27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

PROFESA MAGHEMBE ASEMA AACHWE APUMZIKE

NA GABRIEL MUSHI

ALIYEKUWA Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amesema kwa sasa anapumzika baada ya kazi ngumu ya kuiongoza wizara hiyo.

Maghembe ambaye uteuzi wake na ule wa Naibu wake, Ramo Makani, ulitenguliwa wiki iliyopita na Rais Dk. John Maguli, pia alisema hana jambo la kumshauri Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangala, kwa kuwa si muda mwafaka wa kuanza kuichambua wizara hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu Alhamisi wiki hii, Maghembe aliyeiongoza wizara hiyo kwa vipindi viwili tofauti kuanzia mwaka 2007 hadi 2008 wakati wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na mwaka 2015 hadi mwaka huu, alisema licha ya changamoto alizozikuta wizarani hapo lakini ameiwezesha sekta ya utalii hapa nchini kukua kwa kasi.

“Sina comment, si wakati wangu sasa, niacheni nipumzike kwanza, lakini niwaambie kila kitu kinajieleza kwa sababu tumeona Tanzania ilivyopanda katika viwango vya utalii duniani na Afrika kwa ujumla, Watanzania wanaweza kutambua mchango wangu kwa kutathmini ukuaji wa sekta ya utalii hapa nchini,” alisema.

Kauli ya Maghembe ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Waziri wa Maji wakati wa uongozi wa Kikwete, imekuja baada ya wiki hii Mlima Kilimanjaro kushinda tuzo kubwa Afrika kwa kuwa Kivutio Bora cha Utalii Afrika kwa mwaka huu inayotolewa kila mwaka na Taasisi ya World Travel.

Pia katika kipindi cha uongozi wa Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga, idadi ya watu maarufu kutoka nje ya nchi walikuja hapa nchini kutazama vivutio vya utalii huku mtandao wa kimataifa wa kibiashara wa SafariBookings.com ukiitangaza Tanzania kuwa ni nchi ya kwanza Afrika inayowavutia zaidi watalii.

Hata hivyo, Maghembe aliwahi kutajwa kuwa ni mmoja wa mawaziri mizigo katika utawala wa Kikwete kutokana na hoja zilizoibuka katika mikutano ya hadhara iliyofanywa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho, Nape Nnauye.

Pia mjadala wa Faru John ulioibuliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokuwa katika ziara ya kikazi Ngorongoro, ulionekana kumtikisa Maghembe.

Alipozungumza Desemba 6, mwaka jana na wafanyakazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Majaliwa alisema ndani ya mamlaka hiyo kuna vitendo vya rushwa na Faru John alihamishwa na kupelekwa Grumeti, Serengeti mkoani Mara baada ya baadhi ya wafanyakazi kupewa Sh milioni 100 na kuahidiwa Sh milioni 100 nyingine zilizokuwa hazijatoka.

Hata hivyo, Desemba 9, mwaka jana, Maghembe alikabidhi taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha Faru John kutoka Ngorongoro kwenda Grumeti na Majaliwa aliahidi kuwa itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles