JPM AFUMUA MTANDAO VIGOGO WA SUKARI

0
37

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameufumua mtandao wa vigogo wanaofanya biashara ya sukari kutoka nje ya nchi, huku akiagiza kuondolewa kwa watumishi wote wanaohusika na utoaji vibali.

Ametoa siku tatu kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na mwenzake wa Wizara ya Kilimo, Dk. Charles Tizeba, kuwaondoa watumishi hao na kuwapangia kazi nyingine kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana baada ya kutembelea Kiwanda cha Sukari cha Kagera ambako anaendelea na ziara ya kikazi mkoani humo.

“Wizara ya Kilimo kuna watu kazi yao ni kutoa vibali vya sukari na vingine ni vya kughushi ajabu, nafikiri wote wafukuzwe tu na kuhamishiwa kwingine ambapo hawatoi vibali.

“Vibali wamekuwa wakipewa watu ambao hawajawahi kusafirisha sukari, halafu na wao wanakwenda kuviuza kwa wengine… na wengine ni wanachama wa CCM na vyama vingine.

“Ndani ya siku tatu mkawatoe muwapangie kazi nyingine, ni lazima tufanye mabadiliko ya msingi kwa ajili ya kulinda viwanda vyetu. Hata kama walisomea kutoa vibali, watapangiwa kutoa vibali hata vya chanjo za mbwa.

“Na watoa vibali hawawezi kufurahia wakiona viwanda vinafanya kazi kwa sababu ndivyo vinawafanya waishi mjini. Nafuu waondoke waende sehemu nyingine, wawe wamesoma au la, tunataka kwenda mbele, mambo ya kuendekezana tunachelewa,” alisema Rais Magufuli.

 

UZALISHAJI SUKARI

Rais Magufuli alikipongeza Kiwanda cha Sukari Kagera kwa uzalishaji wa sukari na kutoa ajira kwa watu 5,000.

Hata hivyo, alikitaka kiwanda hicho na vingine vinavyojihusisha na uzalishaji sukari, kuongeza uzalishaji ili kuweza kukidhi mahitaji.

Alisema kwa sasa mahitaji ya sukari nchini ni tani 450,000, lakini viwanda vilivyopo vinazalisha tani 320,000.

Alifafanua kuwa Kiwanda cha Kagera kinazalisha 65,000 hadi 67,000, Kilombero (109,000), TPC (100,000), Mtibwa (30,000) na kiwanda kidogo cha Manyara (6,000).

“Mahitaji ya sukari ni makubwa na yanaongezeka siku hadi siku, wito wangu kwa wafanyabiashara wa Tanzania na wawekezaji kutoka nje, huu ni wakati wa kuwa na viwanda vya sukari, tusichelewe.

“Kwa pengo lililopo, naomba kila kiwanda kiongeze uzalishaji angalau tani tano, ili sukari iweze kutosheleza mahitaji,” alisema.

 

WATAHADHARISHWA

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwatahadharisha wenye viwanda kuacha kufanya ujanja ujanja kwa kuagiza sukari ya viwandani kisha kuiweka kwenye mifuko yenye nembo za viwanda vya ndani na kuwauzia wananchi.

“Wenye viwanda vya sukari mtusaidie vinginenyo nchi hii itakuwa dampo, kila kiwanda kinachotegemea malighafi ya ‘Industrial sugar’, mnatakiwa mkijue na mahitaji yao kwa mwaka ni kiasi gani.

“Kuna wafanyabiashara wenye tamaa ambao hawajali afya zetu, sukari hii haifai kuliwa, lakini Watanzania wanakula. Hivyo hakikisheni inayoletwa iwe ni yenyewe kweli inayohitajika.

“Kuna mmoja alileta ‘Industrial sugar’ akasema ni ya kutengeneza Coca Cola, tulipo – calculate, tutakuta uwezo wake wa kutumia ni mdogo kuliko aliyoingiza.

“Kuna wengine wanaleta sukari kutoka nje na kubadili mifuko kwa kuweka ya Kagera Sugar. Hawa wanaosema wanaingiza industrial sugar, mpige mahesabu kama anazalisha kreti 100, ijulikane ni sukari kiasi gani inahitajika.

“Wasitumie ‘loopholes’ hii kuwauzia Watanzania ‘industrial sugar’,” alisema Rais Magufuli.

 

BEI YA SUKARI/MIWA

Rais Magufuli aliagiza bei za miwa zirekebishwe ili zilingane maeneo yote na kuondoa malalamiko kutoka kwa wakulima.

Alisema wakulima wa Mvomero mkoani Morogoro wamekuwa wakilipwa Sh 55,000 kwa tani moja ya miwa, lakini Kagera wamekuwa wakilipwa Sh 53,000 na kuzua malalamiko kutoka kwa wananchi.

Kuhusu bei ya sukari, Rais Magufuli alishangazwa na kuwapo kwa tofauti ya bei katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kagera, hasa Bunazi ambako wananchi wamekuwa wakiuziwa Sh 2,800 kwa kilo moja.

“Wananchi wamesema bei ya kiwandani ni Sh 2,000 hadi 2,200 kwa kilo, lakini Bukoba Mjini wanauziwa Sh 2,500 na Bunazi Sh 2,800.

“Huku ni kujenga chuki kwa wananchi wanaokaa karibu na kiwanda, walitakiwa wafaidi matunda ya kiwanda chenu kwa sababu baadhi ya watoto wao ndio wanashiriki kulinda rasilimali hii,” alisema Rais Magufuli.

Pia aliitaka menejimenti ya kiwanda hicho kuhakikisha mishahara ya wafanyakazi inalipwa kulingana na taaluma zao badala ya kuwapo kwa tofauti kubwa ya mishahara.

 

BOT

Rais Magufuli ameagiza kusitishwa kwa mkataba baina ya Benki Kuu (BoT) na Kampuni moja ya usafi ambao ulikuwa usainiwe kwa Dola za Marekani.

“Jana (juzi) saa 8 usiku niliuzuia, haiwezekani wao (BoT) ambao ndio wasimamizi wa fedha yetu halafu waingie mkataba kwa dola, atakayesaini mkataba huo ndio itakuwa siku yake ya kusaini kuondoka. Tuthamini fedha yetu, huo ndio uchumi,” alisema.

 

MIGOMO KAZINI

Rais Magufuli aligiza kuwe na usawa mahala pa kazi, lakini akatahadharisha tabia ya kuendekeza migomo kwamba itafika mahali itawakera wawekezaji.

“Wafanyakazi waache ulalamishi, mtu ni kibarua anataka apewe mkataba, kila siku migomo, mwekezaji atatengeneza faida lini? Atalipaje mkopo wake?

“Lazima wafanyakazi tujifunze kuvumilia, tutafika mahali tutaonekana nchi yenye fujo na Wizara ya Kazi isijifanye ni msemaji sana.

“Lakini wenye viwanda wasije wakalichukulia hili kama kigezo cha kutowapa wafanyakazi mikataba, lazima kuwe na usawa kwa ajili ya ‘win win situation’,” alisema.

 

WAZIRI MWIJAGE

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema kwa ardhi iliyopo nchini, uzalishaji sukari unaweza kufikia tani milioni 2 na kuna miradi 13 inaendelea ya uzalishaji bidhaa hiyo.

 

MWENYEKITI WA KIWANDA

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Sukari Kagera, Seif Seif, alimuhakikishia Rais Magufuli kwamba wataongeza uzalishaji wa sukari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here