27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MUTUNGI AVIONYA VYAMA VYA SIASA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ameviasa vyama vya siasa kuepuka vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani, ili kuhakikisha kunakuwapo na uwanja sawa wa ushindani katika uchaguzi mdogo wa madiwani.

Kampeni  za uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 zilianza Oktoba 26 na zinatarajiwa  kuhitimishwa Novemba  25 mwaka huu.

Akizungumza jana alisema zimebainika kasoro ndogondogo ambazo si ishara nzuri kuelekea uchaguzi wa amani.

“Si jambo lenye tija kuacha kasoro hizi ziote mizizi, tunastahili kukemea kwa nguvu zote, hivyo kila chama kitekeleze wajibu wake ili uchaguzi huu ufanyike kwa amani na utulivu.

“Vyama vya siasa na wagombea wote wanaoshiriki katika uchaguzi huu waepuke kutumia maneno ya uongo na yenye  kuudhi, matusi, uchochezi, kashfa, na mambo yanayofanana na hayo kwani ni kinyume na sheria na badala yake vyama vinadi sera zao,” alisema Jaji Mutungi.

Aliviataka vyama hivyo kuepuka vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani na kuepuka propaganda ambazo zinawatia hofu wananchi na wapigakura.

Jaji Mutungi alisema vyama havipaswi kujichukulia sheria mkononi wala kujihusisha na vitendo vya uchokozi kama vile kuingilia mikutano ya kampeni ya chama kingine, kuchoma ama kuchana bendera/ mabango ya chama kingine.

“Msijihusishe na vitendo vyovyote vya rushwa, kununua wapigakura au kuuza shahada ya mpiga kura. Kuepuka propaganda ambazo zinawatia hofu wananchi na wapigakura,” alisema.

Alisema vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo vina wajibu wa kisheria wa kuwaasa na kuwadhibiti wanachama na wagombea wao kuheshimu na kufuata sheria zote zinazohusika.

Alisema kila chama cha siasa ambacho kinashiriki katika uchaguzi huo kinapaswa kuwashawishi wananchi kwa sera zake na si vinginevyo.

“Lengo ni kuhakiksha kuwa kunakuwepo uwanja sawa wa ushindani katika uchaguzi, hakuna chama chochote kinachoingilia mikutano ya chama kingine kwa kufanya vurugu, kuepusha matumizi makubwa ya fedha na kuweka uwazi katika matumizi ya fedha na rasilimali nyingine katika kampeni,” alisema.

Alisema pia maofisa kutoka katika ofisi yake wapo katika kata zote 43 wakifanya uangalizi wa karibu kubaini ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Miongoni mwa majukumu ambayo yanatekelezwa na maafisa hao ni pamoja na kutoa mafunzo elekezi kwa vyama vya siasa, wagombea wa udiwani, viongozi wao na wananchi juu ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi na matendo yaliyokatazwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles