24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Jamii ichukue tahadhari dhidi ya corona

Mwandishi Wetu

KWA sasa dunia imekuwa ikishuhudia idadi kubwa ya watu wakipoteza maisha kutokana virusi vya ugonjwa wa corona (Covid-19).

Kwa hapa nchini na kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu hadi sasa Watanzania 25 wamethibitika kupata maambukizi ya ugonjwa huo huku mmoja akipoteza maisha.

Hata hivyo awali ilionekana maambukizi ya ugonjwa huu yalitokana na taarifa za mwingiliano wa wageni kutoka mataifa ya nje jambo lililoifanya Serikali kuchukua hatua ikiwamo kutenga maeneo dhidi ya wasafiri wote waliotoka nje ya nchi.

Pamoja na mikakati hiyo, maambukizi kwa upande wa wageni kutoka nje hali hiyo inatajwa kudhibitiwa na sasa maambukizi yanahamia kwa Watanzania wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo ni hatari.

Tunajua utamaduni wetu Watanzania pindi tunapokutana ni kusalimiana kwa kupeana mikono huku tukishindwa kutambua kwamba jambo hilo ni la hatari kwa mustakabali wa afya zetu.

Si hilo tu, pia hatua ya kutokuwapo kwa mikusanyiko isiyo ya lazima itasaidia kuepuka kuenea kwa ugonjwa huu nchini, hivyo ni vema hata kwa viongozi wa dini hasa kupitia misikiti na makanisa kulitambua hilo.

Mkusanyiko wowote katika nyumba za ibada au katika vituo vikuu vya mabasi na hata masokoni ni vema iangaliwe, ikiwamo watu kutakiwa kutofanya hivyo vinginevyo tutakuwa tunaweka rehani afya za wananchi.

MTANZANIA tunashauri kwamba ni vema viongozi wa dini kupitia nyumba za ibada wakachukua tahadhari kwakuwa Tanzania imetoka kwenye maambukizi ya nje na kuingia kwenye maambukizi ya ndani na waumini wajisafishe nyumbani kwao kabla ya kufika kwenye nyumba za ibada.

Tunajua kwamba viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika jamii dhidi ya kupambana na majanga mbalimbali duniani.

Hivyo viongozi wanajua kuwa ugonjwa wa corona upo na muhimu wakaweka utaratibu ili kuhakikisha wanaelimisha na kufundisha waumini wao kuhusu ugonjwa huo na kuwapatia njia za kupambana, ikiwamo kuwapa moyo na matumaini kuweza kuushinda.

Kwa mujibu wa takwimu za dunia, kwa muda wa saa 24 kuna wagonjwa takribani 1,300,000 na vifo 39,275 na kwa Afrika wagonjwa 7,647 na vifo 326.

Kwa wale wanaosema Afrika hatutaguswa wanajidanganya kwani takwimu hizo zinaonyesha si nzuri kwani zinatutaka tuendelee kuchukua tahadhari kuhusu ugonjwa huo.

Ikiwa kila mwanajamii atatambua wajibu wake ikiwamo kwa kutoa elimu hii kuanzia ngazi ya familia, ni wazi Tanzania inaweza kudhibiti ugonjwa huu.

Tunajua corona sasa imeleta athari mbalimbali ikiwamo za kiafya na kiuchumi kutokana na kuwapo kwa kasi ya maambukizi na hatua zisipochukuliwa kwa haraka na kila Mtanzania tunaweza kujikuta kwenye majuto.

Sisi MTANZANIA tunasema kinga ni bora kuliko tiba na hakika kila mwanajamii akilitambua hili tutafanikiwa mapambano dhidi ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa corona nchini kwetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles