31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali zatakiwa kubuni njia za kupata vifaa tiba vya kisasa

Julieth Peter, Mbulu

HOSPITALI nchini zimetakiwa kubuni mbinu mbadala za kujiendesha ili kutoa huduma bora za kiafya badala ya kusubiri msaada kutoka serikalini.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga, katika shehere za miaka 64 ya Hospitali ya Rufaa ya Kilutheri ya Haydom iliyoanzishwa na Wamisionari wa Norway mwaka 1955.

Sherehe hizo zilienda sambamba na uzinduzi wa mashine ya mpya ya CT Scan, Digital X-Ray, mashine ya kuchoma taka hatarishi na ya Oxygen.

Alisema ni vyema viongozi wa hospitali nchini kubuni mbinu ya kuongeza vifaa tiba katika hospitali zao badala ya kusubiri mpaka Serikali kuu iwaletee.

“Hospitali ya Haydom inafanya vizuri kiasi kwamba inaitangaza Wilaya ya Mbulu, madaktari wapo safi sana sio tu weledi wa matibabu lakini pia utafikiri wote wamepita jeshi, tulipata ajali ya gari kutumbukia korongoni walitupa ushirikiano ndani ya nusu saa majeruhi  wote wakawa wamepatiwa matibabu” alisema Mofuga.

Alisema kwa sasa Serikali kwa kushirikiana na hospitali hiyo wanafanya juhudi za kuipandisha hadhi ili iwe hospitali ya rufaa ya Kanda kwa kuwa moja ya vigezo ambavyo vilikuwa vinasubiriwa  ni kuwa na vifaa tiba vya kisasa na hiyo tayari wameshaijibu hivyo watahakikisha hilo linafanikiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tiba Hospitali hiyo, Dk. Emmanuel Nuwass, alisema  hospitali  hiyo itaendelea kutoa huduma za afya kwa kuzingatia sera na miongozo ya wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine ili kuimarisha vita dhidi ya maradhi na umaskini.

Alisema  wanamshukuru Rais John Magufuli, kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya nchini.

Alisema katika kuboresha huduma za afya katika hospitali yao walishirikiana na wadau wa ndani na nje kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kununua vifaa tiba vipya.

Alisema katika njia walizotumia kukusanya fedha hizo ni pamoja na mbio za hisani ‘Haydom Marathon’ mwaka 2018 ambapo walikusanya Sh milioni 107.

Mbali na mbio hizo alisema walishirikisha wadau wao wakuu NORAD na NCA ambao waliwachangia Sh bilioni 1.1 wakati FoH wakichangia Sh milioni 285.

Alisema kupitia fedha kutoka serikalini, KKKT Dayosisi ya Mbulu, watumishi wa hospitali na wadau wengine, waliweza kupata Sh milioni 185 ambapo jumla walikusanya Sh bilioni 1.5.

Kwa upande wa vifaa walivyonunua alisema CT Scan iligharimu Sh milioni 654.2 na imeshawahudumia zaidi ya wagonjwa 250, Digital X-Ray Sh  milioni 320.2, mtambo wa kuzalisha a Oxsijeni kwa ajili ya wagonjwa Sh milioni 372.9 ambayo ina uwezo wa kuzalisha mitungi yenye mita za ujazo 8.5 kuanzia 40 hadi 56 kwa siku.

Mashine ya kuteketeza taka hatarishi zinazozalishwa hospitalini yenye uwezo wa kuchoma taka kilo 100 kwa saa katika nyuzi joto 1,200 ambayo imegarimu Sh milioni 203.

Mwakilishi wa balozi wa Norway nchini, Britt Hilde Kjolas, alisema anafurahi kuona Watanzania wanaongoza hospitali ya Haydom kuwa na weledi na kufanya mambo makubwa ambayo kwake.

Alisema ni jambo jema kuona vifaa vipya vimenunuliwa ambavyo vitaenda kuwasaidia wagonjwa ambao wengi wao ni wa vijijini na wenye kipato cha chini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles