27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

January Makamba atangaza kugombea urais

Januari Makamba
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba

ARODIA PETER NA EVANS MAGEGE, DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ameweka wazi dhamira yake ya kutaka kugombea urais mwakani na kueleza kuwa amefikia uamuzi huo kwa asilimia 90.

Makamba alitangaza dhamira hiyo juzi usiku, alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Mahojiano hayo yalikuwa yakirushwa kutokea London, Uingereza ambako yalifanywa na mtangazaji Salim Kikeke.

Makamba alisema amekwisha kujitafakari, kujitathmini na ameridhika kwamba wakati ukifika atachukua fomu za kugombea nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema kutokana na kujitathmini kwake, dhamira imemtuma kwa asilimia 90 kuwania kiti hicho akiwa na lengo la kuwatumikia Watanzania na kuwatoa walipo.

“Kwanza niweke wazi kwamba mgombea mzuri wa urais atatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), hilo halina ubishi na mimi nimejipima na kujitathmini kwa asilimia 90 kwamba wakati ukifika nitachukua fomu ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.

“Na asilimia 10 zilizobaki nimewaachia wazee, viongozi wastaafu na viongozi wa dini wanishauri. Nafahamu matatizo waliyonayo Watanzania na ninachokitafuta ni utumishi si kazi,” alisema Makamba.

Makamba ni miongoni mwa makada wa CCM ambao kwa muda mrefu walikuwa wakitajwa kutaka kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.

Katiba Mpya

Akizungumzia kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Makamba, ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, alishauri ni vema mchakato huo ukarudishwa kwa wananchi kuweza kupata maoni kuhusu muundo wa Muungano.

“Mimi binafsi naona suala la Katiba limetushinda sisi wanasiasa, ni vema tulirudishe kwa wananchi waamue mambo mawili; moja kama wanautaka Muungano uliopo na wanataka uwe na muundo wa aina gani.

“Ni ukweli mchakato umetushinda sisi wanasiasa, option (njia sahihi) iliyopo ni kuurudisha kwa wananchi waweze kuamua,” alisema Makamba.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Makamba kuhusu mchakato wa Katiba Mpya kurudishwa kwa wananchi inakwenda kinyume cha matamshi ya CCM ambayo imeweka msimamo wa kuendelea na mchakato huo, licha ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuugomea.

Ukawa waligoma kuendelea na mchakato huo katika Bunge Maalumu la Katiba Aprili mwaka huu, wakidai hawaridhishwi na mwenendo wa wenzao wa CCM kutaka kubadili maudhui ya maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji (Mstaafu) Joseph Warioba.

Wajumbe wa CCM walitaka maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Warioba ifumuliwe na kusukwa upya ikiwa na maudhui yanayolenga kuwa na Muungano wa Serikali mbili.

Makamba aliusifu uongozi wa Rais Jakaya Kikwete akisema umefanya mambo mengi, licha ya changamoto zilizopo.

Adhabu kwa makada

Februari 18 mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu, katika kikao chake ilipendekeza zichukuliwe hatua za nidhamu kwa makada wake ambao wamekwisha kuanza kampeni ya kuwania urais wa mwaka 2015.

Katika adhabu hiyo, makada hao walizuiwa kujihusisha na masuala ya siasa ndani ya chama hicho kwa miezi 12, huku mwenendo wao wa siasa ukifuatiliwa kwa uangalizi mkali katika kipindi chote cha kutumikia adhabu hiyo.

Uamuzi huo ulibarikiwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyokutana Februari 17 mwaka huu mjini Dodoma, chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.

Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa tuhuma za kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati ni pamoja na January Makamba.

Wengine ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Makada wengine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Kabla ya adhabu hiyo, makada hao waliitwa na kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ambayo iliwatia hatiani kwa kutumia Kitabu cha Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).

Wakati akisoma uamuzi huo wa Kamati Kuu, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema Ibara 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa chama hicho inawazuia kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.

Alisema: “Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo, imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo, chama kitawachukulia hatua kali.”

Nape alisema Kamati Kuu imeiagiza Kamati ya Maadili kuwachunguza mawakala na watendaji wa wanachama hao waliokuwa wakiratibu shughuli mbalimbali waweze kuchukuliwa hatua kali za nidhamu, hatua inayolenga kuhakikisha chama hakigawanyiki.

Hata hivyo, siku chache zilizopita, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alishiriki katika harambee moja jijini Mwanza ambayo pia ilikuwa na mwelekeo wa kujionyesha kuwa anaweza kuwania urais mwakani.

Membe alisema kabla ya kwenda Mwanza alikutana na Rais Jakaya Kikwete, ambaye alimpa Baraka zote.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles