25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JINSI UTAKAVYOWEZA KUMGUNDUA MPENZI KATILI

Na Christian Bwaya


MATUKIO ya watu kuuawa na wapenzi wao yameshamiri katika siku za hivi karibuni. Juzi tulisikia taarifa za kusikitisha za mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma, Rose Mndenye, kuuawa kwa kuchomwa kisu na mumewe. Sababu iliyotajwa ni wivu wa mapenzi. Marehemu aliacha mtoto mmoja mdogo wa umri wa mwaka mmoja na nusu.

Siku chache kabla, tulisikia taarifa za mwanamke aitwaye Rosemary Magombora aliyepigwa na mume wake mpaka kufanakisha mwili wake kufukiwa katika shimo lililokuwa jirani na nyumba yao. Inadaiwa mume huyo aliambukizwa Virusi vya Ukimwi na marehemu.

Katika hali isiyo ya kawaida, Aprili 27, mwaka huu, vyombo vya habari vilitangaza taarifa za mwenyekiti wa kitongoji cha Kikonda, mkoani Kagera, Salvatory Tiganyila, aliyeuawa kikatili na mkewe kwa kumpiga na kitu kizito kichwani. Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza chanzo cha tukio hilo.

Hayo si matukio ya kawaida kutokea kwenye jamii ya watu wastaarabu na ni hatari kuzoea habari za namna hii. Kushamiri kwa matukio kama haya ni dalili ya tabia za kikatili zinazoendelea katika jamii zetu lakini pengine hazigongwi vichwa vya vyombo vya habari.

Tunafahamu, kwa mfano, wapo wapenzi wengi wanaonyanyaswa na kuonewa majumbani lakini habari zao pengine hazifikii kiwango cha kutangazwa kwenye vyombo vya habari. Inawezekana, kama jamii, tumeanza kuyachukulia matukio haya kama sehemu ya maisha ya kawaida katika familia.

Kufuatia matukio kama haya ya kikatili yanayofikia hatua ya kuchukua uhai wa watu, kuna ulazima wa jamii kwa pamoja kuchukua hatua za kudhibiti hali hii. Hatua ya kwanza, nafikiri ni kujielimisha namna ya kuwatambua wapenzi wenye tabia hatarishi. Katika makala haya tunaangalia ishara tatu za mpenzi anayeweza kuwa na tabia za kikatili.

Unaweza kuwa na mpenzi mwenye tabia ya kutumia mabavu katika kutatua mambo yake. Huyu hakupigiwa la kugusa mwili wako akuumize lakini anao uwezo mkubwa wa kuumiza hisia zako. Mtu kama huyu anaweza kuwa na hasira kali sana ukimkosea. Mnapopishana mawazo anapandwa na hasira kali kiasi kwamba anaweza kufanya kitu kisichoingia akilini. Kuna vitu kama kutukana matusi ya nguoni, kusema maneno makali yanayo dhalilisha utu wa mtu mwingine na hajisikii hatia.

Mtu wa namna hii ni mwepesi kusema maneno kama ‘nitakuua’, ‘nitakumaliza’ hata kama anaonekana hamaanishi. Unaweza kumkosea akakasirika na akakwambia, ‘Kuna siku nitakuua kwa ujinga wako. We endelea.’ Hasira zikipoa anaweza kujutia kile alichokifanya lakini siku nyingine unashangaa anafanya yale yale. Usichukulie kirahisi unapoona mwenzako yuko hivi. Hiki anachokisema kimejificha kwenye ubongo wake. Ndicho anachokiamini hata yeye mwenyewe hana habari.

Pia, kuna mpenzi mwenye tabia ya kutokusahau. Huyu anaweza kuwa mtu mkimya. Ukimkosea analalamika, hakupigi wala hakutukani, lakini haonekani kusamehe. Mtu wa namna hii unaweza kumtaka mzungumze myamalize, lakini akakukatisha kuwa mambo yameisha. Kwa namna anavyoongea unaweza kumwamini lakini ukimkosea kesho atakukumbusha kosa la jana na juzi, hasahau.

Kukosa msamaha ni dalili mbaya. Mtu anayeweka mambo moyoni anao uwezekano wa kufanya jambo baya baadae. Unajua, wakati mwingine kuongea kile kinachokunyima amani kunaondoa sumu moyoni. Kadiri unavyoongea ndivyo unavyosafisha moyo wako. Mtu asiyetaka kuongea pale mnapokosana anaweza kukufanyia kitu kisichokuwa cha kawaida bila wewe kutarajia.

Lakini pia kuna tabia ya ugomvi. Unapomkosea mtu mgomvi, ni mwepesi kukupiga kibao, kukusukuma uanguke na hata kukurushia ngumi. Usichukulie kawaida, kuna watu wakikasirika wanaweza kuvunja vunja vitu vya ndani. Huyu anaweza kuona kitu asichokitarajia kwenye simu yako akaivunja. Unamkosea na anarusha rusha vitu ndani ya nyumba, unabaki kushangaa inakuwaje?

Mpenzi mgomvi anaweza asiwe mgomvi kwako lakini anaonesha ugomvi kwa watu wengine au vitu. Unaweza kuwa na mpenzi anayekupenda sana na hajawahi kukugusa lakini anakawaida ya kupiga watoto kipigo kisicholingana na makosa yao. Huyu ni mtu anayeweza kumfunga kamba mtoto na kumwacha alale barazani kwa sababu tu ameiba fedha ya mafuta ya taa ndani.

Ukiona dalili kama hizi kwa mpenzi wako, usipuuze. Kama ni mchumba wako, usifikiri kuna siku atabadilika. Chukua hatua, kama ni mwenza wako wa ndoa.

 

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754870815

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles