25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

JESHI LA UGANDA LAOMBA RADHI WANAHABARI KUPIGWA

 

 

KAMPALA, UGANDA


JESHI la Uganda limeomba radhi katika tukio la nadra baada ya askari wake kuonekana kwenye mkanda wa video wakimpiga mwandishi wa habari aliyekuwa akitimiza wajibu wake kwenye maandamano ya kupinga kushikiliwa kwa Mbunge Bobi Wine Jumatatu hii.

Katika tukio hilo waandishi wengine nao walipigwa walipokuwa wakiarifu jamii juu ya maandamano hayo kupitia vyombo vyao vya habari.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi, ilieleza kuwa kitendo hicho kilichofanywa na askari wake si cha weledi na kuwa watakamatwa kwa mujibu wa sheria za jeshi hilo.

Kumekuwa na mvutano wa kisiasa nchini Uganda baada ya Mbunge Bobi, na wengine wanne wa upinzani, kukamatwa wiki iliyopita.

Bobi ni maarufu nchini Uganda kutokana na kujihusisha na tasnia ya muziki kabla ya kuchaguliwa kama mbunge mwaka jana, ambapo amefanikiwa kuteka umma wa Waganda miongoni mwao vijana, na kuendesha harakati za kisiasa dhidi ya Rais Yoweri Kaguta Museveni.

Vijana wengi walioko sasa nchini Uganda walikuwa hawajazaliwa wakati Rais Museveni alipotwaa madaraka mwaka 1986.

Mapema wiki hii chama cha kutetea haki za binadamu kilichoko mjini New York, kiliwataka polisi na jeshi nchini Uganda kusitisha mara moja mashambulizi yao dhidi ya vyombo vya habari na waandishi habari nchini humo na kuheshimu haki za waandamanaji.

Katika video iliyorushwa mtandaoni, mwandishi wa habari wa Shirika Habari la Reuters, James Akena, anaonekana akipigwa kwa fimbo na askari wawili moja ya mitaa ya mji mkuu, wa Kampala.

Kipigo kiliendelea kumuangukia hata alipoamua kusalimu amri na kuweka mikono yake juu huku akiwa amepiga magoti.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu linasema kupigwa na kukamatwa kwa waandishi wa habari ni ushahidi tosha kuwa wa mamlaka nchini Uganda wanataka kuficha mwenendo wa vikosi vya usalama nchini humo.

Katika taarifa yake, Jeshi limejitetea kuwa awali lina uhusiano mzuri baina yake na vyombo vya habari nchini humo.

Mbunge Bobi, ambaye jina lake kamili ni Robert Kyagulanyi, bado anaendelea kusalia kizuizini na kwamba anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya kijeshi siku ya Alhamisi kujibu mashtaka ya umiliki wa silaha kinyume cha sheria.

Familia ya mbunge huyo inadai kuwa alishambuliwa vikali, lakini jeshi, ambalo linamshikilia Mbunge huyo , limekana vikali madai hayo kama ilivyokuwa kwa Rais Museveni.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles