25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ijue historia ya Aston Villa aliko Mbwana Samatta

Badi Mchomolo

LIGI Kuu ya England ni miongoni mwa Ligi ambazo zinatazamwa na idadi kubwa ya watu duniani huku ikitajwa kuwa namba moja kwa soko la mpira wa miguu.

Ligi hiyo imekuwa na mashabiki wengi katika kila kona ya dunia kuliko ligi nyingine yoyote. Kabla ya Januari 20 mwaka huu, Tanzania haijawahi kuwa na mchezaji anayekipiga katika Ligi hiyo.

Mbali na kukosa mchezaji wa kuipeperusha bendera ya Tanzania, lakini mashabiki wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kuiangalia Ligi hiyo kila mwishoni mwa wiki kuliko Ligi yoyote.

Sasa ni wakati ambao mashabiki wa Kitanzania watazidi kuitazama mara baada ya Mbwana Samatta nahodha wa timu ya taifa Tanzania (Taifa Stars), kujiunga na klabu ya Aston Villa kwa mkataba wa miaka minne na nusu akitokea K.R.C Genk ya nchini Ubelgiji.

Wapo ambao wanashangaa kuona kwa nini Samatta amejiunga na klabu hiyo ambayo ipo hatarini kushuka daraja ikiwa inashika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi.

Mbali na kushika nafasi ya 16, lakini timu hiyo imekuwa na uhakika wa kushiriki Ligi Kuu mara kwa mara, viongozi wenyewe wanaamini itaendelea kubakia kwenye Ligi hiyo msimu ujao. Ijue Aston Villa kwa undani zaidi.

Ilianzishwa mwaka gani?

Hii ni klabu ambayo ipo mjini Birmingham, ilianzishwa Machi 1874, huku ikitumia uwanja wa nyumbani unaojulikana kwa jina la Villa Park tangu mwaka 1897.

Aston Villa ni miongoni mwa klabu ambazo zilianzisha ligi mwaka 1888, pia Ligi Kuu England mwaka 1992.

Klabu hiyo ipo chini ya kampuni ya NSWE, ambayo inamilikiwa na bilionea Nassef Sawiris kutoka nchini Misri na Wes Edens kutoka Marekani.

Mataji

Aston Villa inatajwa kuwa moja kati ya klabu za England zenye historia kubwa ya mafanikio tangu kuanzishwa kwake.

Imekuwa miongoni mwa klabu tano ambazo zimewahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati huo linajulikana kwa jina la European Cup, wakichukua msimu wa 1981-82.

Wamewahi kuchukua taji la Kombe la FA mara saba, Kombe la Ligi mara tano pamoja na UEFA Super Cup mara moja.

Kupanda na kushuka

Mbali na kuwa miongoni mwa timu ambazo zilianzisha Ligi Kuu England, lakini imekuwa ikipanda na kushuka kutokana na ushindani mkubwa.

Mara ya kwanza ilishuka daraja mwaka 1936 na kwenda moja kwa moja Ligi Daraja la pili. Hii ni kutokana na matokeo mabaya ambayo waliwahi kuyapata msimu huo.

Katika michezo 42 ambayo walicheza waliruhusu kufungwa jumla ya mabao 110, jambo ambalo liliifanya timu hiyo kushuka.

Ilikaa miaka minne ikipigania nafasi ya kurudi kwenye Ligi daraja la kwanza ikaja kufanikiwa miaka minne baadae ambapo ilikuwa mwaka 1940, lakini misimu miwili baadae ikashuka tena daraja.

Mwaka 1967, mashabiki wa timu hiyo wakachoshwa na kitendo cha kushuka daraja mara kwa mara, hivyo wakawataka viongozi wa klabu hiyo kufanya maamuzi magumu ya kuachia ngazi hasa baada ya timu hiyo kumaliza nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi daraja la pili, hivyo walikubali kutokana na nguvu ya mashabiki.

Hata hivyo baada ya kuja uongozi mpya bado timu ilionekana kufanya vibaya zaidi na hatimaye ikashuka tena hadi daraja la tatu kwa mara ya kwanza msimu wa 1969-70.

Mwaka 1971 timu hiyo ikawa chini ya kiongozi Vic Crowe, ambaye aliwahi kuwa nahodha wa timu hiyo miaka ya nyuma, hivyo ikiwa chini yake iliweza kupanda daraja pili baada ya kuwa mabingwa wakiwa na pointi 70.

Mwaka 1974, Ron Saunders aliteuliwa kuwa kocha mkuu, hivyo timu hiyo ikafanikiwa kutwaa Kombe la Ligi na mwishoni mwa msimu wa 1974–75 ikaingia daraja la kwanza pamoja na kushiriki Europe. Hata hivyo kocha huyo aliweza kuwapa ubingwa msimu wa 1980-81

Kocha huyo aliendelea kuwaonesha maajabu mashabiki zake hasa msimu wa 1981-82 kwenye michuano ya Kombe la Uefa, ambapo wakati huo likijulikana kwa jina la European, lakini katikati ya msimu alitangaza kuachia ngazi wakati wapo hatua ya nusu fainali.

Nafasi yake ikachukuliwa na kocha msaidizi Tony Barton, ambaye aliifanya timu hiyo kutwaa ubingwa huo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bayern Munich, bao likifungwa na Peter Withe. Msimu uliofuata wakatwaa ubingwa wa UEFA Super Cup kwa kuwafunga Barcelona mabao 3-1.

Miaka 24 kwenye Ligi Kuu

Ikumbukwe kuwa Ligi Kuu England ilianzishwa mwaka 1992, ambapo msimu huo wa kwanza Manchester United wakatangazwa mabingwa huku Aston Villa wakishika nafasi ya pili na Norwich City wakishika nafasi ya tatu.

Mbali na kutwaa Kombe la UEFA, UEFA Super Cup na FA, hawajawahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England. Mwaka 2000 walifika fainali ya Kombe la FA lakini wakalipoteza dhidi ya Chelsea kwa kupokea kichapo cha bao 1-0.

Mabadiliko makubwa yalianza mwaka 2007, baada ya ujio wa kocha Martin O’Neill. Walikuwa na muonekano mpya wa jezi, wadhamini pamoja na mambo mengine mengi. Walifika nusu fainali kwenye Kombe la FA, lakini walikubali kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Chelsea ikiwa ni siku tano kabla ya kuanza kwa msimu wa 2010-11, hivyo O’Neill akatangaza kuachia ngazi.

Februari 2012, ilitangaza kuwa na ukata wa fedha, ikidai kupoteza pauni milioni 53.9, hivyo mmiliki akatangaza kuiuza kwa pauni milioni 200, lakini hakufanikiwa. Msimu wa 2014-2015, Aston Villa ilifanikiwa kupachika jumla ya mabao 12 kwenye michezo 25, ikawa ni mabao machache kuwahi kutokea kwenye historia ya Ligi hivyo kocha akafukuzwa na nafasi yake ikachukuliwa na Tim Sherwood.

Juni 2016, tajiri kutoka nchini China, Tony Xia aliinunua klabu hiyo kwa pauni milioni 76. Kocha wa zamani wa Chelsea, Roberto Di Matteo akatangazwa kuwa kocha mpya, lakini akafukuzwa kazi kutokana na mwenendo mbaya wa timu na nafasi yake ikachukuliwa na Steve Bruce. lakini Oktoba kocha huyo akafukuzwa baada ya kushinda mchezo mmoja kati ya tisa, hivyo nafasi yake ikachukuliwa na Dean Smith, John Terry na Richard O’Kelly wakiwa makocha wasaidizi ambapo walipambana hadi kupanda Ligi Kuu.

Lengo lao kubwa ni kubakia kwenye Ligi Kuu msimu ujao, hivyo wakaona bora wamsajili Samatta wakiamini atawasaidia kubaki kutokana na uwezo wake wa kupachika mabao, kila la heri Samatta, dua za Watanzania zipo pamoja nawe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles