23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI LUBUVA AKUMBUKA MACHUNGU NEC

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, amezungumzia machungu aliyokumbana nayo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Amesema uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkubwa na wakati mwingine alipokea malalamiko mengi kutoka kwa vyama vya siasa, lakini anashukuru Mungu uchaguzi huo uliisha kwa amani.

Jaji Lubuva alifichua hali hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam jana.

Pamoja na mambo mengine, Jaji Lubuva alikuwa akitoa maoni yake kuhusu uchaguzi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) uliofanyika Aprili 14 mwaka huu jijini Arusha, huku akitoa nasaha zake kwa Rais mpya wa chama hicho Fatma Karume.

“Ni kweli lawama zilikuwepo wakati ule wa uchaguzi wa mwaka 2015, lakini pamoja na lawama hizo mimi ni miongoni mwa waliopitia ofisi nyingi.

“Kimsingi Tume ya Uchaguzi haikumpendelea mtu yeyote wala chama chochote, lakini nilipata faraja baada ya matokeo yote kutoka na tukahitimisha kazi ile,” alisema.

Jaji Lubuva ambaye alipata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye Tanzania Bara, alikiri uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkubwa tofauti na uchaguzi mwingine wa nyuma.

“Tuliendesha uchaguzi kwa ufanisi mkubwa pamoja na ushindani mkubwa lakini uliisha kwa amani. Hata waangalizi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakati ule wa uchaguzi walinieleza awamu hii…walitegemea kwamba vurugu zingetokea lakini mwishoni wakashangazwa uchaguzi kumalizika kwa salama na amani,” alisema.

Akizungumzia changamoto alizokumbana nazo akiwa NEC, alisema mara nyingi ilikuwa mafungu ya fedha kutotosha.

“Uchaguzi uliopita changamoto kubwa ilikuwa ni mashine za BVR ambapo ulitumika mfumo mpya. Tulikuwa tunahama na zile mashine lakini katika changamoto zote tulizozipata tulipewa ushirikiano mkubwa serikalini,”alisema.

Alipoulizwa ni kitu gani cha kujivunia alichokiacha NEC alisema. “Niliondoka kifua mbele kwa maana kwamba nilifanya kazi kwa ufanisi kwa kushirikiana na wenzangu. Napumzika kwa amani kwa maana kazi nilikamilisha vizuri,” alisema.

MADED

Akizungumzia kuhusu wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi, alisema pamoja na kwamba ni makada wa vyama lakini wanafuata maelekezo kutoka NEC.

“Huwa wanaapa kuwa watazingatia maelekezo ya tume na si ya mtu yeyote. Azma ni kuwa na watumishi wa tume nchi nzima, lakini lazima kwenda hatua kwa hatua,”alisema.

AMPONGEZA FATMA KARUME

Kuhusu uchaguzi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Jaji Lubuva alimpongeza Rais mpya wa chama hicho, Fatma Karume kwa kuaminiwa na wanataaluma wenzake.

Alisema binti huyo wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume anafaa kutokana na ujasiri alionao kwa kusimamia kile anachokiamini tangu anaanza kazi za sheria.

“Nikiwa mwanasheria wa Zanzibar, nilikuwa nafahamiana na wazazi wake, alipoanza kazi ya sheria mimi nilikuwa mahakama ya rufaa alikuwa jasiri pamoja na kwamba hakuwa na uzoefu wa kutosha lakini alifanya kazi zake jinsi inavyostahili.

“Pia Fatma ana sifa nyingine kwa kuwa ni mzanzibari hii inaonyesha Tanzania tumekomaa kwa sababu tunadumisha muungano wetu, ingawa wajumbe wamemchagua kwa kutoangalia anatoka wapi,”alisema.

Aipa somo TLS

Mbali na pongezi hizo, mwanasheria huyo nguli alimtaka kiongozi huyo wa TLS kusimamia vizuri misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho ili kuitendea haki taaluma ya sheria.

Jaji Lubuva alisema TLS ikitimiza majukumu yake vizuri itasaidia muhimili wa mahakama kufanya kazi zake vizuri katika suala zima la utoaji wa haki.

Hata hivyo mwanasheria huyo alionesha kutoridhishwa na tabia za baadhi ya mawakili ambao wamekuwa ‘wafanyabiashara’ kwa kujali zaidi maslahi ya kifedha na kuwaacha wananchi wanyonge wakidhulumiwa haki zao.

“TLS inawajibu wa kuhakikisha misingi yake inafuatwa na hasa maadili ya kitaaluma, siku hizi wanaoingia kwenye fani hii wengi wao ni vijana, wanafikiria zaidi fedha kuliko maadili ya kitaaluma.

“Hii ni hatari sana, kwani wananchi wakivunjika moyo na kukosa imani na wanasheria ndiyo kusema kwamba watakosa pia imani na mahakama, jambo ambalo si zuri,” alisema.

Alisema aliufuatilia uchaguzi wa TLS uliofanyika na kwamba aliviona vipaumbele vya Fatma, lakini akashauri wazingatie suala la maadili na ujuzi katika taaluma hiyo.

“Nakubaliana na vipaumbele vyake alivyovitoa lakini kwa maoni yangu, ingefaa wakaongeza pia na suala la maadili katika taaluma kwa mawakili na kuongeza ujuzi wao ambayo inasisitizwa katika kifungu cha 4 (1)(2) ya Sheria ya Mawakili.

“Pia TLS ifikirie utaratibu wa kuanzisha rasmi utaratibu au mfumo wa kuwa na mawakili wa ngazi mbalimbali yaani kuwe na mawakili waandamizi na madaraja mengine tofauti na hali ilivyo sasa,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles