30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

IRELAND WAPIGA KURA KURUHUSU UTOAJI MIMBA

DUBLIN, IRELAND        |     


WANANCHI nchini Ireland wamepiga kura kwa wingi kuliko ilivyotarajiwa ili kubadilisha baadhi ya sheria kali za utoaji mimba.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni ya kura hiyo ya kihistoria, ni kwa minajili ya kuondoa marufuku iliyomo katika nchi hiyo ambayo kimsingi ina Wakatoliki wengi.

Katiba ya Ireland ilipiga marufuku kutoa mimba isipokuwa tu katika wakati ambao maisha ya mama yamo hatarini, lakini zoezi la upigaji kura limeonyesha wananchi wanaounga mkono utoaji mimba wanatarajiwa kushinda kwa wingi wa theluthi mbili ya kura.

Gazeti la Irish Times limesema kuwa, uchunguzi wao umeonesha kwamba, asilimia 68 ya wananchi wa Ireland walipiga kura ya ‘ndiyo’ kufanya mabadiliko ya nane ya Katiba, wakati uchunguzi wa maoni uliofanywa na kituo cha Televisheni ya Taifa, RTE, kimeweka idadi ya wanaokubali ni asilimia 69.4.

Taasisi ya uchunguzi wa maoni ya Ipsos nayo iliwauliza zaidi ya wapiga kura 4,500 katika maeneo 160 ya kupigia kura katika kila jimbo ili kubaini idadi ya wanaounga mkono na wale wasiokubali.

Uchunguzi wa RTE ulihusisha watu 3,800 na ukiwa na wastani wa makosa wa asilimia 1.6. Umeonesha mgawanyiko mkubwa miongoni mwa makundi ya umri, ambapo asilimia 87.6 ya watu wenye umri kati ya miaka 18-24 wamepiga kura ya ‘Ndiyo’, wakati watu wenye umri wa miaka 65 na kuendelea ni kundi pekee lililokataa mabadiliko, na asilimia 58.7 walipiga kura ya ‘Hapana’.

RTE wamesema kuwa, watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa wengi na katika baadhi ya maeneo kumeripotiwa idadi ya zaidi ya asilimia 70.

“Inaonekana kuwa tutaandika historia kesho (jana),” ameandika kwenye ukurasa wa Twitter Waziri Mkuu Leo Varadkar, ambaye amefanya kampeni ya ‘Ndiyo’.

Matokeo rasmi yalitarajiwa kutangazwa jana. Kura hiyo imeligawa taifa hilo, ambalo kimsingi lina waumini wengi wa Kikatoliki, huku kukiwa na hisia kali katika pande zote zilizoshiriki katika mjadala huo.

Utoaji mimba unaruhusiwa tu kwa sasa iwapo maisha ya mama yamo hatarini, lakini si katika matukio ya kubakwa au udhalilishaji kingono kupitia ndugu.

Kiongozi wa upinzani wa Chama cha Sinn Fein, Mary Lou McDonald, ambaye pia alifanya kampeni ya ‘Ndiyo’, ameieleza kura hiyo ya maoni kuwa ni kufunga ahadi na hatima kwa wananchi wote wakati akipiga kura yake mjini Dublin.

Kura hiyo ilifuatia miezi kadhaa ya mjadala mkali baina ya wale wanaofanya kampeni ya kura ya ‘Ndiyo’ na ‘Hapana’ juu ya iwapo nchi hiyo ifanye mabadiliko yake ya nane ya katiba, ambayo inampa mama na mtoto ambaye bado hajazaliwa haki sawa ya kuishi iwapo itabadilishwa.

Wapiga kura waliulizwa iwapo wanataka kuendelea na sheria hiyo ua kuibadilisha pamoja na kuongezwa kipengele kipya katika katiba ambacho kitatoa uwezo kwa Bunge kuhalalisha utoaji mimba.

Kambi ya waliokuwa wanafanya kampeni ya ‘Ndiyo’ wanadai kwamba kifungu hicho cha sheria kiliwazuia madaktari kufanya utoaji mimba hata wakati maisha ya mama yalikuwa hatarini.

Zaidi ya watu milioni 3.2 waliandikishwa kupiga kura katika kura hiyo ya maoni, ambayo inafuatia miito ya mara kwa mara kutoka Umoja wa Mataifa kuifanyia mabadiliko sheria hiyo nchini Ireland na kuwa katika mstari moja na viwango vya sheria za kimataifa za haki za binadamu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles