27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

IGP Sirro: Hakuna aliye salama

ELIYA MBONEA-ARUSHA

TAARIFA za kiintelijensia zinaonyesha kuwa bado kuna matishio ya kiusalama, makundi ya kigaidi yanaendelea kujiimarisha, kufungua vituo maeneo mbalimbali ndani ya nchi na ukanda wa Mashariki mwa Afrika.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro alipofungua vikao vya Kamati Tendaji na Wakuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ikiwa ni maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi Mashariki mwa Afrika (EAPCCO).

Akizungumza na wajumbe wa mkutano huo Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), IGP Sirro alisema matukio ya kigaidi yanayotokea maeneo mbalimbali duniani ni kiashiria tosha kwamba nchi wanachama pia haziko salama.

“Katika jambo hili hakuna nchi iliyo salama, kwa mantiki hiyo lazima tuweke msingi madhubuti wa kujenga uwezo wa kubaini, kuzuia, kupambana na kutanzua uhalifu kwa lengo la kujiepusha na matumizi ya nguvu nyingi baada ya tukio kutokea.

“Kwa kufanya hivyo mtapunguza madhara ya majeruhi, vifo na uhalifu wa mali. Tukumbuke usemi usemao kinga ni bora kuliko tiba,” alisema.

Katika hotuba yake IGP Sirro aliwataka wajumbe kubuni mkakati wa utendaji unaozingatia utatuzi wa changamoto za uhalifu kimitandao, unaotokana na mabadiliko ya kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano.

Alisema ni vyema kufanyike maboresho ya namna ya kufanya operesheni, kukusanya na kuchakata taarifa za kiintelijensia, uratibu wa kubadilishana taarifa, tathmini ya pamoja na nini cha kufanya.

“Msisitie kutupia jicho au kujadili mianya, mapungufu yaliyopo katika sheria zetu ili hatimaye mje na mapendekezo ya jinsi ya kuzirekebisha.

“Niwashukuru Interpol wamekuwa wakiratibu operesheni za kuzuia makosa yanayovuka mipaka na nchi zetu nyingi zimekuwa zikishiriki.

 “Operesheni hizi hasa za kuwatafuta wahalifu wanaovuka mipaka zitakuwa na mafanikio zaidi endapo tutaweka mifumo ya 1-24/7 katika mipaka yetu na kuzisimamia kwa karibu,” alisema IGP Sirro.

Pamoja na hayo, aliwaambia wajumbe hao kuwa Jeshi la Polisi Tanzania linalotarajiwa kuwa Mwenyekiti wa EAPCCO, litaendeleza ushirikiano na nchi wanachama katika kuhakikisha eneo la Mashariki mwa Afrika linakuwa mahali salama pa kuishi.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz alisema mkutano huo unafanyika katika kipindi ambacho ukanda huo unakabiliwa na changamoto kadhaa.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni magenge ya uhalifu, matatizo ya kuzagaa silaha miongoni mwa jamii, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya, ujangili, usafirishaji haramu wa binadamu, wizi wa magari, vitendo vya ugaidi na mafunzo ya kihafidhina.

DCI Boaz alisema kuwa kwa siku mbili wajumbe wanatarajiwa kujadili masuala muhimu yakiwamo uhalifu unaovuka mipaka ambapo maazimio yake yatakuwa sehemu ya agenda katika mkutano mkuu wa 21.

Kikao hicho kinaongozwa na kaulimbiu ya ‘Kuimarisha ushirikiano na ubunifu katika mapambano dhidi ya uhalifu unaovuka mipaka na nje ya Mashariki mwa Afrika’.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Uratibu ya EAPCCO na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Sudan (DIC) anayemaliza muda wake, Meja Jenerali Khalid Mahdi, alisema lazima wafanye kazi kwa pamoja ili kuwa na usalama wa uhakika.

“Kupitia EAPCCO, Polisi ya Sudan imeweza kuanzisha mbinu zilizosaidia kupambana na matukio ya uhalifu, ikiwamo ugaidi. Ninaishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kuandaa mkutano huu,” alisema Meja Jenerali Mahdi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles