26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Joto la siasa lazidi kupanda Kenya

Isiji Dominic

PANDE mbili ndani ya chama tawala cha Jubilee zinazovutana zinamweka katika wakati mgumu Rais Uhuru Kenyatta kutekeleza ajenda nne kuu, pia zinaashiria dalili ya mpasuko ndani ya chama zikiwa imebaki takribani miaka mitatu kufanyika uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, wakati wa mazishi ya baba mzazi wa Seneta wa Igembe Kusini, Kaunti ya Meru, Mithika Linturi, Naibu Rais William Ruto licha ya kukiri hali sio shwari ndani ya Jubilee, aliwahakikishia wanachama kuweka mambo sawa.

Ni dhahiri joto la siasa linazidi kupanda nchini Kenya huku wanasiasa wakijipanga kuwania nafasi mbalimbali, lakini kikubwa kuegemea kwa mgombea wanayeona anazo dalili za kumrithi Rais Uhuru.

Historia katika uchaguzi mkuu nchini Kenya tangu mwaka 2002, zinaonyesha mwanasiasa anayewania urais anakuwa na mvuto zaidi ya chama anachogombea, ndiyo maana haishangazi ukiachia KANU, hakuna chama kinachotetea kiti cha urais isipokuwa mwanasiasa.

Jubilee inakabiliwa na mtihani huo kuelekea 2022 na ndani ya chama hicho kumeibuka kundi lililopachikwa jina la Tangatanga linalomuunga mkono Ruto, wakimuona anafaa kumrithi Rais Uhuru na kundi lingine linalojiita Kieleweke linalompiga Ruto.

Hivi majuzi, wanasiasa wa makundi haya mawili walisababisha vurugu katika nyumba ya ibada jambo ambalo lilimkera Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, ambaye alisema kitendo hicho kimeitia aibu chama cha Jubilee.

Kuria alidai mvutano ndani ya Jubilee kunawanufaisha upinzani na kuongeza kuwa wapinzani wao wakuu, Chama cha ODM, walifanya kwa amani mchujo wa kumpata mgombea wa uchaguzi mdogo jimbo la Kibra wakati ile ya Jubilee iligubikwa na vurugu.

Akikiri katika mazishi ya baba mzazi wa Seneta wa Igembe Kusini kuwa kuna mvutano ndani ya Chama cha Jubilee, Naibu Rais Ruto alimshutumu kiongozi wa ODM, Raila Odinga, akimtaja ndiye anayechochea.

Ruto aliwashutumu wanasiasa wanaoshinikiza mabadiliko ya katiba kwa maslahi yao binafsi kuwa ndiyo chanzo cha kuibuka makundi mawili ya Kieleweke na Tangatanga ndani ya Chama cha Jubilee.

“Ndiyo kuna mvutano ndani ya Jubilee inayochochewa na makundi ya kisiasa wengine wakitaka ‘punguza mizigo’ na wengine wakitaka ‘ongeza mzigo.’ Yote haya yameleta shida ndani ya Jubilee,” anasema Ruto na kuongeza:

“Nyote mnajua nini kinachotokea kuhusu masuala ya katiba. Mabingwa wa mabadiliko ya katiba wanajulikana. Hii sio biashara ya Jubilee lakini watu wengine wanaojulikana vyema na Wakenya.”

Ni kauli iliyotafsiriwa kulenga uhusiano kati ya Raila na Rais Uhuru iliyoleta ‘Building Bridges Initiative’ ambayo kwasasa imejifungia ikiandaa mapendekezo ya maoni ya wananchi waliokusanya nchi nzima na huenda ikatoa mwelekeo wa upigaji kura ya maoni kubadilisha katiba. 

Hata hivyo, Ruto aliwataka viongozi wasikate tamaa kwa sababu tofauti zilizopo ndani ya chama ni ndogo na zitatuliwa ikionekana ni jibu kwa Gavana wa Meru, Kiraitu Murungi, aliyelia na Jubilee kuwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) na inahitaji huduma ya haraka.

Kauli ya Kiraitu inaendana na ya Seneta wa Nairobi, Johnson Sakaja, ambaye katika mahojiano na moja ya runinga nchini Kenya, alisema Jubilee imevunjika na juhudi za kuifufua zinaonekana kushindikana.

“Jubilee haijakufa lakini inaumwa ina inaitaji matibabu ili ifufuke. Tulianzisha chama tukiwa na fikra kwamba miaka 20 baadaye bado itakuwepo lakini tofauti zimeibuka,” anasema Sakaja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles