31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Jitihada za Tanapa kulinda wanyama walio hatarini kutoweka

8NA SAID NJUKI, ARUSHA
TAFITI mbalimbali za ndani na nje ya nchi zinaonyesha idadi ya wanyama pori wakiwamo tembo na faru imezidi kupungua hali inayotishia uhifadhi endelevu wa maliasili zetu.

Baadhi ya tafiti hizo zinaonyesha kuwa zaidi ya tembo milioni 45 sawa na asilimia 90 ya tembo milioni 50 waliokuwapo barani Afrika mwaka 1930, wanasadikiwa kuuawa na majangili ikiwa ni miaka 83 tu. Sasa inasadikiwa tembo waliopo barani Afrika si zaidi ya 50,000.

Hapa nchini inaaminika kuwa mwaka 1960 kulikuwa na tembo kati ya 250,000 na 300,000, takwimu za mwaka 2002 zinaonyesha tembo hao walipungua na kufikia 130,000. Hata hivyo takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa tembo waliopo si zaidi ya 55,000.

Kwa takwimu hizo ni wazi kuwa tembo 850 huuawa kwa mwezi sawa na takribani tembo 10,000 wanaopoteza maisha kwa ujangili hali inayotishia kuwepo kwa wanyama hao wakubwa na adimu duniani.

Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), ndilo lenye dhamana ya uhifadhi wa wanyama nchini likiwa na hifadhi 16.

Miongoni mwa hifadhi hizo ni pamoja na Serengeti, Tarangire, Mikumi, Ruaha na hifadhi changa ya Mkomazi iliyopo mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.

Kwa baadhi tu ya hifadhi za taifa, Serengeti inaonyesha idadi ya tembo imepungua kutoka 2,500 mwaka 1985 hadi 500 mwaka 2012 huku nyati wakipungua kutoka 70,000 hadi 40,000 katika kipindi hicho.

Lakini mbaya zaidi hata wanyama adimu duniani faru nao walipungua katika hifadhi hiyo kipindi hicho toka 1,000 hadi faru 20 tu. Hizo ni takwimu za hifadhi moja tu ya Serengeti hatujazigusa hifadhi zingine kama Tarangire.

Shukrani za dhati kwa jitihada zinazofanywa na Serikali, taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, huku mataifa makubwa duniani kama Marekani yakisaidia mapambano dhidi ya ujangili huo.

Jitihada hizo ndizo zilizofanikisha kuwapo kwa ndege aina ya MLB Super-Bat DA-50 yenye uwezo wa kupiga picha usiku na mchana isiyokuwa na rubani, inayoendeshwa kwa mitambo maalumu ya kompyuta. Ni hatua kubwa zinazostahili pongezi.

Lakini pia pamoja na ulinzi huo wa kutumia ndege, Tanapa imejipanga kuhakikisha idadi hiyo ya wanyama hao na wengine walioko katika hatari ya kutoweka duniani haipungui kwa gharama yoyote.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, anasema hifadhi nyingi bado zipo katika uoto wa asili licha ya baadhi ya wanyama kupungua.

“Wengine wapo katika tishio la kutoweka lakini tumejipanga kuhakikisha wanyama wetu walioko katika hatari hiyo kama tembo, faru, mbwa mwitu na wengine wanabaki salama kwa gharama zozote,”anasema Kijazi.

Anasema shirika linafahamu maisha ya wanyama wanaoishi kutokana na hatari ya ujangili, ndiyo sababu wanakwenda vizuri katika uhifadhi kwani takwimu zinaonyesha kupungua kwa kiasi kikubwa cha matukio ya kiujangili katika hifadhi hizo.

Kijazi anasema katika kuhakikisha wanfanikiwa kiuhifadhi tayari wanayo miradi maalumu ya faru na mbwa mwitu katika Hifadhi za Serengeti na Hifadhi ya Mkomazi lengo likiwa ni kulinda na kuendeleza vizazi vya wanyama hao adimu duniani.

Anawataka wananchi hasa wale wanaoishi jirani na hifadhi hizo kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa maliasili hizo hususan wanyama kwa faida ya jamii na taifa kwa ujumla, kwa kuwafichua majangili huku akiwahakikishia kuwa maliasili hizo ni mali zao.

“Tumekuwa tukishirikiana na jamii jirani na hifadhi katika ulinzi wa wanyama wetu kwa kutoa elimu juu ya uhifadhi sanjari na kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kuonyesha ni kwa kiasi gani hifadhi hizi ni mali yao,”anasisitiza.

 

Hifadhi ya Mkomazi

Moja ya hifadhi zinazopiga hatua kiuhifadhi endelevu ni pamoja na Mkomazi hifadhi ambayo ilianza mwaka 2008 baada ya Pori la Akiba la Mkomazi-Umba kupandishwa hadhi na kuwa hifadhi kamili.

Mhifadhi Mwandamizi wa hifadhi hiyo, Angela Nyaki, anasema licha ya hifadhi hiyo kuwa change na ukame unaoikabili lakini imepiga hatua kubwa za kiuhifadhi na kuaminika kuwa na mradi nyeti wa faru na mbwa mwitu.

“Hifadhi ya Mkomazi inayo sehemu ya uoto wa asili wa ‘sahel’ yaani jangwa kwa lugha ya kiarabu, uoto unaowakilishwa na mimea aina ya acacia-commiphora ambapo katika Afrika Mashariki huishia katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

“Uoto huu umegawanyika katika makundi mawili, misitu mikavu ya nyanda za juu iliyoko magharibi mwa hifadhi na mbuga zenye vichaka vidogo na nyasi za uwanda wa chini wa hifadhi hali inayoifanya hifadhi kuwa na kitu tofauti na hifadhi zingine,” anasema Angel.

Pia anaishukuru jamii wanayopakana nayo kwa ushirikiano wao kwani wamekuwa msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya majangili kuingia hifadhini na kufanya ujangili wao.

Neno Mkomazi linatokana na maneno mawili ambayo ni ‘Mko’ na ‘Mazi’ kwa lugha ya kipare yaliyounganishwa pamoja ‘Mko’ yenye maana kijiko kidogo cha asili cha mti na ‘mazi’ lenye maana ya maji yakiimanisha maji yanayopatikana kwenye hifadhi hiyo ni kidogo kuweza kujaza kijiko.

Hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 1951 kama pori la akiba likiwa limetengwa kutoka katika pori kubwa la akiba la Ruvu.

Hifadhi ina ukubwa wa kilometa za mraba 3,245 na kwamba pori hilo lilipendekezwa kuwa hifadhi ya taifa kwa misingi ya kunusuru maeneo na rasilimali zilizomo kutokana na matumizi yasiyoendana na uhifadhi kwa ajili ya kizazi kijacho.

Mbali na wanyama, zipo takribani aina 450 za ndege wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja faru weusi walioingizwa kutoka kutoka nchi za Afrika kusini na Uingereza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles