27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali Benjamin Mkapa kuvunja mawe mfumo wa mkojo bila upasuaji

MWANDISHI WETU – DODOMA                         

HOSPITALI ya Benjamin Mkapa ya Dodoma imezindua huduma ya kwanza ya kisasa ya kuvunja mawe kwenye mfumo wa mkojo bila kufanya upasuaji.

Huduma hiyo imezinduliwa baada ya kuwasili kwa mtambo wa kisasa unaotumia mionzi katika kufanya huduma hiyo tofauti na awali ambapo wagonjwa walikuwa wakifanyiwa upasuaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk. Alphonce Chandika, alisema kuwa huduma hiyo itafanyika kwa mara ya kwanza nchini na inawezekana ikawa ni mara ya kwanza pia kwa nchi za Afrika Mashariki.

Dk. Chandika alisema mtambo huo umekuja sehemu sahihi kwa sababu Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma na Singida imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya wagonjwa wengi wenye matatizo ya mfumo wa mkojo.

“Tunashukuru sana Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, hakika tumejionea kwa vitendo utekelezaji wa ahadi zake, hasa katika sekta ya afya.

“Mtambo huu unaenda kuwa mwarobaini wa tatizo la mfumo wa mkojo kwa wananchi wetu wengi.

“Kanda ya Kati imekuwa na idadi kubwa ya watu wenye changamoto hii. Kwa wiki tumekuwa tukipokea wagonjwa watatu hadi wanne wenye shida ya mfumo wa mkojo hasa mawe kwenye figo, hivyo kuwasili kwa mtambo huu tuna uhakika kabisa unakwenda kuwa msaada kwetu na kwa wagonjwa,” alisema Dk. Chandika.

Aidha alisema Hospitali ya Benjamin Mkapa pia imechukua tahadhari ya kupambana na maambuziki ya virusi vya corona kwa kuweka utaratibu wa kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na yenye ‘sanitizer’ kwa kila mtu anayeingia na kutoka hospitalini hapo.

“Katika kuchukua tahadhari pia tumetoa tangazo kwa wagonjwa na wananchi wetu kuwa idadi ya ndugu watakaokuja kuwaona wagonjwa haitozidi wawili ili kuepuka msongamano usio wa lazima, lakini pia tumeweka sanitizer na maji kwa ajili ya kujikinga na maambukizi,” alisema Dk. Chandika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles