33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Jinsi mabilioni yalivyochotwa

MTZ Alhamisi new july.inddFredy Azzah, Dar es Salaam

WAKATI Watanzania wakiumiza kichwa kujua watu waliofaidika na rushwa ya Sh bilioni 12 (dola za Marekani milioni 6), zilitokana na mkopo wa dola za Marekani milioni 600 (Sh trilioni 1.3), ambao Tanzania iliomba kwenye Benki ya Standard kupitia mshirika wake Stanbic Tanzania, imebainika kuwa mchakato ulianza mwaka 2011 na kushirikisha watu mbalimbali wakiwamo maofisa wa Serikali na watoto wao.

 

KESI ILIVYOANZA

Mwenendo wa kesi iliyotolewa hukumu Novemba 30 nchini Uingereza, unasema tangu mwaka 2011 Serikali ya Tanzania ilifanya juhudi za kupata mkopo wa miradi ya miundombinu kupitia soko la kimataifa la hati fungani bila mafanikio kutokana na kile kilichoelezwa ni kukosa vigezo.

Mwenendo huo unasema, benki ya Standard na Stanbic kwa pamoja zikachukua jukumu la kutafuta mkopo huo kwa Serikali ya Tanzania kupitia waziri wa fedha wa wakati huo ambaye alikuwa Mustafa Mkulo.

“Pendekezo lilikuwa Standard na Stanbic iwasilishe wazo la kuiwezesha Serikali kupata mkopo, na lilikuwa liwasilishwe kwa waziri wa fedha kwa sharti kwamba Standard na Stanbic kwa pamoja zipokee ada ya asilimia 1.4 kwa kuandaa na kuwezesha mkopo huo.

“Standard na Stanbic zilisema kwamba wazo lao hilo litauzwa kama mchakato binafsi kwa mujibu wa sheria na mwongozo wa usalama wa Marekani,” unaeleza mwenendo huo wa kesi.

Katika barua pepe ya Februari 25, 2012, Kaimu Mkuu wa Masuala ya Uwekezaji wa Stanbic, Shose Sinare, aliwafahamisha watu fulani ndani ya Standard na Stanbic, akiwamo Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji wa Standard na Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic, kwamba wazo lao limekubaliwa na waziri wa fedha.

Kwa herufu kubwa na maandishi manene, Sinare ambaye kwenye mwenendo wote huo ametajwa kwa nafasi yake bila kugusia jina lake, alibainisha kwamba watapata asilimia 1.4 kama ada ya kuwezesha mpango huu kwa Serikali ya Tanzania.

Mwenendo huo unasema kuwa Mei 2012, kabla ya wazo la mpango huo kusainiwa, Waziri wa Fedha, Mkulo aliondoshwa na nafasi yake kuchukuliwa na waziri mwingine (Dk. William Mgimwa).

“Kuanzia Mei 2012 kuelekea mwishoni mwa mwaka 2012, Standard na Stanbic zilijaribu kufufua mpango huo kupitia juhudi zilizofanywa na Sinare na Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic (Bashir Awale), ambao walikutana na maofisa wa Serikali nchini Tanzania.

Mkuu wa Kimataifa wa Madeni ya Mitaji ya Masoko alikuwa akifahamishwa hatua kwa hatua ya maendeleo hayo na Standard, pamoja na timu ya ndani ya ushauri iliyohusika kuandaa nyaraka za mpango huo.

Juni 2012, Sinare aliwasilisha kwa ofisi ya Waziri wa Fedha  nakala ya mpango huo, ukiendelea kuonyesha Standard na Stanbic kwa pamoja kama maneneja viongozi wa mpango huo, wakitarajia kupokea ada ya asilimia 1.4 ya sehemu ya mkopo huo.

 

MTOTO WA WAZIRI ALIVYOAJIRIWA

Julai 2012, Stanbic ilimuajiri mtoto wa kiume wa waziri huyo mpya wa fedha.

Agosti 29, 2012, Sinare alimwandikia barua pepe Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji wa Standard, kwamba yeye na Bashir wamefikia ‘mahali pazuri’ baada ya mkutano mzuri na Waziri wa Fedha na timu yake, na kwamba kwa sasa wako katika mwelekeo mzuri wa kusaini makubaliano ya mpango huo.

Mwenendo wa kesi hiyo unasema Sinare pia alimfahamisha Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji wa Standard, kwamba mkutano na Waziri wa Fedha ulithibitishwa utafanyika Septemba 18.

“Septemba 4, Kaimu Mkuu wa Uwekezaji wa Benki ya Stanbic (Sinare) alimtumia Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic (Bashir) na mtoto wa kiume wa Waziri wa Fedha pendekezo la mpango wa kutafuta mkopo, na kumtaka mtoto wa Waziri wa Fedha kuziwasilisha nyaraka kwa Ofisi wa Waziri wa Fedha, kitu alichofanya siku iliyofuata.

 

EGMA ILIVYOINGIA

“Suala hili jipya kwa mujibu ya barua ya pendekezo la mpango huo lilikuja na ada mpya ya asilimia 2.4 ya mkopo wa dola milioni 600 Tanzania ilizoomba. Nyaraka hizo pamoja na mambo mengine zilieleza Meneja Kiongozi ni Stanbic na Standard, kwa kushirikiana na mshirika wa ndani.

“Kwamba Stanbic imlipe mshirika wa ndani, ambaye Standard ilibaini baadaye kuwa alikuwa EGMA, ada ya asilimia moja ya mkopo, kutoka jumla ya ada ambayo iliongezwa kutoka asilimia 1.4 hadi asilimia 2.4,” unaeleza mwenendo wa kesi hiyo.

Mwenendo huo unasema katika barua ya Septemba 20, 2012, kutoka kwa Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji wa Standard kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic na Kaimu Mkuu wa Uwekezaji wa Stanbic, alieleza kwamba wanafanyia kazi barua ya upande wa pili baina yao na washirika wao, kuonyesha namna ada itakavyogawanywa na wajibu wa kila mmoja katika suala hili.

Mwenendo huo unasema kuwa wakati timu ya mkakati ya Standard ilipomjibu Sinare kwamba mshirika wa ndani (Kampuni ya EGMA) anahitaji kusaini barua ya dhamana, Sinare alijibu huku nakala ikienda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic na Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji, kwamba: “Hapana. Lengo ni kuwaleta kupitia makubaliano ya pembezoni baina yetu na mshirika.

“Katika michakato mingine iliyofanyika (Serikali na benki nyingine) na kadhalika. Hii ndiyo namna inavyofanywa. Serikali inapenda kuhusiana na upande mmoja tu, ambao baadaye kwa njia zake huingiza na kuendesha au kuratibu mshirika au washirika wengine.”

 

UZEMBE ULIOFANYIKA

Kwa mujibu wa mwenendo huo wa kesi, benki ya Standard ilionyesha uzembe kwa kutochukua hatua yoyote kufahamu uhusika wa EGMA katika mchakato wa uwezeshaji mkopo, ambao ulishuhudia ikilipwa ada ya dola milioni sita na hakuna kumbukumnbu za mawasiliano miongoni mwa maofisa wa Standard na Stanbic kuhusu umiliki wa EGMA, ushirikiano wake kwa Serikali ya Tanzania au kwanini ilifanywa kuwa sehemu ya mchakato huu.

“Septemba 20, 2012, Kaimu Mku wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic na Kaimu Mkuu wa Masuala ya wa Uwekezaji wa  Stanbic walifanya mkutano kwa njia ya simu kujadili  mgawanyo wa ada na EGMA.

“Katika mkutano huo pamoja na mambo mengine liliibuka suala kwamba Standard haingeweza kuilipa EGMA bila kupitia mchakato wa ‘Mjue Mteja Wako’ (KYC) kutathimini utambulisho wa mteja huyo.

“Mwishowe ikakubaliwa baina ya maofisa hao watatu kwamba ni Stanbic pekee itakayoendesha mchakato wa KYC kuhusu EGMA.

“Katika mkutano huo wa simu, Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Madeni ya Masoko ya Mitaji pia alieleza kwamba; ‘nadhani hakuna haja ya kuendesha mchakato wa KYC kwa jamaa hawa na ninadhani mmefanya kazi nao na hivyo mnawafahamu vilivyo jamaa hawa’.

“Katika mkutano huo wa njia ya simu pia ulikubaliana ada nzima kuwa asilimia 2.4 ya mkopo wa dola milioni 600.

 

SEKESEKE LA MGAWO

“Kwamba Stanbic itailipa EGMA mgawo wake wa asilimia moja na kugawa mgawo mwingine uliobakia wa ada ya 1.4 kwa Standard.

“Kutokana na makubaliano hayo, Standard haikuwa mtia saini wa makubaliano ya ada hiyo na EGMA. Katika mawasililiano mengine ya simu Septemba 26, 2012, washiriki hao hao watatu walikubaliana kwamba kwa vile EGMA haitahusika kwa vyovyote kama Meneja Kiongozi, inahitaji kutotajwa kabisa katika barua ya dhamana ya kuendesha mpango huo na Serikali,” unaeleza mwenendo huo.

Unaongeza: “Kwa ombi la Stanbic, Standard ilishiriki kikamilifu katika kuandaa makubaliano ya ushirikiano baina ya Stanbic na EGMA. Kati ya Septemba 2012 na Februari 2013, Stanbic na Standard zilirekebisha vipengele kadhaa katika makubaliano ya ushirikiano. Mkataba huo wa ushirikiano ulieleza majukumu ya EGMA kuhusu mchakato huo wa mkopo. Lakini hakuna ushahdi wowote kuonyesha EGMA ilifanya majukumu hayo.

 

SERIKALI ILIVYOBARIKI DILI

“Serikali kupitia Waziri wa Fedha, ilipitisha barua ya dhamana, inayotoa dhamana au mamlaka kwa Standard na Stanbic kuwezesha upatikanaji wa mkopo kwa ajili yake Novemba 15, 2012.

“Ikaziteua Standard na Stanbic kuwa Meneja Kiongozi kuhusiana na mkopo huo. Barua ya dhamana ilihusisha ‘ada ya uwezeshaji’ ya asilimia 2.4, lakini haikueleza popote mshirika yeyote wa ndani wala upande wa tatu. Barua ya ada ya Meneja Kiongozi ilionyesha kwamba ada ya asilimia 2.4 italipwa kwa Standard na Stanbic wakiwa kwa pamoja kama mameneja kiongozi kwa ushirikiano na mshirika wake. “Ijapokuwa, barua ya ada iligusia ‘mshirika wa ndani’,  EGMA haikubainishwa kama mshirika wa ndani.”.

 

MAWASILIANO TATA

Mwenendo huo unasema Februari 25, 2013, Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji alishiriki katika mawasiliano ya njia ya simu na wenye kuonyesha mwelekeo wa kuwekeza nchini Tanzania kupitia hati fungani.

“Wawakilishi wa Serikali ya Tanzania ambao walikuwa katika mawasiliano hayo walihusisha Waziri wa Fedha, pamoja na Kamishina wa TRA, ambaye alikuwa mwanahisa wa EGMA.

“Katika mawasiliano hayo ya simu, Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Madeni ya Masoko ya Mitaji alieleza kwa muhtasari suala hilo bila kugusia kabisa EGMA, wala uhusiano wa wanahisa wake kwa Serikali, wala kuonyesha majukumu yake katika suala hilo na iwapo itapokea ada ya dola milioni sita.

“Standard haikubainisha uhusika wowote wa EGMA na ada ambayo itapokea. Standard ilisaidia kuandaa mpango wa ada ambao Serikali ilikubali kuilipa Standard, Stanbic na mshirika (EGMA) ya asilimia 2.4, bila kugusia au kufafanua kuhusu EGMA,” unasema mwenendo huo.

 

DILI LILIVYOKAMILIKA

Unasema Februari 27, 2013, Serikali ya Tanzania ilitoa hati zake fungani zisizoorodheshwa kupitia sheria ya uwekezaji binafsi na kupata mkopo wa dola milioni 600, zilizoingizwa katika akaunti yake mjini New York Machi 8, kisha ilihamisha ada ya asilimia 2.4 sawa na dola za Marekani milioni 14.4 kwa Stanbic Tanzania.

“Stanbic ikaipatia EGMA asilimia moja katika akaunti ya EGMA iliyofunguliwa Stanbic. Baada ya EGMA kufanya malipo ya gharama za kisheria zinazohusiana na fedha hizo, karibu dola milioni 5.2 za zile milioni sita zikachotwa kati ya Machi 18 na 27, 2013. Standard haikufahamu uwapo wa fedha hizo hadi pale zilipochotwa na haina ufahamu wowote wa malengo ya waliozichota,” unasema mwenendo huo.

 

KAULI YA IKULU

Juzi, katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Septemba 29, 2015, Mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Ufisadi ya Uingereza (SFO), aliiandikia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), akiomba ushirikiano kwenye uchunguzi na uendeshaji wa kesi dhidi ya Standard Bank Plc, ambayo sasa inajulikana kama ICBC Standard Bank Plc.

Alisema Oktoba 29, 2015, Benki Kuu, iliiandikia SFO kutoa taarifa kuhusu ukaguzi lengwa ambao BoT iliufanya tarehe 15 – 19 Julai, 2013 kwenye Benki ya Stanbic Tanzania.

“Ushahidi huo kutoka Benki Kuu ulikuwa sehemu ya ushahidi uliosaidia SFO kushinda kesi. Katika kipindi chote ambacho SFO ilikuwa inafanya uchunguzi, ilishirikiana na taasisi zetu ikiwamo Takukuru, Benki Kuu, FIU na wengine. Mafanikio haya ndiyo yaliyosababisha uamuzi wa Tanzania kurejeshewa dola milioni 7 (Sh bilioni 15),” alisema Sefue.

Alisema baada ya ushindi huo, uchunguzi unaendelea ndani ya nchi ili kujua dola milioni sita zimekwenda wapi, na kama zilitumika kumhonga mtu ajulikane aliyeongwa.

“Katika hili tutaomba ushirikiano wa wenye kampuni hiyo ya EGMA ambao kwa taarifa za vyombo vya habari vya Uingereza ni Harry Kitilya aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Fraten Mboya  ambaye ni marehemu na Gasper Njuu,” alisema Sefue.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles