Wednesday, May 22nd

You are here
Banner
Banner

Serikali yatangaza ajira mpya kwa walimu

SERIKALI imetangaza mpango mpya wa ajira za walimu 28,638 wa shule za msingi na sekondari, katika mikoa inayokabiliwa na changamoto ya uhaba wa walimu.

Mpango huo ulitangazwa juzi na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, wakati akizungumza katika mahafali ya nne ya Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (MUCE) mkoani Iringa.

Akizungumzia mpango huo, Mulugo alisema walimu watakaomaliza masomo yao awamu hii, wataajiriwa katika maeneo ya vijijini na si katika shule zilizopo mijini kama ilivyozoeleka.

“Tutawaajiri wote hapa hapa, lakini safari hii, hakuna ajira mijini na wote mtakaoajiriwa, tunawapeleka katika wilaya zenye changamoto ya utumishi,” alisema.

Aliitaja mikoa ya changamoto hiyo kuwa ni pamoja na Katavi, Kigoma, Rukwa, Mbeya, Shinyanga, Manyara, Mtwara na Lindi.

Mulugo alisema licha ya Serikali kupanga kuajiri walimu 28,638 utafiti unaonyesha kuwa walimu wote waliopo katika vyuo vya ualimu, havikidhi idadi ya uhitaji wa Serikali.

Alisema ajira hizo kwa mujibu wa ikama ya Serikali, zitatangazwa rasmi Januari mwakani, huku akiwaonya wahitimu wa shahada ya kwanza ya ualimu katika fani mbalimbali.

Mulugo aliwataka wahitimu hao wasithubutu kupenyeza vijinyaraka kwa wakubwa wizarani, kuomba kuteuliwa kuwa maofisa elimu wa wilaya na mikoa.

Naibu waziri huyo alisema, Serikali imegundua tatizo kuhusu walimu waliotoroka kazini na kujiunga na vyuo vya elimu ya juu pasipo ridhaa ya mwajiri.

Alisema tatizo hilo limeiathiri zaidi mikoa iliyopo Kanda ya Ziwa na mikoa ya Kaskazini, ambayo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu.

“Nawatangazia kiama, wale ambao walitoroka kazini na kuja kujiunga na vyuo vya elimu ya juu pasipo ridhaa ya mwajiri wake…Wizara imewaagiza maofisa elimu wa wilaya na mikoa, kuleta haraka majina hayo wizarani ili tuchukue hatua,” alisema Mulugo.

Mkuu wa chuo hicho, Prof. Amandina Lihamba alisema baadhi ya miradi ya ujenzi wa miundo mbinu imekwama na hivyo kuathiri shughuli za taaluma chuoni hapo.

Alisema ni asilimia 49 ya wanafunzi ndiyo wanaoishi ndani ya chuo na kwamba asilimia 51 iliyosalia wanaishi nje ya chuo, jambo ambalo alisema ni moja ya changamoto kubwa.

Profesa Lihamba alisema, chuo chake kimepokea Sh  bil 1.3 tu kutoka Hazina, zilizoidhinishwa na Serikali na kueleza kuwa, fedha hiyo haitoshi kukamilisha miradi ya chuo hicho.

Maoni   

 
0 #3 Dr. Boa Mathias 2013-05-17 07:46
Kwa kweli ualimu ni wito; hivyo basi mwlimu akipangiwa kazi sehemu yoyote ni lazima aende. Aende akatusaidie kufudisha watoto wa watanzania wenzake ili waelewe mabo vizuri. Sasa wanapong'angani a mjini wote; shule zetu za kata watoto watfundishwa na nani? Tusibembelezane ; watoto kufeli namna hii ni janga la taifa! Hivyo ili jambo hili lisijirudie tena, ni lazima serikali ihakikishe waalimu walio-"qualify" wanaenda huko na kufundisha vizuri. Si kufundisha alimuradi tu siku zinaenda. Pia waalimu waliostaafu na wanexperience zuri waajiriwe kwa mkataba tuondokane na tatizo hili ones and for all. ni hatari sana kuwa na taifa la mambumbu! Mungu apishilie mabli hili.
Nukuu
 
 
-2 #2 denis 2013-01-13 15:05
mi naipongeza serikali ya rais wetu kwa kazi nzuri ya kutoa ajira kama wajibu wa serikali zote zenye mamlaka hapa duniani,lakini uhuru wa mfanyakazi ni kama haupo,hii ni kutokana na mfanyakazi kulazimishwa kufanya kazi sehemu asio itaka,na mazingira mabovu mbona viongozi wao hupenda mazira bora,m naishauri serikali kua ili kutatu tatizo la uhaba wa walimu ni maslahi bora,au wakishindwa basi chama cha walimu kivunjwe ianzishe benki ya walimu yenye riba ndogo,ili serikali ipunguze mzigo wa kutegemewa. walimu watafanya biashara hata huko vijijini mnapo pakataa nyie viongozi .swala ni ubunifu wa wizara c udictator .
Nukuu
 
 
0 #1 Benson 2012-11-19 07:24
Mimi napenda kuunga mkono haja iliyowahi kutolewa na Naibu Spika katika kipindi fulani cha mahojiano kwenye TV, pale aliposema kwamba, ingekuwa vizuri kama hizi nafasi za kazi za waalimu, madaktari na wafanyakazi muhimu katika idara za serikali, zikawa zinatangazwa na Mikoa husika, ili kwamba wale wote wanaoajiriwa kupitia matangazo hayo, kuwe na uhakika wa wao kudumu kwenye nafasi hizo bila kukimbilia kwingine. Maana wengi wanaoajiriwa kupitia Wizara, wakitumwa mikoani wanakimbia kwa kisingizio cha hali ngumu, ilhali kuna watu wanaotamani kufanya kazi hukohuko wasikokutaka. Serikali iliangalie hili wazo la Mheshimiwa Ndugai.
Nukuu
 

Toa Maoni yako kwa habari hii


Neno la usalama
Huisha

Airtel, leader of the market
Banner