27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Hulka kusikiliza maoni ya watu huanzia kwenye familia

Na MWANDISHI WETU

WATAWALA wengi barani Afrika wanapopata madaraka huziba masikio yao na kutosikiliza kero za wananchi wao na kuhakikisha vivywa vyao haviwezi kusema kinyume na maoni waliyonayo. 

Kutosikilizwa kwao wananchi katika kuamua aina ya utaratibu utakaotumika kujitawala kunawafanya wajisikie kuminywa na hata kunyang’anywa haki muhimu ya raia kujieleza. 

Hata hivyo, ni dhahiri kuwa viongozi mbalimbali hutokana na jamii inayowachagua kuwasaidia kufikia malengo yao. Haiba, hulka na mienendo ya watawala haiwezi kuwa tofauti na hali halisi ya wananchi wao.  Wanayoyafanya–kwa kujua au kutokujua– ni sura halisi ya utamaduni wa wananchi. 

Tutumie mfano. Wananchi wanaothamini elimu, hutafuta na kuchagua miongoni mwao viongozi wanaothamini elimu. Kinyume chake, wananchi wasiothamini elimu huweza, na kwa kweli hufurahia, kuchagua ‘wajinga’ wenzao kuwa viongozi wao. 

Vivyo hivyo, wananchi wanaopenda njia za mkato kujipatia kipato, huthamini na kuwachagua wagombea ‘wajanja wajanga’ ambao baadae huja kufahamika kama mafisadi. Haiwezekani viongozi kuwa tofauti na wananchi.

Tukizitazama nchi zinazosifika kwa demokrasia tunabaini kuwa ni utamaduni wa wananchi. Demokrasia ni maisha yanayoanzia kwenye utawala wa familia. Kila mwanafamilia anajengewa mazingira ya kujisikia kuwa na uhuru wa kuchangia maoni yake. 

Mtoto hupewa nafasi ya kufanya uamuzi kwa mwongozo wa mzazi. Mke naye anakuwa na fursa ya kushiriki katika maamuzi anayoyafanya mumewe kwa sababu demokrasia katika jamii hizo ni utamaduni unaoanzia kwenye familia na si matamanio bandia ya kisiasa.

Ninapotafakari madai ya raia katika nchi za Kiafrika, kutaka watawala wawe wanademokrasia, maswali kadhaa yanajitokeza. Ninajiuliza, kwa mfano, inawezekana kweli kudai kuwa jamii Fulani ni inayoamini katika demokrasia kuanzia ngazi ya familia? Je, demokrasia ni utamaduni wao? 

Wanaume wa Kiafrika, mathalani hawatishwi na kukua kwa demokrasia kwenye ngazi ya familia? Wanawashirikisha kweli wake zao katika uamuzi bila kuwawekea mipaka? Wanaheshimu maoni ya watoto wao kama wanavyotaka watawala wao waheshimu maoni yao? 



Kwamba, wanahitaji demokrasia kwenye vyama  vya siasa na serikalini, hili halina mjadala. 

 Je, madikteta wa familia (wasiowapa wake/waume/watoto wao uhuru wa maoni kwa kuogopa kukosa mamlaka yao wakiwa wazazi/wanaume, wanaweza kuwa na uhalali kwa kudai hawapendezwi na tabia za viongozi wa nchi za Afrika wanaoonesha hulka na tabia za kidikteta?

Yapo mapendekezo mawili. Kwanza, ili kujenga taifa linaloamini uhuru wa mawazo kweli kweli, ni vema kuanza kuanza kujenga demokrasia ya kweli ndani ya familia. Kuanza kuzishirikisha familia  katika uamuzi bila hofu ya kupokonywa madaraka. Kuanza kuthamini na kuheshimu maoni/mahitaji ya watoto  na kuyasikiliza. Kujenga taifa la kweli la watu wanaoamini demokrasia.

Mawasiliano 0754870815, Twitter: @bwaya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles