamwino alisema Rais Magufuli amefanya kosa kubwa kuifuta CDA kutokana na kuupanga vizuri mji wa Dodoma.

“Dodoma ni tofauti kabisa na mikoa mingine, tembelea mtaani kumekaa vizuri hata mtu akiwa Dar es Salaam akianza kukuelekeza nenda Kisasa utaenda mpaka mtaa aliokuelekeza kutokana na ramani nzuri iliyochorwa ya mji huo na CDA,” alisema. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles