31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JE UNAZIJUA TABIA ZA ‘NYUMA YA PAZIA’ ZA MARAIS WA MAREKANI?

Rais Kennedy akiwa na watoto wake
Rais Kennedy akiwa na watoto wake

Na JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM

KINAWEZA kuwa kitu cha kuchekesha na pia kustajaabisha kwa namna baadhi ya Wamarekani wanavyowaangalia marais wao kwa nyakati zilizopita.

Wanawaangalia kana kwamba walikuwa viumbe wenye uzito wa kipekee, wenye kufaa kuabudiwa na kwamba wana chembe fulani ya utakatifu au utukufu tofauti na Wamarekani wengine.

Hiyo ni pamoja na kwamba, kwa wengi baadhi ya uchafu wa marais wao, kwao si kitu kama walikuwa na utendaji kazi uliotukuka, iwe ni ushujaa wa kivita au mafanikio ya kiuchumi au kijamii.

Ukiachana na hilo, marais wengi bila kujali umaarufu au kupendwa na kuaminiwa kwao, walitenda mambo machafu nyuma ya pazia tena wengine wakiwa Ikulu (White House) au wakiwa tayari wakazi wa jumba hilo jeupe la Marekani.

Hiyo ni kinyume ya baadhi walivyodhani, kuwa unapokuwa rais wa taifa hilo lenye nguvu kubwa duniani, ina maana wewe ni mtu wa maaadili ya juu na mwenye heshima ya kipekee jambo ambalo halina ukweli wowote.

Katika makala haya, yatagusia kwa ufupi baadhi ya marais hao kuhusu upande wao wa pili wa shilingi licha ya umaarufu na uwezo wao wa kutawala uliowafanya wajulikane duniani kote. Kwa kuanza tunaanza na Rais wa kwanza wan chi hiyo, George Washington.

Washington ndiye baba mwasisi wa taifa la Marekani, aliyeweka misingi mingi inayoonekana hadi leo hii.

Yeye alisimamia mkutano ambao ulishuhudia kupitishwa kwa Katiba ya Marekani, ambayo ilichukua mkataba wa shirikisho ambayo sasa imebakia kama sheria kuu ya taifa hilo.

Washington alichaguliwa kuwa rais kwa kura nyingi mwaka 1788, na kutumikia vipindi viwili madarakani na alishuhudiwa akijenga Serikali imara na yenye kujitosheleza kifedha.

Alihakikisha Marekani haisimami upande wowote katika bara lililokuwa limetawaliwa na vita la Ulaya, akikabiliana na uasi, akaushinda ukoloni wa kiingereza na kuwa kiongozi wa kwanza katika historia ya dunia kuushinda mfumo huo.

Kwa mengi aliyofanya, alifanikiwa kuteka nyoyo za Wamarekani wa aina na tabaka zote na si ajabu hadi leo hii anasimama katika tatu bora ya marais kipenzi cha wengi na wenye utendaji uliotukuka nchini humo.

Hata hivyo tukizungumza upande hasi, Washington aliendekeza utumwa na yeye mwenyewe alikuwa na watumwa wengi jumbani kwake na mashambani mwake.

Hilo la utumwa pengine ndiyo maana limemfanya awe na kura nyingi za maoni tangu utaratibu huo uanze nchini humo kwa kushikilia nafasi ya pili nyuma ya Abrahamu Lincolin.

Lincoln, Rais wa 16 wa Marekani ambaye aliuawa kutokana na misimamo yake ya kupiga vita utumwa na kutaka haki za weusi, alifanikiwa kuyaunganisha majimbo ya Kusini na Kaskazini yaliyokuwa yakielekea vitani na kutaka kujitenga kutokana na kukinzana kuhusu utumwa na haki za weusi.

Kitu kingine ambacho wengi hawakuwa wakikifahamu na ambacho bado wanakibishania ni kwamba kwa  viwango vya sasa Washington alikuwa mfanyabiashara wa dawa za kulevya bila kujali tafiti zinazomlinda.

Washington, alikuwa mkulima wa bangi zilizolimwa na watumwa wake na alikampenia matumizi yake, ijapokuwa watetezi wake walisema alilenga zitumike kwa ajili ya tiba.

Aliwahi kukaririwa akisema asifikiriwe vibaya kwa ukulima wake huo wa bangi kwa kuwa alikuwa akiamini kuwa, bangi ni dawa na anakumbushia kilichoandikwa katika Biblia Takatifu kwa kuhalalisha madai yake.

Alitumia Kitabu cha Mwanzo 1. 29 kinachosema;  “Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu, vitakuwa ndivyo vyakula vyenu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ya vitu vinavyokatazwa nchini humo ni kosa kumiliki au kutumia bangi.

Rais wa pili wa Marekani ijapokuwa upande wake wa pili wa shilingi si siri, naye alipotoka.

Rais huyo, John Adams aliendekeza uhusiano wa mapenzi na ndugu zake na alimuoa na kumzalisha watoto binamu yake mwenyewe wa damu, Abigail Smith.

Rais Thomas Jefferson naye anadaiwa alikuwa mbakaji na alifanya mapenzi na watumwa wake huku Rais Richard Nixon akidaiwa kujishughulisha na genge la wahalifu ambao pia walishuhudiwa wakati wa kashfa iliyomtoa Ikulu ya Watergate.

Rais wa 35 wa Marekani John F. Kennedy ambaye Novemba 22 mwaka huu anatimiza miaka 52 tangu kuuawa kwake, alikuwa funga kazi.

Akihesabiwa kama kipenzi cha wengi miongoni mwa marais wa vizazi vya karibuni, Kennedy aliyejulikana kwa ufupisho wa majina yake JFK, alikuwa mtumiaji mzuri wa dawa za kulevya.

Dawa hizo pia zilimuathiri ikiwamo kumsababishia maumivu ya mara kwa mara ya mgongo au miguu, hali ambayo inadaiwa mara nyingi alitembelea magongo.

Hata alipotakiwa kuonekana hadharani, alijitutumua kana kwamba hakuna lililotokea na alikuwa akifanya hivyo kwa msaada wa dawa za kutuliza maumivu alizopatiwa na daktari wake.

JFK, aliyekuja kutengeneza familia maarufu ya kisiasa nchini humo, mbali ya pia kudaiwa kuwahi kuwa na uhusiano na genge la Mafia, anajulikana zaidi kwa mlolongo wa wanawake aliowabadili kama nguo wakiwamo wasanii nyota, makahaba na watumishi wake wa Ikulu.

Mwenendo huo wa ukiwembe kwa wanawake mara kadhaa uliiyumbisha ndoa yake.

Wakati hayo yakiwa si siri, hivi karibuni kimetolewa kitabu kipya kinachomhusisha JFK ambapo mfanyakazi wa zamani wa Ikulu aliyekuwa akifanya mazoezi akitokea chuoni, Mimi Alford katika kitabu chake amesimulia kuhusu uhusiano wake wa miezi 18 na JFK ambao alikuwa ameufanya kuwa siri kipindi chote hicho.

Alford aliyekuwa na miaka 19 kipindi hicho, alisema kwamba ni Kennedy aliyekuwa na umri wa miaka 45 wakati huo ndiye aliyeondoa bikira yake katika kitanda cha mkewe wakati wa kiangazi mwaka 1962.

Akiwa amejipumzika katika bwawa la kuogelea la Ikulu, Mimi anasema aliibukiwa na Rais kutokea majini na akamwuliza iwapo hatajali kuungana naye mahali hapo.

Anasema siku tano tu tangu awepo Ikulu, alishtushwa wakati msaidizi wa habari wa rais, David Powers alipomchukua kutoka katika kundi la wafanyakazi wenzake ambao walikuwa katika karamu na akaongozwa hadi katika chumba cha mke wa rais na wakiwa humo walifanya mapenzi kwa mara ya kwanza.

Katika umri wa miaka 19 kipindi hicho anasema kwamba hakuwa na uwezo wa kufanya lolote kumzuia rais asitimize lengo lake.

Aidha, anasema kabla ya kufanya ngono siku chache baada ya kuonana mara ya kwanza katika bwawa la kuongelea, alilazimishwa kufanya ngono ya mdomo na Powers.

Na wakati alipohisi ana mimba JFK alimuagiza Powers afanye mpango na daktari kuitoa, wakati kitendo hicho kilikuwa hakiruhusiwi kipindi hicho.

Alford, sasa 69 na anaishi New York, pia anaandika kuwa wakati wa uhusiano wao hakuwahi kumwita Kennedy kwa jina lake la kwanza  ‘Jack’ na daima alimwita ‘Bwana Rais hata wakati wakiwa pamoja kitandani.

Lakini, pia alifichua upande mwingine ambao ulimkera, mbali ya dawa za kulevya ambazo yeye aliwahi kulazimishwa azijaribu na kuzigomea, na pia kutakiwa afanye ngono na mdogo wa JFK, lakini pia aligomea hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles