JAFO: HALMASHAURI ZENYE MADENI SUGU LIPENI WENGINE WAKOPE

0
5
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa, Richard Mfugali kuacha kukaa ofisini na kuzitembelea halmashauri zote zinazodaiwa kukusanya madeni hayo haraka ili taasisi hiyo iweze kutekeleza majukumu yake.

Amesema hatua hiyo ni itatoa nafasi kwa halmashauri nyingine zenye uhitaji kuendelea mikopo inayotolewa na taasisi hiyo ambapo pia amezitaka halmashauri zilizokopa kulipa madeni yao kabla ya Desemba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma leo Alhamisi, Oktoba 12, Waziri Jafo amesema japo halmashauri nyingi zimejitahidi kurejesha mikopo lakini kuna Halmashauri tisa zimeonyesha usugu uliopitiliza katika kurejesha mikopo hiyo ambazo zina jumla ya deni la zaidi ya Sh bilioni mbili ambapo hatua hiyo inazinyima fursa halmashauri nyingine kupata mikopo.

“Pamoja na mambo mengine, naomba bodi itoe mikopo katika halmashauri zinazolenga kutekeleza miradi ya viwanda na uwekezaji mdogo na mkubwa ili kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema Jafo.

Amezitaja baadhi ya halmashauri zinazodaiwa kuwa ni Jiji la Mwanza, Mbeya, Manispaa ya Moshi, Mbinga, Pangani na nyingine.

Hata hivyo, Jafo amesema hadi Septemba mwaka huu, Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 9.742 kwa halmashauri 54 kati ya 185 zilizopo hivi sasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here