27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Hujuma yatajwa kuzama Mv Nyerere

Na FREDRICK KATULANDA NA PETER FABIAN-UKARA

BAADHI ya wazamiaji wanaoshughulika na uakoaji wa kivuko cha Mv Nyerere kilichozama Septemba 20 wakati kikitoka eneo cha Bugorola kisiwani Ukerewe kwenda Ukara, wamedai kuona dalili za  hujuma zilizofanywa na baadhi ya watendaji.

Zaidi ya watu 227 walikufa katika kivuko hicho kilichozama kikiwa kimebakiza takribani mita 100 kufika mwisho wa safari yake kisiwani Ukara.

Hivi sasa wataalamu wa uzamiaji, uokoaji na vyombo vya majini wanaendelea na kazi ya kukiibua kwenye maji  kabla ya kuvutwa hadi nchi kavu.

Wakizungumzia vitu walivyoviona wakati wakiendelea na hatua ya kunyanyua kivuko hicho jana, baadhi ya wazamiaji hao walisema wamebaini kuwa matanki ya uwiano (Balance tanks) yalikuwa hayajajazwa maji kama inavyotakiwa.

Walisema sababu za kutojazwa  maji matanki hayo ni pamoja na kubana mafuta yanayotumika kwenye kivuko na kutumia matanki hayo kubebea mizigo kuliko uwezo wa kivuko.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, mmoja wa watumishi wa kivuko hicho, alidai kivuko hicho kilikosa uwiano majini kutokana na kuondolewa maji katika matanki yake mawili lengo likiwa ni kubeba mizigo mingi zaidi na kubana kiwango cha mafuta kinachotumika.

Alidai katika vivuko vyote vya Serikali ambavyo vimekuwa vikisimamiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), baadhi ya watendaji wamekuwa wakiiba mafuta na mapato kwa kuuza tiketi mara mbili.

Mtaalamu mwingine   kwenye eneo hilo kwa shughuli za uopoaji, alisema kwa mazingira aliyoona amebaini uwezekano wa kivuko hicho kutokuwa na maji kwenye matanki hayo ambayo kazi yake ni  kukisaidia kuwa na uwiano.

“Kawaida meli au kivuko hupata ‘balance’ (uwiano wa kuelea) kutokana na matanki ya maji (Balance tanks), chombo kikiwa na maji kwenye matanki hayo siyo rahisi kupinduka labda kuzama (sink), hivyo ikitokea kikapinduka kama MV. Bukoba au MV. Nyerere lazima tatizo litaanzia kwenye uwiano,” alisema.

Mtalaamu mwingine alisema: “Kawaida huwa kuna kipimo cha kupunguza mwendo kwenye meli au kivuko kinapokaribia kufika bandarini au kwenye gati.

“Sasa ninachokiona kanuni hii haikuzingatiwa, nahodha atakuwa alijisahau. Ukiweka kosa la kubeba mzigo na hili la kutozingatia kanuni ya kupunguza mwendo, vilisababisha ajali,” alieleza.

Alisema kwa mtazamo wake kupinduka  kwa kivuko hicho kunaweza kuwa kulitokana na sababu mbili  ya kwanza ikiwa  ni kuwa na maji kidogo ama kutokuwa nayo  kwenye matanki ya uwiano na ya pili ni kubeba mzigo mkubwa kuliko uwezo wake.

Nao baadhi ya wafanyakazi wa Temesa walisema tatizo la kupunguza maji kwenye matanki kwa kivuko cha Nyerere lilikuwa likitokana na kubana   mafuta ili yatumike kidogo.

“Unajua wakati mwinginge bajeti ya mafuta hutoka ndogo, sasa ili wafanyakazi nao wapate fedha wamekuwa wakipunguza maji kwenye balance tanks.

“Pia wapo watu wasio waaminifu ambao wamekuwa wakifanya hivi kwa ajili ya kuuza mafuta na kupata fedha, hata hilo suala la watu kuzidi uwezo ilikuwa ni njia ya kujipatia fedha,” alieleza mmoja wa wafanyakazi hao.

Wakati huohuo, mtu mmoja kati ya wanne waliozikwa Septemba 23 bila kutambulika, ametambuliwa baada ya ndugu zake kujitokeza na vipimo vyao vya vinasaba kufanana.

Mwili uliotambuliwa ulitajwa kuwa ni wa Muleba Mavere ambaye awali alizikwa kwa utanbulisho wa namba 10 K.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kukabidhi kaburi la marehemu kwa ndugu zake kwa ajili ya ibada na taratibu za familia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu), Jenister Mhagama, alisema vipimo vya utaalamu vilithibitisha bila shaka kuwa vinasaba vya marehemu vililingana na mmoja wa watoto wake wa kike.

“Tumefanya vikao na familia hadi jana usiku ambako baada ya kuridhika na maelezo yao, wataalamu walikamilisha kwa kufanya vipimo ambavyo vimetupatia uhakika,” alisema Mhagama.

Kutambuliwa kwa marehemu Muleba kunafanya waliozikwa bila kutambulika kubakia watatu.

Miongoni mwa ndugu wa marehemu waliojitokeza ni pamoja na mume wake, Matindi Mavere mkazi wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera na watoto wake wawili.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, ambaye yuko Ukara kusaidiana na mwenzake John Mongella wa Mwanza kuratibu kazi ya uokoaji, aliwataka watu wenye uhakika kuwa ndugu zao walikuwa ndani ya kivuko cha Mv Nyerere lakini hawajaonekana, wajitokeze.

“Hatutafanya makosa katika utambuzi; tutawahitaji na kijiridhisha na kukamilisha utambuzi kwa vipimo ya DNA,” alisema Malima.

Katika hatua nyingine, watu mbalimbali wameendelea kutoa misaada kwa ajili ya kuwafariji wafiwa, ambako Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki (TEC) limetoa  Sh milioni 25.

Akipokea fedha hizo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Issack Kamwelwe, alisema fedha hizo zitatumika kama ilivyopangwa na kuwataka wananchi mbalimbali kuendelea kujitolea.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. hakika inahuzunisha sana kupotelewa na ndugu zetu, huu ni msiba mzito katika nchi yetu. Mwenyezi Mungu wa rehema wape uvumilivu wafiwa wote pia natoa pole sana kwa Rais wetu Joseph Pombe Magufuli. RIP wapendwa wetu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles