31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MKUU: LISSU NI JARIBIO LA MAUAJI

  • Asema kilichomtokea ni funzo kwa nchi, Ataka uchunguzi ubaini waliohusika

NA WAANDISHI WETU

TUKIO la kushambuliwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), limezidi kuchukua sura mpya baada ya Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, kusema kuwa ni la uhalifu wa kujaribu kuua, huku Chama cha Wanasheria Uingereza kikimwandikia barua nzito Rais Dk. John Magufuli.

Mbali na hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, naye ameibuka akisema kuwa Serikali ipo tayari kugharamia matibabu ya Lissu popote duniani.

Kauli ya waziri huyo imekuja muda mfupi baada ya Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM), kusema kwamba madaktari wa Kenya wameeleza kuwa Lissu hawezi kusafirishwa kwenda nje kupatiwa matibabu kwa sasa.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu mjini Dodoma.

 ALICHOSEMA JAJI MKUU

Jaji Mkuu Profesa Juma, alisema tukio la kushambuliwa kwa risasi mbunge huyo wa Singida Mashariki na watu wasiojulikana ni tukio la uhalifu mkubwa, la kujaribu kuua ambalo ushahidi wake unatakiwa kukusanywa nchini.

Alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana, kuhusu mkutano wa majaji na mahakimu wa Jumuiya ya Madola unaofanyika kwa mara ya kwanza nchini kuanzia Septemba 24 hadi Septemba 28.

Profesa Juma alisema kitu cha kwanza katika tukio hilo ni kukusanya ushahidi na kwamba kilichotokea kwa Lissu ni funzo kwa nchi kuona ni namna gani nchi zimejipanga kupambana na uhalifu.

“Nchi nyingine ikiwemo Kenya, mjini Nairobi kumefungwa kamera za CCTV kila sehemu kwenye barabara kuu na kwenye nyumba, ambao huo ni ushahidi wa kutosha.

“Nadhani tumekubaliana, hili ni tukio la kihalifu, uhalifu mkubwa sio mdogo, ni jaribio la kuua. Kitu cha kwanza ni kukusanya ushahidi na huo ushahidi utakusanywa hapa hapa Tanzania, asikudanganye kwamba mtu kutoka nje atakuwa na uwezo wa kukusanya ushahidi. Ushahidi unakusanywa Tanzania,” alisema.

WARAKA WA WANASHERIA UINGEREZA

Vyombo vitatu vya wanasheria nchini Uingereza kwa pamoja vimeandika na kutuma waraka mzito kwa Rais Magufuli, vikieleza kusikitishwa na mlolongo wa matukio yaliyomkuta Lissu, likiwamo lile la kupigwa risasi na watu wasiofahamika.

Lakini pia si tu kuhusu vitisho vinavyomkabili Lissu, bali pia uwapo wa tishio la kuifuta TLS na kulipuliwa kwa mabomu kwa ofisi za mawakili ya IMMMA, ambayo walieleza kufahamu kuwa ina uhusiano na mwanasheria huyo wa Chadema.

Kwa sababu hizo na nyinginezo, vyama hivyo; Chama cha Wanasheria, Baraza la Wanasheria na Tume ya Wanasheria wa Haki za Binadamu, vimelaani vikali matukio hayo na kutoa wito kutaka chombo huru kipewe nafasi ya kufanya uchunguzi wa matukio hayo na kupigwa risasi kwa Lissu.

Vyama hivyo pia viliorodhesha mlolongo wa matukio ya kukamatwa kwa Lissu ikiwamo mahakamani na wakati alipokuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akiwa njiani kwenda kuhudhuria mkutano mjini Kigali, Rwanda.

Tukio la kukamatwa uwanja wa ndege, lilikuja licha ya awali alipokuwa mahakamani mjini Dodoma, polisi walimhakikishia kuwa hawana mpango wa kumkamata.

Vyama hivyo vilieleza kuwa matukio ya kumkamata Lissu bila sababu za msingi kisheria, ni ukiukaji wa sheria za kimataifa ambazo Tanzania imeridhia na kuzisaini.

“Tukio la kumpiga risasi Lissu na mengineyo yaliyotokea kwa wanasheria pamoja na tishio la kutaka kuifuta TLS yanasitikisha sana. Ni muhimu ieleweke kuwa uhuru wa vyama vya wanasheria unapaswa kuheshimiwa kwa sababu ni vyombo muhimu vya kuhakikisha ufanisi wa utawala wa sheria.

“Februari  2017, tunafahamu kwamba aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, alitoa onyo la kuifuta TLS kwa sababu za ‘harakati za kisiasa.’

“Mwezi uliopita mabomu mawili yalilipuliwa katika lango la ofisi ya IMMMA Advocate. Tunafahamu kwamba mmoja wa wanasheria katika kampuni hiyo amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali kuhusu kukiukwa kwa utawala wa sheria na amekuwa akiituhumu kuingilia mhimili wa mahakama,” umesema waraka wa vyama hivyo.

Vilikumbushia kuwa Tanzania iliridhia na kusaini mikataba ya kimataifa ikiwamo ya haki za kiraia na kisiasa wa Juni 11, 1976, ambao pamoja na mambo mengine, unasisitiza haki za kuishi, usalama, kutoa maoni, kukusanyika na kadhalika.

Aidha vilikumbushia kuwa Tanzania ilisani Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu Februari 18, 1984 na ule wa Umoja wa Mataifa unaohakikisha wanasheria wanafanya kazi kwa uhuru bila vitisho.

“Tunatoa wito kuundwa kwa chombo huru kuchunguza sababu na mazingira ya kupigwa risasi kwa Lissu pamoja na uhalifu mwingine uliofanywa dhidi ya wanasheria na wahusika kushtakiwa kwa mujibu wa mchakato wa viwango vya kimataifa,” vilisema.

Aidha wametaka kufutwa kwa mashitaka yanayomkabili Lissu isipokuwa tu kama kuna ushahidi wa kutosha kisheria.

Pia wameitaka Tanzania itii na kufuata mikataba na sheria za kimataifa ilizoridhia na kuzisaini na kuhakikisha wanasheria wanafanya kazi zao bila vitisho, ukandamizaji na mwingilio usio na sababu.

Kwa ufupi vyama hivyo vilisema vinasubiri uhakikisho kuwa uhuru wa TLS utaheshimiwa, waliompiga risasi Lissu wanashtakiwa, mashtaka yanayomkabili yanapitiwa upya na wenzake wanahakikishiwa usalama.

Nakala ya waraka huo pamoja na wengine imetumwa pia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, IGP, Spika na Jaji Mkuu wa Tanzania.

AZUNGUMZIA TAMKO LA WANASHERIA WA UINGEREZA

Akizungumzia kuhusu tamko la Chama cha Wanasheria Uingereza, alisema kanuni zao, hawaruhusiwi kutoa maoni wala kuongelea jambo moja kwa moja ambalo litafika mahakamani, ndiyo maana wamekaa kimya.

“Tuko kimya, hatutasema kwa jambo ambalo litakuja mahakamani. Mnajaribu kutuvuta, tumekaa kimya. Hata aliposhambuliwa hakimu hadi kusababisha kifo, tulikaa kimya. Tuache sheria zifanye kazi, pale tutakapoona waliopewa jukumu la kukusanya ushahidi wakikaa kimya, tutapiga kelele,” alisema Profesa Juma.

UHURU WA MAHAKAMA

Alipotakiwa kuzungumzia uhuru wa mahakama, alisema chombo hicho ni huru sana kimfumo na binafsi.

“Jaji Mkuu hawezi kuingilia hakimu yeyote katika kufanya kazi, hata awe wa mahakama ya mwanzo, shughuli za mahakama ziko wazi zaidi kuliko za mihimili mingine.

“Kuna utaratibu, amri ya mahakama ikivunjwa unatakiwa kurudi katika mahakama hiyohiyo iliyotoa uamuzi. Vyama vya siasa vinaniandikiaga barua kutaka Jaji Mkuu aingilie hili, lakini nawajibu wafuate utaratibu,” alisema.

KUJILINGANISHA NA MAHAKAMA ZA KENYA

Alipotakiwa kulinganisha mahakama zetu na Kenya, alisema hatutakiwi kujilinganisha nayo kwa sababu kila nchi ina sheria zake na historia yake.

Alisema Mahakama ya Juu nchini Kenya, ilipewa mamlaka ya kusikiliza mashauri kama hayo ya matokeo ya urais, lakini wao hawajapewa mamlaka hayo.

“Waangalizi wa uchaguzi wanatupima kwa kuangalia sheria zetu tunazotumia kupata jaji,” alisema Profesa Juma.

MKUTANO WA MAJAJI NA MAHAKIMU

Akizungumzia mkutano wao, alisema utafunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Septemba 25 katika ukumbi wa Benki Kuu na kufungwa Septemba 27 na Rais wa Zanzibar, Dk. Mohammed Ali Shein.

Alisema maudhui ya mkutano huo ni mahakama madhubuti, inayowajibika na jumuishi.

Mkutano huo utahudhuriwa na majaji wakuu 13 kutoka nchi mbalimbali zikiwamo Guyana, Uganda, Malawi, Turks & Caicos Islands, Swaziland, Lesotho, Zanzibar na Tanzania.

Alisema washiriki katika mkutano huo ni 354 na malengo yake ni kuwajengea uelewa wajumbe kuhusu uhuru wa mahakama, mikataba ya kimataifa, maendeleo ya kisheria, upatikanaji wa huduma ya haki na changamoto za mahakama katika usikilizaji wa mashauri.

Alisema mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwamo masuala ya ugaidi ambayo changamoto ni namna gani ushahidi unatumika.

Jaji Kiongozi Fredrick Wambali alisema katika mkutano huo pia watajadili makosa ya kimtandao kuangalia nani anapaswa kushtakiwa kati ya aliyetuma ama aliyepokea.

Alisema watajadili pia namna gani watafanya kuomba msaada kwa nchi nyingine ili aliyetenda kosa kama yuko nje ya nchi aweze kushtakiwa.

KAULI YA WAZIRI UMMY

Wakati huo hu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema Serikali ipo tayari kugharamia matibabu ya Lissu mahali popote duniani.

Hata hivyo, katika maelezo yake, alisema Serikali itafanya hivyo kama familia itawasilisha maombi rasmi serikalini ya kuhitaji kupatiwa ufadhili wa matibabu hayo.

“Kama familia itakuwa tayari kupatiwa ufadhili huo wa Serikali, sisi tupo tayari ila tunachosubiri ni kupatiwa taarifa rasmi kuhusu uhitaji uliopo wa matibabu zaidi, iwe ni India, Ujerumani au hata Marekani, tutampeleka.

“Tunachohitaji katika hili ni maombi rasmi yawasilishwe, yakiwa yameambatana na taarifa za madaktari ili Serikali kupitia wizara yetu tuweze kuyafanyia kazi,” alisema.

Pamoja na hayo, alisema tangu mbunge huyo aanze kupatiwa matibabu nchini Kenya, hawajapata taarifa ya uhitaji wa matibabu.

Hata hivyo, waziri huyo alionyesha kukerwa na utaratibu wa kuendesha michango kwa wananchi wanaochangia fedha za matibabu ya mbunge huyo.

“Dhamira ya wananchi kuchangishwa fedha za matibabu sisi kama Serikali tunaona haijakaa sawa, kwani wanaweza kuibuka matapeli ambao wataweza kutumia mgongo huo kujinufaisha,” alisema.

Pamoja na hayo, alionyesha pia kukerwa na taarifa za upotoshaji juu ya matibabu ya Lissu, zinazosema Serikali imemtelekeza wakati ikijua anahitaji matibabu.

MAJIBU YA LEMA KWA UMMY

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alimtaka waziri huyo kuacha kutapatapa.

Nataka nimjibu Ummy kwamba aache kujitapatapa, hakunaga mbunge hata mmoja ambaye familia yake au ndugu anaandika matibabu kwa ajili ya mbunge, mke wa Spika hakuandika barua kuomba Spika atibiwe na ni mbunge.

“Huko nyuma Mbunge wa Geita alishalazwa zaidi ya mwaka hospitalini, lakini familia haikuandika barua, ilikuwa ni suala la bima, Mwandosya (aliyekuwa Mbunge wa Rungwe, Mark Mwandosya) aliumwa muda mrefu sana Bunge lililopita, familia yake haikuwahi kuandika barua atibiwe,” alisema Lema.

Alisema Bunge linatambua wabunge wake wote aliowaapisha na ndio sababu inawapa bima za afya, hivyo mbunge anapoumwa si wajibu wake au familia yake kuandika barua.

“Ni wajibu wa Bunge na Serikali kumtibu mbunge wake kama ambavyo inafanya kwa viongozi wengine wa Serikali.

“Sasa Ummy anatapatapa kwa sababu hii aibu imekuwa kubwa na wanaona kusudio limeshindikana na wanafuatilia taarifa ya mgonjwa wanajua Mungu anavyompigania.

“Lakini Lissu alipigwa risasi Septemba 7, Ummy anasema familia iandike barua Septemba 21,” alisema Leman a kuongeza kuwa hana uhakika kama chama kitakubaliana na hilo.

Aliongeza: “Lakini wanaogopa kwa sababu mpaka mwaka 2020 itakuwa si kweli Lissu atakuwa amepata matatizo ya ajali kama alivyopata, hata wabunge wao wengi watapata matatizo tu au hata yeye mwenyewe kwa sababu hakuna aijuaye kesho.

“Sasa kwamba familia iandike barua ni kutapatapa na kuyumba kwa Bunge na Serikali, hatutashindwa kumtibu Lissu bila msaada wa Serikali, hapa tulipofika tumefika bila msaada wa Serikali, tumefika kwa msaada wa wengi na hela za Watanzania wanaopenda umoja.

“Hili la Ummy limekuja baada ya mbunge wao ambaye wanamwona ni msaliti akifanya kazi ya kumwuguza mgonjwa, ambaye ni Lazaro Nyalandu.

“Kwa hiyo wanajaribu kujiosha kwa ulimwengu wa kimataifa na mataifa, kwamba wana-concern, lakini hawana concern yoyote, leo ni siku ya 21 Spika, Naibu wake hawajawahi kukanyaga kumwona Lissu wala Katibu wa Bunge wala Sekretarieti ya Bunge.

“Na zaidi kabisa wamemnyang’anya Freeman Mbowe gari, lile gari lililokuwa linamhudumia mwenyekiti wamelirudisha Tanzania.

“Kwa hiyo hawa watu wana roho mbaya, ingekuwa huyu mbunge hili shambulio hakulijua Sekretarieti ya Bunge ingekuwa imeshafika kule kama ambavyo wangekuwa wanawahi misiba.

“Nina uhakika kama wangekuwa wamepata taarifa mbaya ya msiba, wangeshafika kule na kununua jeneza la bei mbaya, utaratibu na mbwembwe za kuzika.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles