25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Jinsi ya kumtambua rafiki msaliti

Na CHRISTIAN BWAYA

MAKALA iliyopita tulizungumzia umuhimu wa kuwa mwaminifu kabla ya ndoa. Tulisema mchumba asiyeweza kujizuia kabla ya ndoa, itakuwa muujiza akiweza kujizuia akiwa kwenye ndoa. Hujakosea kusoma, rudia. Ingawa ni kweli yapo mambo mengi yanayochangia watu kuwa na michepuko, ambayo hata hivyo si mjadala wa leo, lakini sababu inayoongoza ni historia ya mtu.

Unapokuwa na rafiki asiyejua wapi pa kuishia katika uhusiano wenu, usitegemee atajifunza mipaka hiyo mtakapoingia kwenye ndoa. Najua wakati mwingine unaweza kufurahia kufanya kosa na mtu ambalo usingependa alifanye na mtu mwingine. Lakini unapofanya makosa hayo, fahamu kuwa unatengeneza msingi mbaya kwa maisha yenu ya baadae. Ikiwa hupendi kuwa na mume/mke asiye na utaratibu, mtu anayeanzisha uhusiano na kila anayekutana naye, usikubali kuingia kwenye ndoa na mtu anayefikiri ngono ndio kipimo kikuu cha upendo. Haya si mawazo yangu bali tafiti zinaonesha hivyo.

Nawafahamu wanandoa wengi wasioaminiana. Mume hawezi kumruhusu mke wake aishi maisha yake kama binadamu huru. Hapa namaanisha tabia ya kuchungana inayovuka mipaka kwa sababu tu kuna mtu anafikiri mwenzake akiwa huru lolote linaweza kutokea. Tafiti za uhusiano zinaonesha kuwa mara nyingi watu wenye historia ya maisha yasiyo na nidhamu kabla ya ndoa ndio hasa huongoza kutokuaminiana wanapoingia kwenye ndoa. Tafsiri yake ni kwamba kama unatamani kuishi na mume au mke anayekuamini na atakayekupa uhuru wako bila kuwa na shaka isiyo na sababu, ishi maisha yenye nidhamu kabla ya ndoa.

Upande mwingine wa uaminifu ni uwezo wa mtu kulinda urafiki katika mazingira yoyote. Neno linalobeba maana kamili ni ‘loyalty’ kwa Kiingereza. Uaminifu, katika mukhtadha huu, ni ile hali ya mtu kuwa na imani na mtu mwingine bila wasiwasi kuwa mtu huyo anaweza kumsaliti. Usaliti ni tabia ya kuuza siri za mtu aliyekuamini kwa watu wasiohusika kwa sababu mtu huyu hana uaminifu. Kumsema mtu aliyekuamini kwa sababu hayupo huo unaitwa ni usaliti. Usaliti unaweza kueleweka kama tabia ya kushindwa kumtetea mtu aliyekuamini hata katika mazingira unayojua kuwa yeye mwenyewe hatafahamu ulichokifanya.

Ndoa, kimsingi, ni muunganiko wa watu wawili wanaopaswa kuaminiana kwa kiwango cha juu sana. Kuaminiana kunapokosekana, uwezekano wa migogoro huwa ni mkubwa zaidi. Swali utajuaje kuwa unayetaka kuingia naye kwenye ndoa hatakuwa mwaminifu kwako? Tutumie mfano rahisi, chukulia una mchumba anayeweza kuthubutu kueleza upungufu wako kwa watu wengine, bila taarifa yako. Fikiria rafiki yako wa karibu unayemwamini anaweza kuzungumzia matatizo yako kwa rafiki zake/zenu bila ridhaa yako. Hii ni mifano ya dalili kwamba uliyenaye ana tatizo la uaminifu kwako.

Uaminifu wa mtu kwako unategemea kiwango chake cha ukomavu. Fikiria mazingira ambayo mume/mke wako hawezi kuamua jambo bila kwanza kuwasiliana na wazazi au ndugu zake. Fikiria mazingira ambayo mume/mke wako anaweza kukuweka pembeni na kufanya uamuzi anaojua si sahihi kwa sababu tu anaogopa kuwaudhi ndugu zake. Ukweli wa mambo ni kwamba huwezi kuwa na ndoa imara kama hujajua kusimamia mipaka yako na wazazi na familia yako. Ukiruhusu familia yako iendelee kuongoza uamuzi wako baada ya ndoa unakaribisha matatizo.

Unapojiandaa na ndoa, ni muhimu kuangalia uhusiano wake na familia yake. Je, anaweza kujisimamia mwenyewe bila kutegemea aambiwe nini cha kufanya na wazazi? Je, anaweza kusema hapana kwa jambo analojua si sahihi hata kama kufanya hivyo ni kinyume na matarajio ya watu wake wa karibu? Mtu ambaye anaweza kuwa tayari kufanya lolote kwa sababu tu ndilo linalotakiwa na familia yake huyo bado anahitaji muda zaidi wa kukomaa. Sisemi tuwe na uhusiano mbaya na familia zetu wala tusiwashirikishe ndugu zetu mambo yanayotuhusu. Ukinielewa hivyo pengine unahitaji kurudia aya hii. Ninachozungumzia hapa ni uwezo wa mtu kujisimamia bila utegemezi uliopindukia kwa wazazi au ndugu.

Pengine una bahati na hujasikia akikusaliti kwa watu wake wa karibu. Hiyo haitoshi kukuaminisha kuwa atakuwa mwaminifu kwako. Jiulize, anaweza kuficha siri za wengine? Je, anaweza kujizuia kuzungumzia siri za watu wake waliomwamini? Unapokuwa na rafiki mwenye tabia kuvunja makubaliano yake na watu waliomwamini, mtu anayeweza kukueleza siri za watu wengine wa karibu yake, ambao wasingependa siri hizo zifahamike, hapo jua kuna tatizo.

Ingawa kwa haraka unapoambiwa mambo ya watu unaweza kufikiri umeaminiwa na umekuwa mwandani wake, usifurahie tabia hii hatari. Wahenga walisema ukiona wengine wananyolewa, zako tia maji. Usikubali kuaminiwa na mtu asiyejua kuwaheshimu waliomwamini.

INAENDELEA

Christian Bwayani Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Kwa unasihi wasiliana naye kwa0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles