24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mutungi busara zako zinahitajika

Jaji Mutungi
Jaji Mutungi

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

WASOMAJI wa haki hainunuliwi naamini mko salama, kwa wale waliokutana na majaribu nawapa pole kwa uwezo wa Mungu atawafanyia wepesi katika hilo.

Hivi karibuni Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), walifikia makubaliano ya kwenda Dodoma kwa kile walichodai kuhakikisha mikutano ya kisiasa haifanyiki hadi mwaka 2020 ukiwemo wa CCM unaotarajiwa kufanyika Julai 23 mwaka huu.

Maazimio hayo yalisababisha watu kadhaa kukamatwa lakini kutokana na busara za Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe alisitisha mchakato huo.

Vijana hao walitaka kuzuia mkutano kwa kuandaa vijana zaidi ya 4,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini kwenda kuzuia mkutano utakaotumika kumkabidhi Rais Magufuli uenyekiti wa CCM.

Hatua hiyo ilionekana ingesababisha vurugu hivyo Polisi walikemea na kuonyesha kwamba hawahitaji kusaidiwa kufanya kazi na atakayethubutu kufanya hivyo bila kupata ridhaa watamchukulia hatua.

Nawapongeza Chadema kwa kutoa uamuzi wenye busara kwa masilahi ya Watanzania kwa kuepusha vurugu ambazo zingeweza kutokea.

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi aliwahi kusema kwamba chama cha siasa kufanya jambo lililozuiliwa kufanyika ni uhalifu na si siasa.

Alisema kuna wakati busara inahitajika kutawala kwa masilahi ya Watanzania na Taifa kwa ujumla na kwamba pale panapotokea kutoelewana kwa jambo fulani mazungumzo ya meza moja yanahitajika kumaliza sintofahamu.

Wakati umefika kwa Jaji Mutungi kufanya mazungumzo na wanasiasa kujua tatizo liko wapi hasa kufuatia kauli iliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli ambayo ilitafsiriwa kwamba amezuia siasa hadi mwaka 2020.

Kila mmoja aliitafsiri kwa alivyoielewa na ni wazi kabisa inasababisha vuguvugu la maneno ambayo hayapaswi kuendelea kuwepo kwa muda mrefu.

Wanasiasa ni wasikivu siamini kama ukiwaita kwa mazungumzo wanaweza kugoma kufanya hivyo, uamuzi huo unaweza kuzaa faida katika demokrasia.

Kwa kauli yako uliwahi kusema kwamba demokrasia inataka watu wapewe nafasi ya kusema, wanasiasa wameshasema umeyasikia ni jukumu lako kuona mahali gani panahitaji mazungumzo ili kuwekana sawa.

Jaji Mutungi uliwahi kuwaasa wanasiasa wabadili mfumo wa siasa uliopo maana hauleti tija katika mustakabali wa maendeleo ya Taifa, naamini katika uamuzi wa Chadema hilo limezingatiwa.

Hongereni sana Chadema kwa uamuzi wa busara naamini kauli ya Mbowe itasikilizwa ili amani itawale.

Zipo njia mbadala za kudai haki hivyo kwa kutumia busara hiyo pale panapoonekana kuna shaka, hapajaeleweka vizuri au panaleta mkanganyiko kuna haja ya kutumia busara nyingi kumaliza tofauti hiyo ili siasa ziendelee.

Polisi kwa nafasi yao wanahitaji kuwa makini katika siasa kwani kauli na maneno makali yanaweza kuongeza ushawishi kwa jambo husika, katika siasa kila upande unahitaji kutumia busara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles