23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jali heshima ya mtu kabla ya kumwambia ukweli

CHRISTIAN BWAYA

UKWELIi hauna mbadala. Hata usiposemwa wazi wazi, hubaki kuwa ukweli tu. Ukweli huwa una tabia ya kujitenga. Unaweza kufanya juhudi za kuukana lakini hauwezi kuuficha kwa muda mrefu. Utauzuia leo kwa sababu zako, lakini kesho utachipua.

Ukweli una nafasi kubwa maishani. Katika uhusiano na watu, iwe kwenye familia, kazini, biashara na maeneo mengine unakochangamana na watu, hutokea nyakati mkalazimika kuambiana ukweli. Lakini wakati mwingine inashangaza kwanini umwambie mtu ukweli na asiwe tayari kuupokea? Umewahi kujiuliza kwanini ukweli wakati mwingine hupuuzwa na kukataliwa? Kwanini baadhi ya watu huwachukia watu kwa kosa moja kubwa la kuzungumza ukweli? Kosa ni nini?

Fikiria uko kwenye kikao kazini na kuna mwenzenu asiyeweza kukaa na kitu kwenye nafsi yake bila kukitoa. Huyu ni mtu ambaye ikitokea hajaridhishwa na uamuzi wa bosi, atazungumza waziwazi kikaoni. Shida inakuja baada ya kuusema ukweli huo, si tu wafanyakazi wanaweza kujawa hofu, lakini pia uongozi unaweza kujenga uhasama na mtu huyu. Kosa lake ni lipi? Kusema ukweli?

Hata kwenye uhusiano wa kifamilia, unaweza kuwa na jambo unalodhani mwenzako ni muhimu alifahamu na kulifanyia kazi. Labda ni uamuzi mbaya anayoyafanya na yanaweza kumgharimu, au tabia fulani zisizofaa ambazo ikiwa zitaendelea, hutafurahia. Basi kwa kutambua umuhimu wa kusema kile unachokiamini bila kuficha, unakaa naye kumweleza kwa uwazi. Kwa mshangao wako, mwenzako anakujia juu na kupambana na ulichokisema. Usipokuwa makini huo unaweza kuwa mwanzo wa matatizo katika uhusiano wenu. Kosa ni lipi hapo? Kusema ukweli?

Pamoja na umuhimu wake, unaona kwamba ukweli unaweza kuchangia watu kufarakana, marafiki kuelewana vibaya, uhusiano kazini kuzorota, waajiriwa kufutwa kazi na hata kuzalisha misuguano baina ya ndugu na jamaa. Hili linashangaza kwa sababu kwa hali ya kawaida ungefikiri shida ingeweza kuwa watu kuzushiwa, kusemwa kwa mabaya wasiyo yafanya, kusingiziwa kwa mambo yasiyokuwapo. Inapotokea shida inakuwa ni ukweli kujisimamia kinyume na matarajio ya wale wanaoathirika na matokeo ya ukweli huo unajiuliza je, ni kwamba ukweli haupendwi vile ulivyo au kuna kingine kinachoumiza kuliko ukweli wenyewe?

Katika kujibu swali hili, nikukumbushe kuwa hitaji muhimu la mwanadamu. Kila mwanadamu anahitaji kupewa heshima. Hadhi ni kipaumbele kikubwa cha mwanadamu. Uhusiano wako na binadamu huyu unategemea namna gani unalinda heshima na hadhi yake. Inapotokea umeshindwa kulinda heshima hiyo aliyonayo, mwanadamu hawezi kukusikiliza. Kwa lugha nyingine, chochote unachokifanya kwa mwanadamu huyu anayelinda heshima na hadhi yake lazima kwanza kilenge kulinda heshima yake. 

Hapa ndiko wasema ukweli wengi wanapokosea. Kwa kuamini kuwa wanachokijua ni ukweli usio na shaka, watu hawa hutumia ukweli huo kama kichaka cha kuumiza hisia za wale wanaotakiwa kuupokea. Fikiria mume anayejua mke wake amekosea na anazungumza kwa lugha yenye kumdhalilisha na kumvunjia heshima yake. Fikiria mke asiyependa tabia fulani aliyonayo mume wake na kutumia ukweli huo kama sababu ya kumvunjia heshima na kumdhalilisha. Fikiria mfanyakazi anayefahamu udhaifu wa bosi wake na kuamua kuuzungumza hadharani bila kujali bosi atajisikiaje.

Tabia ya kutokujali wanaoguswa na ukweli huo watajisikiaje, unajikuta ukitengeneza mazingira ya wao kujihami kulinda hadhi na heshima zao ingawa ukweli halisi wanaujua. Katika mazingira kama haya namna ukweli unavyosemwa unakuwa chanzo cha migogoro inayoepukika. Tunachojifunza ni kwamba unapomwambia mtu ukweli unaojua unaweza kutishia hadhi na heshima yake, ni muhimu kuchukua tahadhari. Hakuna binadamu anayethubutu kuukubali ukweli anaojua unaweza kubomoa hadhi yake.

Lakini pia, binadamu anahitaji kujihakikishia kuwa wewe unayemwambia ukweli unajali kwanza. Hii nayo ni hulka inayomtawala mwanadamu. Humsikiliza anayejua anajali hisia zake, anaheshimu mawazo yake, aliye tayari kusikiliza na anayejua thamani ya hadhi yake. Hulka hii ndiyo inayomfanya mwanadamu huyu asiweze kuchukulia kwa uzito kile kinachosemwa na mtu anayejua fika kuwa hajali hisia zake, haheshimu mawazo yake na haoni thamani yake.

Ndio kusema ili binadamu aweze kukusikiliza lazima kwanza ajiridhishe kuwa unamjali. Tunachojifunza hapa ni kwamba ukweli usioambatana na upendo unachukuliwa kama ukatili. Unapomwambia mtu ukweli bila kumwekea mazingira ya kujisikia unamjali na kumpenda, hutafsiri ukweli huo kama njia ya kumdhalilisha na hatakubali.

Siku nyingine kabla hujasema ukweli kama ulivyo, jiulize; unajali vya kutosha? Unampenda unayetaka kumwambia ukweli? Unatumia lugha inayoonesha kuheshimu utu wake? Ukweli usiotanguliwa na utu una tabia ya kupuuzwa.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles