27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JINSI YA KUMSAIDIA MTOTO ANAYEKOSA CHOO

Na MWANDISHI WETU


KWA kawaida watoto wadogo hasa wale ambao bado wananyonya na ndio kwanza wameanza kula vyakula vingine zaidi ya maziwa, hupatwa na choo kigumu au kukosa kabisa hali ambayo kitaalamu huitwa constipation.

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema kuwa hali hiyo huanza pale mtoto anapoachishwa maziwa ya mama na kuanza kunywa maziwa ya kopo au ya ng’ombe.

Mara nyingi watoto wanaonyonya maziwa ya mama huwa hawasumbuliwi na tatizo hilo.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa kwa mama ambaye anasumbuliwa na tatizo la kukosa choo, huenda mwanawe pia akasumbuliwa na tatizo hilo.

Mtoto mwenye tatizo la kukosa choo mara nyingi hupata choo kigumu tena kwa shida huku akisumbuliwa na maumivu ya tumbo.

Hali hii pia huchangia wakati mwingine hulia wakati akipata choo huku akijiminya na kukunja uso.

Unachotakiwa kufanya pindi unapoona hali hii ni kumuona daktari, iwapo mtoto ana umri wa chini ya mwezi mmoja na hajapata choo kwa siku nne.

Kwa mama ambaye mtoto wake ni mchanga au mdogo ana tatizo la kukosa choo au kupata choo kigumu, anapaswa kuwasiliana na daktari au kumpeleka hospitali ili kupata ushari wa kitaalamu.

Huduma ya kwanza unayopaswa kumpatia mtoto ni kumpa maji safi na salama kuanzia mililita 60 hadi 120 kwa siku, punguza au ongeza kiasi hicho kwa kuzingatia jinsi hali ya mwanao inavyokuwa.

Iwapo maji hayatasaidia, jaribu kumpa juisi za matunda kama tufaa (apple), iliyotengenezwa kwa kutumia maji safi.

Anza kwa mililita 60 hadi 120 kwa siku na punguza au ongeza kiasi hicho kwa kuzingatia jinsi hali ya mwanao inavyokuwa.

Njia nyingine ni kujitahidi kumpa chakula chenye ufumwele au fiber, iwapo mwanao ameanza kula vyakula vigumu, basi mpe vyakula vyenye ufumwele kuliko vyakula vyenye wanga, kama vile kutumia unga wa shayiri au tunda la tufaa na peasi lililopondwa pondwa vyema na kuwa kama uji.

Pia inashauriwa kuepuka kumpa mtoto uji wa mchele kama anatatizo la kukosa au kufunga choo.
Jenga utaratibu wa kumpaka mafuta kidogo sehemu ya haja kubwa ili kurahisisha utokaji wake. Usitumie mafuta ya madini (mineral oil) au dawa za kulainisha choo na za kuharisha katika kutibu tatizo hilo.

Muone daktari au mpeleke mtoto wako hospitalini kama tatizo hilo la kukosa choo linaendelea hata baada ya kubadilisha aina ya chakula cha mtoto au linaambatana na dalili nyingine kama vile kutapika au mtoto kukosa utulivu na kuhangaika.

Inaelezwa kuwa kuna baadhi ya watoto wanakosa au kuwa na choo kigumu kutokana na kutumia maziwa ya ng’ombe.

Lakini pia iwapo umetumia dawa na umefuata maelekezo ya kuondoa ukosefu wa choo na hukufanikiwa, sitisha kumpa mtoto maziwa ya ng’ombe kwa siku mbili au tatu, baada ya siku hizo iwapo bado hajapona endelea kumpa maziwa huenda tatizo hilo halisababishwa na maziwa ya ng’ombe.

Njia nyingine ni kumwogesha au kumweka mtoto katika beseni la maji ya uvuguvugu na hakikisha maji yanafika hadi kifuani. Mkande mtoto tumbo lake wakati akiwa kwenye maji, njia hiyo husaidia kulegeza misuli ya mwili wa mtoto na kumsaidia kupata choo kwa urahisi.

Utafiti unaonyesha kuwa hakuna uhusiano wowote kuhusu kukosa choo mtoto na kupewa nyongeza ya chuma au ‘iron supplement.’

Hivyo, usimkatishe kumpa mwanao chuma iwapo anakosa choo kwa kuwa ni muhimu katika kuzuia upungufu wa damu mwilini. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles