27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Jinamizi la Ukawa lamtesa Sitta

1...1..1.NA SARAH MOSSI, DODOMA
MAKADA wengine watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samuel Sitta, Profesa Sospeter Muhongo na Dk. Titus Kamani nao wamechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kuwania nafasi ya urais.
Kujitosa kwa wanasiasa hao katika kinyang’anyiro hicho kunaifanya idadi ya makada wa chama hicho waliochukua fomu kufikia 13 hadi kufikia jana.

SITTA
Sitta, ambaye ni Waziri wa Uchukuzi, ndiye aliyekuwa wa pili kuchukua fomu hiyo kwa siku ya jana, akitanguliwa na Profesa Sospeter Muhongo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu, Sitta alisema bado anayo nafasi ya kukaa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili kufikia muafaka baada ya wabunge wake kususia Katiba Iliyopendekezwa.
Sitta alichukua fomu hiyo saa 05:10 asubuhi, huku akisindikizwa na mkewe, Margareth Sitta na baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri.
Waziri Sitta ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba ambalo wabunge wa vyama vya upinzani walisusia kupitisha Katiba Iliyopendekezwa, wakidai kuondolewa mambo ya msingi yaliyopendekezwa katika Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba, huku wakimlaumu Sitta kutoendesha Bunge kwa kasi na viwango kama alivyoahidi.

Akijibu maswali ya wanahabari, Sitta alisema waliodai hakuliendesha Bunge la Katiba kwa kasi na viwango walikuwa na ajenda ambazo hazikufanikiwa chini ya uongozi wake.

“Hili la Serikali tatu ni uchochoro wa kuvunja Muungano, kwa haraka haraka hata kimantiki tu ilikuwa haikubaliki, watu kama hao hatuwezi kuwakumbatia.

“Mnyonge kutoka Zanzibar au Bara hafaidiki na Serikali tatu zaidi ya watu wanaotaka uongozi na kupigiwa mizinga, CUF wao walitaka mkataba, Chadema wao walitaka Tanganyika na hawa wote walikuwa hawampendi Mwenyekiti alikuwa kikwazo.

“Lakini mimi ni mtu mzima, siwezi kuacha hili jambo likiendelea, nitakaa nao, nitaongea nao kulimaliza hili, lazima nchi itulie,” alisema Sitta.
Awali Sitta alitaja sababu tano zilizomsukuma kujitokeza kuwania kuteuliwa kuwa mgombea, ikiwa ni pamoja na kukiimarisha chama.
Alisema ni lazima kukiimarisha chama kiuchumi na kusisitiza haiwezekani kuwa na chama ambacho watumishi wake hawaridhiki, ikiwa ni pamoja na malipo yao kidogo na huyapata kwa shida pamoja na mafao yao kupatikana kwa tabu.

“Hatuwezi kukubali chama cha ukombozi namna hii, lazima tuwe na chama chenye magari ya uhakika, kuwapandisha vyeo watumishi pamoja mishahara yao kuwa mizuri,” alisisitiza.

Hata hivyo, Sitta alisema hali duni iliyokuwapo sasa ndani ya chama imechangiwa pia na baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakikisaidia na kujifanya wao ndiyo wenye chama.

“Na hili nalisema wazi, lakini naomba nipewe ridhaa ya miaka mitano tu, ikifika mwaka 2020 nitawaachia vijana waliendeleze gurudumu.

Alitaja sababu ya pili ya yeye kujitokeza kuwa ni kuimarisha Muungano baada ya kuwapo chokochoko kutoka kwa baadhi ya watu wanaoeneza sera za utengamano.

“Hakuna faida yoyote kwa mtu wa Bara wala Mzanzibari, ukitokea mtengamano utaanza kuleta vurugu na hili linahitaji anayejua pande zote mbili na mimi nawajua wote, nitaweza kukaa pamoja na pande zote,” alisema.
Alitaja sababu ya tatu kuwa ni kuhakikisha Katiba iliyopendekezwa inafanyiwa uamuzi sahihi na kusisitiza bado ipo nafasi ya kukaa na pande zote mbili zilizosigana kumaliza matatizo yaliyojitokeza.
Sababu ya nne alisema ni kulimaliza tatizo la rushwa kwa kutenganisha uongozi na biashara na kusisitiza moja ya ni jambo atakalofanya ni kuhakikisha ipo sheria itakayomfanya mtu aamue biashara yake anaikabidhi kwa mtu kisheria mpaka atakaporudi aendelee na biashara yake.
“Sisi tunaapa, cheo ni dhamana, sitatoa wala kupokea rushwa, haiwezekani walizuka watu wakiwa wa kawaida lakini sasa hivi wamekuwa mabilionea, rushwa haiwezi kuchezewa tu hivi hivi inaua kabisa maendeleo,” alisema.

Sababu ya tano alisema ni kuleta uhusiano mzuri na motisha baina ya wajasiriamali na serikali yao.

MUHONGO
Kwa upande wake, Profesa Sospeter Muhongo ambaye aliwasili katika viwanja vya Makao Mkuu ya CCM saa 03:45 na kukabidhiwa fomu hiyo saa 04: 01 asubuhi, alikataa kuzungumza na wanahabari, badala yake alifanya mahojiano na Televisheni ya Taifa pekee.

Katika mahojiano hayo, alisema hana hofu na mgombea yeyote kati ya waliojitokeza, huku akisisitiza Watanzania ndio watajua nani mwenye hofu zaidi.
Profesa Muhongo alisema asingependa kuzungumzia watu na siyo vizuri kuzungumzia watu.
Alisema Watanzania wamechoshwa na umasikini, wamechoka kufanya kazi kwa mazoea na hivyo wanataka watu wenye mawazo mapya, ubunifu mpya na pia watu wenye uzoefu wa kitaifa na kimataifa.

KAMANI
Mwanachama wa mwisho kwa siku ya jana aliyejitokeza kuchukua fomu ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, ambaye alichukua saa 07:01 mchana.
Akizungumza na wanahabari, Dk. Kamani alisema moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha kila aliye kwenye nafasi anachukua uamuzi.
Dk. Kamani alisema watu wanalalamika viongozi hawatoi maamuzi magumu na kusisitiza atahakikisha kila mtu katika nafasi yake anachukua uamuzi, ingawa yapo maamuzi mengine ni ya kitaalamu.

Aidha, alisema atahakikisha anawafanya Watanzania wanaupenda Muungano na kuufanya kuwa ni wa kiuchumi ili usitafsiriwe kuwa ni kitu kibaya.

Dk. Kamani pia alisema iwapo atapewa nafasi, atajitahidi kuimarisha uhusiano na nchi jirani pamoja na kuimarisha uhusiano wa kimataifa.

“Tutaimarisha balozi zetu ili kuwa na uwakilishi mzuri na mabalozi zetu watusaidie kufanya biashara na kushindana kiuchumi, lakini tutaendelea kutochaguliwa marafiki,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles