31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JITENGE NA MATATIZO USONGE MBELE KIMAFANIKIO – 2

Na ATHUMANI MOHAMED

ELIMU kuhusu mafanikio haina mwisho. Kila siku tunapaswa kujifunza. Tunapaswa kupanua mawazo yetu mara kwa mara ili kujua namna ya kujitanua kimafanikio.

Kwa asiye nacho ni nafasi yake ya kujifunza mbinu za kupata lakini hata kwa yule ambaye tayari anacho, anatakiwa kujifunza namna ya kulinda kile alichojaaliwa. Hiyo ndiyo sababu nimesema elimu ya mafanikio haina mwisho.

Kama jana umejifunza, leo unatakiwa kujifunza tena na hata kesho pia uendelee kujifunza. Katika mada hii ambayo leo ni sehemu ya mwisho tunajifunza vitu au mambo ya hatari ya kukaa nayo mbali ili kujisogeza kwenye mafanikio.

Ndugu zangu, tukubali au tukatae kuna vitu au mambo ambayo ukiwa nayo karibu basi unajiweka kwenye hatari ya kuingia kwenye matatizo ambayo yatakuchelewesha au kukusababishia ushindwe kutimiza malengo yako ya mafanikio.

Ni kweli matatizo yapo kila siku na kuna wakati tunaweza kusema matatizo hayana taarifa, lakini kuna mengine ni kama tunajitakia wenyewe. Hapa tunajifunza yale ambayo tunapaswa kukaa nayo mbali ili tusizibe mianya ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio kwenye maisha yetu.

Lakini nieleze jambo moja kubwa ambalo wengi wanalipuuza; tusibweteke, tusake maisha kwa nguvu zote. Vijana wengi kwa mfano wenye degree zao hawataki kusikia kazi ambazo siyo zenye hadhi.

Wanataka kazi za ofisini tu. Sawa, umesomea labda mambo ya masoko, lakini mbele yako kuna kazi nyingine hata kama siyo ya ofisini lakini inalipa, kwanini usifanye kuliko kusubiri hiyo ya ofisini ambayo huna uhakika nayo leo?

Hili somo nitalifafanua vizuri siku zijazo ambapo nitajitolea mfano mimi mwenyewe ambaye nimekubali kuweka degree yangu ndani na kujiajiri kwenye ujasiriamali.

Sasa kwa leo tunamalizie somo letu, jiandae kwa somo hilo kwa undani wiki ijayo.

 

FUATA SHERIA ZA NCHI

Ni vizuri sana kufuata sheria za nchi, maana tunaongozwa na utawala wa sheria. Ukivunja sheria maana yake unajiweka kwenye matatizo na kitakachofuata ni kushitakiwa mahakamani.

Yapo makatazo ya wazi kisheria, mfano kuna watu wanaohangaika na wanafunzi, wakati sheria inazuia na wanajua wazi kuwa ukitiwa hatiani miaka 30 jela inakuhusu. Ni jambo la hatari. Kwanini uyatafute matatizo?

Mtu mzima, una familia yako lakini unahangaika na watoto wa shule, kwanini? Au mwanafunzi yupo shule lakini akili yake iko kwenye mapenzi. Huko ni kujiharibia maisha yako yajayo. Tayari Rais Magufuli ameshasema, mwanafunzi ukipata mimba, hurudi tena shuleni. Kwanini ujitakie matatizo ya namna hiyo?

Ishi kwa kuzingatia mambo ya msingi, ujijali mwenyewe na maisha yako yajayo. Mafanikio ni safari, lazima ukae mbali na vizingiti.

 

KUWA MAKINI NA MADENI

Mikopo inaweza kukusaidia kufanikisha baadhi ya mipango yako, lakini inakupasa uwe nayo makini sana. Kukopa sana au kukopa fedha nyingi nje ya uwezo wako ni hatari.

Kabla ya kukopa, tafakari kuhusu marejesho. Je, ni kweli utaweza kurudisha mkopo wako bila kuathiri mipango yako mingine? Kudaiwa sana kunaweza kukurudisha nyuma.

Lakini lenye umuhimu zaidi ni kwamba kopa fedha kwa ajili ya kuzalisha. Ukizalisha inakuwa rahisi kurejesha, ingawa unaweza kukopa kwa ajili ya kununua aseti ila uwe makini na marejesho yasiwe makubwa juu ya uwezo wako na kukusababishia matatizo yatakayokurudisha nyuma.

Maisha hayawezi kusonga bila kutumia akili nyingi, kufanya mambo kwa akili na maarifa ni bora na muhimu zaidi. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.

Ni mimi rafiki yako katika mafanikio, Athumani Mohamed. Wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles