27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

IGP SIRRO UNDA KIKOSI IMARA CHA UPELELEZI

NENO Jeshi kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili sanifu  toleo la tatu la mwaka 2013, ni askari wanaoajiriwa kulinda nchi na tafsiri ya pili ni wingi wa watu.

Ajabu katika maisha ya kawaida ya watu walio wengi  wakiwamo Watanzania, wakisikia neno  Jeshi  tafsiri  inayowajia haraka akilini mwao, ni chombo kinachotumia mabavu katika kulinda nchi.

Kama si sababu za kibaiolojia, basi kisaikolojia  inawezekana   tafsiri ya utumiaji mabavu katika Jeshi ni matokeo ya mfumo uliowakuza Watanzania  kabla, wakati na baada ya Uhuru kwamba askari ni kifaa cha kuogopwa.

Mei 28, mwaka huu Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli alimteua aliyekuwa Kamanda wa  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP)

Hakika uteuzi huu ulioendana na kumtengua aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi hapo awali, Ernest Mangu ambaye muda wake ulikuwa haujaisha,  uliibua maswali mengi kuliko majibu.

Hata hivyo kitendawili cha utenguzi kimeteguliwa Juni 2, mwaka huu baada ya Rais kukutana na makamanda wote wa Polisi kutoka Tanzania Bara na visiwani jijini Dar es Salaam.

Katika tukio hilo Rais amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi  (IGP), Sirro kujipanga vizuri yeye na safu yake ya makamanda, viongozi wakuu wa vikosi na maofisa mbalimbali ili kuondoa dosari zote za utendaji kazi zinazoshusha ufanisi na heshima ya Jeshi la Polisi.
 

“Ni lazima ufanye mabadiliko makubwa, nataka kuona Jeshi la Polisi linakuwa Jeshi la Polisi, wewe IGP Sirro na makamnda wenzako hakikisheni mnakomesha uhalifu, komesheni mauaji dhidi ya raia, ujambazi na dawa za kulevya,” Rais alisisitiza.

Mbali na hilo, pia Rais  amewataka makamanda, maofisa na askari wa Jeshi hilo kujiepusha na rushwa, dawa za kulevya, kutumiwa  na  watu kwa maslahi binafsi, kuingia mikataba isiyo na masilahi kwa Jeshi na Taifa, ubadhirifu na kuacha upendeleo katika utoaji wa ajira na vyeo.

Ni dhahiri haya yaliyotamkwa Rais hata kama kuna sababu nyingine lakini ndicho kiini cha kumteua Simon Sirro kuwa IGP. Hata hivyo ili  Jeshi la Polisi  liweze kukabiliana na vitendo  vya uhalifu mkubwa, kitengo chake cha Upelelezi hakina budi kufanyiwa marekebisho makubwa.

Ni wazi kitengo hiki pamoja na  mazuri yake,  bado kinapwaya katika  utendaji  wake unaoweza kuwa unasababishwa na mfumo wa mafunzo kama si udhaifu binafsi wa kibinadamu.

Ni aibu, fedheha na usaliti kwa afisa  upelelezi kujinadi ovyo ovyo mbele ya raia  ili ajulikane yeye ni nani wakati angejichanganya kimya kimya angeweza kupata taarifa mbalimbali zikiwamo za uhalifu.

Ukiwa mitaani utaona  watu wakiwanyoshea vidole wapelelezi  kuwa  huyo ni CID, mara  afisa upelelezi. Kujulikana kwa namna hii kama si kukaa muda mrefu kituo  kimoja basi  ni huku kujitweza ili kupata  misifa.

Naamini umaarufu hutafutwa na mwanasiasa ili kuwapata wafuasi wengi watakaompa ulaji, lakini  umaarufu hauwezi  kumsaidia mpelelezi  kuwabaini wahalifu.

Wakati umefika IGP Sirro kuunda kikosi  cha Upelelezi chenye mafunzo na uadilifu mkubwa  kama wa  FBI au CIA,  kwani ubora wa Jeshi  si wingi wa silaha  au nguvu ya misuli ya askari kama raia baadhi wanavyoamini,  bali ni mbinu na mikakati chanya  inayoweza  kutambua uhalifu na kuuzuia kabla haujaleta madhara katika jamii ikiwamo kuuawa askari kwa kushtukiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles