Jalada kigogo mwendokasi kutua kwa DPP

0
525

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

Jadala la uchunguzi dhidi ya mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART), linatarajiwa kutua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wakati wowote kuanzia sasa.

Kigogo huyo wa idara ya fedha ambaye kwa sasa anaendelea kusota rumande kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa anashikiliwa yeye na wenzake saba kwa tuhuma za kuhujumu mfumo wa teketi za mabasi ya mwendokasi kwa kutoa tiketi feki na kujiingizia mamilioni ya fedha kwa njia ya udanganyifu.

Akizungumza na MTANZANIA jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kwa sasa wamekamilisha sehemu kubwa ya uchunguzi dhidi ya wafanyakazi hao wa Kampuni ya UDART.

Alisema hatua ya kufikishwa kwa DPP kwa hatua za awali za kuona kama anaweza kufikishwa mahakamani ama laa.

“Kuna baadhi ya maeneo machache ya kiupelelezi bado tunayafanyia kazi, tukikamilisha tutawasilisha jalada kwa DPP ili aweze kuandaa mashtaka mahakamani,”alisema Mambosasa.

Hivi karibuni, Kamanda Mambosasa alipozungumza na gazeti hili, alisema Jeshi la Polisi linawashikilia wafanyakazi hao huku wengine 18 wakiachiwa kwa dhamana.

Siku chache baadaye alisema kuwa,  upelelezi utakapokamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa kosa la uhujumu uchumi.

Alisema watuhumiwa hao wamefanya kosa hilo la kuhujumu mradi wa Serikali ambao ni wa kitaifa na kimataifa kwa kutaka kufifisha jitihada za Serikali.

Hatua ya kukamatwa kwa kigogo huyo inatokana na taarifa iliyoripotiwa na MTANZANIA katika ripoti yake maalumu kuhusu namna mradi huo unavyohujumiwa kutokana na kutotumika kwa tiketi za kieletroniki.

Hali hiyo iliifanya Serikali kupitia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart),  kuunda timu ya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola ambapo walifanikiwa kuubaini mtandao huo hatari kwa mapato ya Serikali.

Awali, mradi huo wakati unaanza mwaka 2016, ulikuwa unabeba abiria 75,000 na kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 200,000 na  kwa kila safari hulazimika kulipa Sh 650 ukijumlisha kwa idadi hiyo mapato kwa siku yaliyokuwa yanakusanywa hufikia Sh milioni 130,000 ingawa kwa sasa yameshuka.

Katika mtandao huo imebainika mbali ya kufyatua tiketi feki pia wamekuwa wakifanya ujanja kwa kuwauzia watu wazima tiketi za wanafunzi ya Sh 200 badala ya Sh 650 huku kiwango kinachobaki kikingia katika mifuko ya wajanja.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here