23 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

JIJI DAR LANUSA UFISADI DDC

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imebaini kuwapo  ufisadi katika Shirika la Maendeleo Dar es Salaam (DDC) na kuamua kupandisha gawio kwa mwaka kutoka Sh milioni 50 mpaka Sh milioni 750.

Uamuzi wa kuongeza gawio hilo ulifikiwa jana wakati Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo lilipopitisha bajeti yake ya mwaka wa fedha 2017/2018 ambayo ni Sh bilioni 20.2 kutoka Sh bilioni 7 za mwaka 2016/2017.

Baraza hilo  liliunda kamati maalumu kufuatilia vyanzo vya mapato ya shirika hilo baada ya kutoridhishwa na gawio lililokuwa likitolewa la Sh milioni 50 kwa mwaka.

Akizungumza katika kikao hicho, Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Humphrey Sambo (Chadema), alisema katika tathmini iliyofanyika ilibainika  mapato ya shirika hilo yalikuwa Sh bilioni 1.2 lakini walielezwa kwamba kiasi kikubwa cha fedha kilikuwa kikitumika kuendesha shirika hilo.

“Tuliambiwa kwamba kodi ya vyumba ni Sh milioni sita kwa mwaka lakini tulipowafuata wapangaji walituambia wanalipa Sh milioni 36 na walituonyesha mikataba. Kwa hiyo anayepokea alikuwa anapeleka Sh milioni sita na Sh milioni 30 anabaki nazo.

“Katika vyumba vingine walisema kodi ni Sh milioni 2.4 kumbe kodi halisi ni Sh milioni 7.8, watu wameligeuza shirika lile kama sehemu ya kuchukua fedha,” alisema Sambo.

Alisema baada ya kubaini hali hiyo waliamua kutangaza zabuni lakini walijitokeza wapangaji na kuomba utaratibu huo usimamishwe kwa kuhofia kukosa vyumba.

“Tulilazimisha kutangaza zabuni lakini wakajitokeza wapangaji wakasema waambiwe ni kitu gani kinatakiwa, tukawaambia hiyo Sh milioni 36 tunataka iingie kama ilivyo na ‘mtu kati’ aondolewe. Kamati ya fedha ikaamua angalau watuletee Sh milioni 750 kwa hiyo hata mapato yao pia yataongezeka,” alisema.

DAR KUKOSA MAKABURI

Halmashauri hiyo pia imetenga Sh milioni 300 katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kununua eneo la kuzikia katika eneo la Kigamboni ama Chanika.

Suala la sehemu za kuzikia, jana lilitawala katika kikao hicho huku wajumbe wakitaka eneo hilo linunuliwe haraka kwa vile  sehemu nyingi za kuzikia zimejaa.

“Wako watu wanaokufa hawana ndugu sisi tunahusika nao, cha ajabu hatumiliki hata eneo, maeneo mengi yaliyopo ni ya halmashauri nyingine ambayo pia yamejaa.

“Ukienda Kinondoni kuna mtihani mkubwa ni utaratibu tu unafanyika aliyekufa asionekane…ikienda ile mifugo isiyokuwa na adabu hali itakuwa tete zaidi,” alisema Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mussa Kafana (CUF).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles