23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JOTO LA UCHAGUZI MONDULI LAPANDA

Na MWANDISHI WETU-ARUSHA


JOTO la uchaguzi mdogo Jimbo la Monduli, limeanza kupanda baada ya baadhi ya viongozi wa CCM, kuonekana kupinga aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Julius Kalanga, kugombea tena nafasi hiyo kupitia chama hicho baada ya kujivua uanachama wa Chadema.

Waliojitokeza kumpinga Kalanga, wanahusishwa na aliyewania ubunge kwenye jimbo hilo mwaka 2015, Namelok Sokoine, ingawa mwenyewe amekanusha taarifa hizo.

Namelok ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alipotafutwa na MTANZANIA kuhusu hilo, alisema hajui chochote.

“Kuhusu hao wananchi ulioniuliza ambao umesema wanadai kanuni zifuatwe, hayo ni mawazo yao, sijui chochote kuhusu hilo, wafuate wao ukawaulize.

“Naamini unajua CCM inaongozwa na kanuni ambazo zinaelekeza mtu mmoja nafasi moja, sasa mimi tayari nina nafasi. Kwahiyo tayari siwezi kuingia kwenye nafasi hiyo. Kwahiyo hizo taarifa unazosikia huko hazina ukweli wowote,” alisema.

Kwa upande wake, Kalanga alisema; “sina cha kusema kwa sasa, nimejiunga na CCM na najua taratibu zitafuatwa, naheshimu hisia za wananchi, mimi si mgeni kwenye chama hiki, ndicho kilichonilea na kunijengea misingi yangu ya siasa.”

WANAOMPINGA KALANGA

Baadhi ya viongozi wa chama hicho kwenye ngazi za kata, walifika kwenye ofisi ya CCM Wilaya ya Monduli, wakipinga Kalanga kuteuliwa kuwania ubunge kwa tiketi ya chama hicho.

Mwenyekiti Kata ya Silalei, Hamis Abdallah, alisema hawatamkubali Kalanga wala kushirikiana naye, bali wanachokitaka ni kanuni na taratibu za chama zifuatwe.

“Kumekuwa na uminyaji demokrasia katika wilaya yetu ya Monduli, huyu ndugu yetu aliyekuwa upinzani akajiuzulu tunamkaribisha CCM, hatukatai, na kama anataka kuitumikia CCM, inawezekana kule alishindwa kutimiza sera ya CCM.

“Tunampokea, lakini tunachotaka sisi ni kanuni na sheria ya CCM zifuatwe. Kama anataka kuwa mgombea, aje kwa wananchi.

“Aje awaambie wananchi alishindwa kufanya nini akiwa nje, sasa yuko ndani anaweza kufanya. Lakini kinachotokea hapa hivi sasa, sisi tunasema hatutakubali na wala hatutashirikiana naye kama kanuni hazitafuatwa.

“Wanaoharibu taratibu na kanuni ni malaigwan, wanawabeba sana hawa watu kwa sababu wao wanachoangalia ni rika na si taratibu za chama zinasema nini.

“Sasa sisi tunasema kama kanuni hazitafuatwa, hatutafanya uchaguzi na hatutamtaka atutumikie sisi kwa sababu hafuati taratibu, kama aliweza kufanya huko nje hata huku anaweza akatuvuruga,” alisema Abdallah.

Naye Katibu wa CCM Kata ya Esilaley, Sairey Loboye, alisema mwanachama yeyote akijiunga na CCM kuna utaratibu wa kuchaguliwa na kuchujwa, lakini anashangazwa kwa taarifa walizopata kuwa Kalanga amepitishwa.

“Tunataka tujue utaratibu kama uligeuzwa ukawa mwingine, kwa sababu kupitia katiba yetu mwanachama yeyote akijiunga na CCM kuna utaratibu wa kuchaguliwa na kuchujwa, sasa kama tumeanza kusikia baadhi ya watu wameshanong’ona na kuanza kupitisha, wengine inatutia shaka,” alisema Loboe.

Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa Kata ya Sekeko, Noeni Nimise alisema; “tunamhitaji Mwenyekiti wa Wilaya ya Monduli kwa sababu kuna utofauti fulani unaotaka kutuingilia kwenye chama.

“Lakini pia tulimwamini Mwenyekiti wa Wilaya atuwakilishe sisi wananchi wake na tuliteseka wote pamoja katika uchaguzi uliopita. Hivyo tunamhitaji mwenyeki atuambie ukweli kuhusu haya ambayo yanaenea katika wilaya yetu ya Monduli.”

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Wilson Lengima, alisema hadi sasa hakuna mgombea yeyote aliyepitishwa na chama hicho kugombea ubunge.

“Niseme tu kwamba taratibu za CCM zinafuatwa na CCM ni chama ambacho kina taratibu zake, katiba na kanuni zote zitafuatwa kwa utaratibu ambao umewekwa.

“Mpaka dakika hii hatuna mgombea yeyote ambaye tumeweza kumpitisha na hatua ya wanachama kufika kwenye ofisi yangu na kulalamikia kuwa kuna mtu kateuliwa, nasema wazi kwamba bado wanachama waendelee kuwa wavulimivu, taarifa zitakuja kwa wakati na zikishafika tutawaambia utaratibu wote.

“Kwahiyo kwa sasa hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa, siku Kalanga aliporudi CCM baadaye kukawa na kikao cha malaigwan na mimi sijahusika na wala sijui chochote na wala chama changu hakijahusika,” alisema Lengima.

CUF YATAMBA

Wakati huo huo, Chama cha Wananchi (CUF), kinachotambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kimesema kimejipanga kuhakikisha kinashinda kwa kishindo katika uchaguzi wa marudio katika majimbo matatu na kata mbili uliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akizungumza na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Mneke Jaffar, alisema wagombea wengi wamejitokeza kuwania nafasi hiyo na ushindani ni mkubwa.

Alisema wanachosubiri ni kupiga kura za maoni ili waweze kuwachuja na kuwapata wagombea wenye sifa ili waweze kulitumikia taifa vyema.

“Hadi sasa wagombea ni wengi waliojitokeza kuwania majimbo matatu na kata hizo mbili, wengi wao wana sifa, hivyo ushindani ni mkubwa na tunachosubiri ni upigaji wa kura za maoni ili kuwapata wawakilishi sahihi na wenye sifa, ambao tunaamini watatuwakilisha vyema katika chaguzi hizo na tutashinda kwa kishindo,” alisema Jaffar.

Uchaguzi katika majimbo matatu ya Monduli, Ukonga na Korogwe Vijijini pamoja na kata 21, unatarajiwa kufanyika Septemba 15.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles