23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JITENGE NA HATARI YA USALITI USIOTARAJIA

Na JOSEPH SHALUWA

NI kweli mapenzi hayana kanuni lakini yapo mambo ambayo kama hutakuwa nayo makini yanaweza kuharibu historia ya maisha yako na ukajutia.

Mapenzi ni hisia, unapokuwa na mtu ambaye unampenda ni kwamba moyo wako umeridhia kwa dhati kumpenda na kumfanya wako wa maisha.

Wakati wewe ukiwa na mapenzi ya dhati kwa huyo unayempenda ni wazi kuwa hata yeye anakupenda kwa dhati. Unapaswa kulinda penzi la mwenzako sanjari na wewe kuheshimu hisia zako za ndani.

Kuna mtindo siku hizi umekuja kwa kasi sana hasa kwa vijana wa kileo. Naweza kusema teknolojia ndiyo inayotupeleka kwa kasi, maana hii mitandao ya kijamii sasa naona imeanza kutumika ndivyo sivyo.

Wapo wadada ambao wapo kwenye uhusiano, lakini wanajikuta wakijiingiza kwenye uhusiano mpya na kuwasaliti wenzi wao bila kujijua.

Siyo kwamba anaanzisha uhusiano akiwa anajua, hapana. Inatokea kama ajali, lakini yeye anakuwa chanzo cha ajali hiyo.

Ukichilia mbali wadada walio kwenye uhusiano bila ndoa, wapo wengine wapo  kwenye ndoa kabisa, lakini wametekwa na kujikuta wakiingia kwenye matatizo bila kutarajia.

Katika mada hii nitafafanua kwa kirefu kisha utaangalia kuwa upo kwenye kundi gani na kuchukua hatua.

CHANZO CHA TATIZO

Tatizo ni teknolojia kama nilivyoanza kusema hapo juu. Mawasiliano ya mitandao ya kijamii yamewaingiza wengine kwenye matatizo.

Mitandao ya kijamii kama Instagram, WhatsApp, Facebook na mingine imekuwa chanzo kikubwa cha matatizo haya. Utakuta mtu yupo kwenye group fulani la WhatsApp kwa nia njema kabisa na anabadilishana mawazo na memba wenzake vizuri tu.

Tatizo linakuja pale anapokutana na wasio waaminifu ambao wataanzisha ukaribu nje ya uwanja wa wazi (inbox) na kuanza kupiga soga za hapa na pale.

Na hili naomba nieleweke wazi mapema, siyo kwamba wanaokutana na changamoto hii ni wanawake pekee, hata wanaume.

Unakuta msichana anamfuata mvulana inbox na wanaanza kuchat siku hadi siku. Katika mazungumzo yao kipindi cha kwanza huwa ya kawaida kabisa.

Hujadili mambo mbalimbali yanayotokea kwenye jamii kama soka, filamu, siasa na mengine mengi. Baadaye hufuata utani na vibonzo vya kawaida na mwisho huja sasa vibonzo vyenye viashiria vya mapenzi.

Hadi kufikia hapo, mhusika mwenye kulenga mtego wake hupima na akiona amepenya pote huko ndipo anapoingiza nia yake. Kumbuka, mtu huyo anavyoingia huwa amejipanga sawasawa.

Anayo majibu ya kila swali na ameshajua vipimo vyake, kwa maana hiyo hata kama anajua upo kwenye uhusiano na mtu mwingine au ni mke au mume wa mtu, kwake siyo tatizo.

WENYE UHUSIANO

Ni muhimu kuwa makini na marafiki wa jinsia tofauti na yako hasa kama upo kwenye uhusiano. Kwa kawaida mapenzi huhitaji muda. Hata kama upo na rafiki ambaye huna hisia naye kabisa za mapenzi, ukaribu wenu wa muda mrefu huweza kuchangia kuanzisha uhusiano.

Kuna haja gani ya kuingia kwenye matatizo ya namna hiyo? Kama unajua wazi upo kwenye uhusiano ni vizuri kulinda penzi la mwenzi wako lakini pia kuheshimu hisia zako.

Usipende mazoea yasiyokuwa na maana kwa mtu ambaye huna haja naye. Ukifuatwa inbox na stori usizozielewa acha kuchekacheka, onyesha msimamo wako.

Jibu lako la kwanza litatoa picha ya msimamo wako ulivyo na akishaujua atajiweka pembeneni.

Haiwezekani unachati na mtu ambaye si mpenzi wako, mmefikia hadi hatua ya kuitana baby, sweet, halafu ukiulizwa unasema ni rafiki tu! Hakuna urafiki wa namna hiyo.

Ilivyo ni kwamba, wengi wa staili hiyo huwa hawana mapenzi ya dhati au niseme siyo serious kwenye mapenzi hivyo hutumia mwanya wa mitandao ya kijamii, kujaribujaribu kila atakayejipendekeza kwake.

Kwanini uruhusu kujaribiwa?

WENYE NDOA

Kwa walio kwenye ndoa ndiyo hatari zaidi. Hawa ndiyo wanaotakiwa kuwa makini zaidi na mazoea yasiyofaa na watu wa jinsia nyingine wanaojisogeza kwao.

Ukijiheshimu hutakubali mazoea yasiyo na staha kwa watu wanaoonekana wazi wana nia ovu kwenye maisha yako ya uhusiano.

Kuwa na msimamo. Usiharibu ndoa yako kwa sababu ambazo zinazuilika. Narudia tena, asimilia kubwa huwa hawana lengo la kusaliti ila baada ya kutekwa na mazingira hujikuta kwenye wakati mgumu.

Joseph Shaluwa ni mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano, unaweza kusoma mada zake zaidi kupitia vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vilivyopo mitaani. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles