24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MUTUNGI: SIHUSIKI NA VIBALI MIKUTANO YA SIASA

PATRICIA KIMELEMETA


MSAJILI wa Vyama Vya Siasa, Jaji Fransic Mutungi amesema hana mamlaka ya kutoa vibali vya kufanyika kwa mikutano ya ndani au nje pamoja na maandamano kwa vyama vya siasa.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya watu mbalimbali kumlalamikia Jaji Mutungi kuwa amekuwa akinyamazia ukiukwaji wa sheria ya uanzishwaji wa vyama vya siasa ambayo inavipa uhuru wa kufanya mikutano kama moja ya kazi zake.

Msajili huyo pia anatupiwa lawama kwamba anakibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuruhusu viongozi wake kuendelea kufanya mikutano ya ndani na nje, huku vyama vingine vikizuiwa kufanya mikutano.

Miongoni mwa vyama vinavyozuiliwa ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambapo baadhi ya viongozi wake wamekamatwa katika maeneo mbalimbali na kuwekwa mahabusu kwa amri za wakuu wa wilaya.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalum ofisini kwake Dar es Salaam jana, Jaji Mutungi alisema wenye mamlaka ya kutoa vibali vya mikutano ya vyama vya siasa ni Jeshi la Polisi kulingana na eneo husika na si ofisi yake.

“Nimeshangazwa kusikia wanasiasa wananipa lawama ya kuwaruhusu CCM kufanya mikutano ya kisiasa huku vyama vingine nikivizuia ili visiweze kufanya mikutano, wakati wanajua kuwa sina mamlaka ya kutoa kibali cha mikutano, ” alisema.

Jaji Mutungi alisema sheria ya vyama vya siasa inatoa mwongozo kuhusiana na suala hilo na kwamba kama kuna tatizo lolote wanapaswa kuandika barua  ya malalamiko kwenda Baraza la Vyama Vya Siasa ili yaweze kushughulikiwa kisheria.

“Wanasiasa wanajua sheria ya vyama vya siasa inasemaje, lakini wanashindwa kuifuata badala yake wanaanzisha lawama zisizo na msingi ili ofisi yangu ionekane inatuhumiwa.

“Nipo hapa kwa ajili ya kuvisimamia vyama vyote vya siasa iwe  CCM, Chadema, CUF,  NCCR -Mageuzi, TLP na vyama vingine, hivyo malalamiko ya kukibeba chama kimoja hayapo na hayo ni maneno yao tu.

“Hakuna sera, kanuni au katiba ambayo inatoa mwongozo kwa vyama vya siasa vinavyopata matatizo kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii au vyombo vya habari ili kuwasilisha malalamiko yao, lakini wanasiasa wamekuwa wakiwatumia wanahabari badala ya kuandika barua kwa baraza la vyama vya siasa, jambo hilo siyo zuri,” alisema Jaji Mutungi.

Katika hatua nyingine Msajili huyo alikataa kuzungumzia hatua ya Chama Cha CUF kuingia katika mgogoro na Chadema, akisema mgogoro huo upo mahakamani si vema yeye kuuzungumzia.

Alisema vyama vingine kuingilia mgogoro huo ni sawa na kukiuka katiba ya nchi ambayo inamtaka kila mwananchi kuheshimu katiba na kama suala lipo mahakamani halipaswi kujadiliwa mpaka mahakama itakapotoa hukumu.

“Nimeshindwa kuelewa Chadema na CUF wanaingiaje kwenye mgogoro wakati ni vyama viwili tofauti na tayari CUF wenyewe wamefungua kesi mahakamani wanasubili uamuzi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles