24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Hotuba ya Rais bungeni tumbo joto kwa mawaziri

ISIJI DOMINIC

IBARA ya 132 ya Katiba ya Kenya inamtaka Rais kuhutubia Bunge mara moja kwa mwaka ambapo atatakiwa kutoa ripoti ya hatua iliyochukuliwa na Serikali yake kuhusu masuala yanayohusu nchi na mafanikio aliyopata.

Hivyo basi, Alhamisi iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta alitoa hotuba yake katika kikao cha pamoja ya Bunge la Taifa na Seneti iliyodumu kwa takribani saa moja. Kama kawaida, wanasiasa, wafanyabiashara na wananchi walipokea hotuba hiyo kwa hisia tofauti. Wapo wale waliompongeza na wapo wale waliosema Rais hajagusa maeneo muhimu.

Mfano, Rais Uhuru hakuzungumzia kuhusu baa la njaa linaloikabili baadhi ya maeneo nchini Kenya japo Naibu Rais William Ruto na Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa, walikaririwa wakisema hakuna mwananchi hata mmoja aliyefariki kutokana na njaa na kusisitiza Serikali imeshasambaza chakula katika maeneo yanayokumbwa na ukame.

Hotuba ya Rais ilifafanua kwa uzito masuala yanayohusu vita dhidi ya ufisadi, ajenda nne kuu na umuhimu wa viongozi kufanya kazi pamoja kwa ajili ya umoja wa taifa na maendeleo.  Ajenda nne kuu ambayo ni matibabu kwa wote, makazi bora, usalama wa chakula na viwanda ni sehemu kubwa ya kumbukumbu anayotaka kuiacha Rais Uhuru pindi muhula wake wa pili ya uongozi ukifika tamati mwaka 2022.

Ili kufanikisha ajenda nne kuu, Rais Uhuru anatakiwa kupambana na ufisadi unaoonekana kupaka matope Serikali yake ndiyo kwa maana alipohutubia Bunge alisisitiza ataendeleza mapambano hayo yanayokusudiwa kulinda rasilimali ya nchi.

“Hatutarudi nyuma vita dhidi ya ufisadi kwa sababu hii ni vita ya kuzuia matumizi mabaya ya rasilimali ya umma yanayotumika vibaya na baadhi ya watu waliokabidhiwa dhamana ya kuvitumia vizuri kwa manufaa yao binafsi,” alisema.

Aidha Rais alisema malengo yaliyowekwa katika makubaliano yake ya Machi 9, mwaka jana na kinara wa upinzani, Raila Odinga  ambaye ni Kiongozi wa Chama cha ODM yataendelea kupewa msukumo na hakuna kitu kitakachowapunguzia kasi.

Rais Uhuru alijua fika Wakenya wanataka kumuona akiwatimua kazi mawaziri ambao wametajwa katika kashfa za ufisadi lakini amesisitiza hataingia katika mkumbo wa kuchukua maamuzi kwa shinikizo na badala yake kuacha mamlaka husika kufanya kazi yake.

Kwa siku za hivi karibuni, Ofisi za Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) zimekuwa zikifanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) wakiwahoji mawaziri na magavana wanaotuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Licha ya kuepuka shinikizo ya kuwatimua mawaziri wanaotuhumiwa kwa ufisadi, Rais Uhuru alisema pindi mawaziri hao au maofisa wowote wa Serikali wakipandishwa kizimbani hawana budi kuacha kazi.

Baadhi ya mawaziri ambao huenda wakalazimika kukaa pembeni endapo watafikishwa mahakamani ni Henry Rotich (Fedha), Wamalwa (Ugatuzi) na Mwangi Kiunjuri (Kilimo) ambao waliitwa ofisi ya DCI kuhojiwa kuhusu kashfa ya mradi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror yaliyopo Kaunti ya Marakwet Magharibi.

Rais Uhuru alisema yeye ni muumini wa sheria na anatumia Katiba kuongoza nchi hivyo anawapa nafasi watuhumiwa kujitetea mbele ya mamlaka za Serikali zinazowahoji huku akiitaka idara ya mahakama kuepuka kutoa dhamana ndogo.

Katika mapambano dhidi ya ufisadi, kiongozi wa Amani National Congress, Musalia Mudavadi, anamshauri Rais awe mkali kidogo kwa kuwaondoa ofisini watuhumiwa ili mamlaka zinazochunguza kufanya kazi zao kwa uhuru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles