24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji akumbusha machungu kifo cha Daudi Mwangosi

kaka1NA SHABANI MATUTU,DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) aliyemaliza muda wake, Jaji Amir Manento, ameonyesha kutofurahishwa na Serikali kushindwa kutekeleza ripoti iliyotolewa na tume hiyo kuhusu mauaji ya mwandishi wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.
Jaji Maneto aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati wa hafla ya kuapishwa kwa mwenyekiti mpya wa tume hiyo, Bahame Nyanduga na makamishna wake.
“Pamoja na kustaafu, jambo ambalo sitalisahau ambalo linaumiza kichwa changu ni namna ambavyo Serikali imeshindwa kutelekeza ripoti ya mauaji ya Mwangosi.
“Wananchi walipokea vizuri ripoti yetu, lakini nasikitishwa ambavyo viongozi wa Serikali walivyoshindwa kulichukulia hatua jambo hili, wakiona ni mwiba kwao,” alisema.
Alisema ripoti hiyo kwa sehemu kubwa ilionyesha namna ambavyo watendaji wa Serikali walionyesha uzembe uliochangia kuuawa kwa Mwangosi.
“Kucheleweshwa kwa haki ya Mwangosi, kisheria ni sawa na kumnyima haki yake, katika sheria tunatambua suala la kucheleweshewa haki ni sawa na kunyimwa haki kwa mhusika,” alisema.
Pamoja na haki hiyo kucheleweshwa, Jaji Manento anaamini huenda Mwenyekiti mpya Nyanduga, atasimamia pale walipokuwa wamelifikisha wao ili haki ipatikane.
Mwangosi, aliyekuwa mwandishi wa habari wa Chanel Ten Mkoa wa Iringa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa mkoa huo, aliuawa Septemba 2, 2012 kwa kitu ambacho kinasaidikiwa kuwa ni bomu.
Katika tukio hilo, Mwangosi alikamatwa na zaidi ya polisi watano, huku mmoja akionekana kumnyoshea bunduki sehemu za tumbo lake.
Tukio hilo, lilitokea katika Kijiji cha Nyololo wakati alipokuwa akitimiza wajibu wake kwenye uzinduzi wa tawi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Tume iliwahusisha maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema.
Katika ripoti ya tume hiyo iliyokuwa chini ya Jaji Manento, ilionyesha kulikuwa na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na kushauri kwamba ili kuwapo kwa utawala bora mamlaka zote za Serikali ni lazima zifuate utawala wa sheria.
Katika taarifa yao ilibaini aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, Septemba 2, 2012 katika utekelezaji wa majukumu yake alikiuka Sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11(a) na (b) na sheria ya Polisi (Sura ya 322) kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za Chadema wakati hakuwa “Officer In-charge” wa polisi wa eneo husika.
“Kwa maana hiyo, amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka kisheria wa kuitoa. Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka, hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora,” ilisema sehemu ya taarifa yao.
Wengine walioapishwa na Rais Kikwete jana ni Iddi Ramadhani Mapuri anayekuwa Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo.
Vile vile aliwateua makamishna ambao ni Rehema Ntimizi, Mohamed Hamadi, Salma Ali Hassan na Dk. Kevin Mandopi.
Kabla ya kuwaapisha, Rais Kikwete alianza kumuapisha Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Katarina Revocati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles