JIJI LA ARUSHA LAJIPANGA KUKUSANYA BIL/- 30

0
775

Janeth Mushi, Arusha

Jiji la Arusha limejipanga kukusanya Sh bilioni 30 kutoka Sh bilioni 15 ya sasa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya jiji hilo.

Katika kufanikisha mpango huo  Maofisa Biashara kwa kushirikiana na Maofisa Maendeleo ya Jamii, Watendaji wa Kata na Mitaa watafanikisha kupata idadi ya wafanyabiashara, maduka na viwanda ili kufanikisha mpango wa Jiji hilo kuvuka lengo la kukusanya mapato kutoka Sh bilioni 15 kwa mwaka hadi kufikia bilioni 30.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi  Mtendaji wa Jiji la Arusha, Dk. Maulid Madeni, wakati akizungumza katika semina ya kuwajengea uwezo Maofisa Maendeleo ya Jamii wa kata zote za Jiji la Arusha namna ya kwenda kuwahamasisha wananchi na wafanyabiashara umuhimu wa kulipia leseni na kodi mbalimbali zinazotozwa.

Amesema kuna vyanzo vingi vya mapato ambavyo  havijafikiwa kikamilifu lakini kupitia mkakati huo vitafikiwa ili kuongeza mapato kwa maofisa hao kushirikiana na maafisa maendeleo ya Jamii walioko kwenye kata kuvifikia vyanzo hivyo.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa  katika kuhakikisha hakuna udanganyifu katika kupokea fedha Jiji litanunua mashine za EFD na kuwagawia wakusanya mapato.

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii Jiji la Arusha, Tajiel Mahega, amesema wameona matumizi ya Jiji ni makubwa kuliko mapato hivyo wameamua kuwapa elimu Maofisa Maendeleo ya Jamii ili kuongeza wigo wa ukusanyaji.

Naye mmoja wa Maofisa Maendeleo wanaopata mafunzo hayo , Evodius Kirefas, amesema mafunzo bila elimu kwa wananchi lengo la kuongeza mapato haliwezi kufikiwa hivyo watakwenda kutoa elimu hiyo.

Aidha Mkurugenzi hiyo amezindua operesheni maalum ya ukusanyaji wa mapato ya jiji hilo kwa lengo la kuhakikisha anaunga mkono juhudi za Rais Dr.John Magufuli kuhakikisha kila mfanyabiashara analipa kodi.

Katika operesheni hiyo Dk. Madeni aliambatana na wataalamu mbalimbali wa halmashauri hiyo ambapo amesema kuwa itakuwa endelevu na atazunguka katika masoko yote pamoja na vyanzo vya mapato vilivyopo katika halmashauri hiyo.

“Hii ni operesheni endelevu kwa lengo la kuhakikisha wafanyabiashara wanalipa kodi,wana leseni,wanatoa risiti halali pamoja na kuaa na mikataba jalali ya halmashauri,” amesema

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here