31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Hongera Magufuli kwa matumizi ya fedha za ndani kwa Maendeleo

Judith Mhina -Maelezo

RAIS wa Kwanza wa Tanganyika na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Baba wa Taifa, aliyetuletea Uhuru, anatimiza miaka 20 tangu alipoiaga dunia Oktoba 14,  mwaka 1999.

Mara baada ya Uhuru Mwalimu Nyerere aliwaandaa Watanzania wakati ule Watanganyika kisaikolojia kuwa ni lazima wajitegemee. Kwa kuwa aliona viashiria vya utegemezi, ambapo wananchi walio wengi wakidhani Uhuru maana yake ni kubweteka na kuletewa vitu vya bure bila kufanya kazi.

Kama hiyo haitoshi Mwalimu akaja rasmi na Azimio la Arusha Februari 5,  1967 baada ya kuona viashiria vya ubwanyenye, unyonyaji, rushwa na upendeleo kwa baadhi ya viongozi. Moja ya mikakati yake katika Azimio hili ni kufanya kazi  kwa bidii  ndipo alipozindua  Elimu ya Kujitegema Shuleni.

Wakati wa uzinduzi huo Mwalimu Nyerere alisema maneno haya; “Tumieni kikamilifu uwezo wetu wa ndani kujitegemea, tumieni watu wetu na ushirikiano katika ngazi mbalimbali fanyeni hivyo na muone utegemezi kuwa ni adui wa nchi”. Tujenge nchi yetu tutumie uwezo wetu wa ndani kwa ajili ya maendeleo yetu.

Kitendo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuamua kuja na sera za kujitegemea na kukataa utegemezi kwa kiasi kikubwa kiliwachefua mabeberu, ambao walitumia silaha ya misaada katika suala zima la kulazimisha nchi kufuata masharti na itikadi wanazizitaka wao.

Tuna haki ya kumwambia Mwalimu Nyerere maneno haya kuwa leo hii Tanzania inatembea kifua mbele kwa kufanya mambo mengi ya maendeleo kwa kutumia fedha zake za ndani. Msingi na muongozo wa kutumia fedha hizo za ndani umeuweka wewe Mwalimu Nyerere.

Rais Dk. John Magufuli sasa ni kielelezoi cha matamshi yako uliyoyasema wakati unazindua Elimu ya Kujitegemea mara baada ya kutangaza Azimio la Arusha.

Nanukuu maneno yako Mwalimu “Tumieni kikamilifu uwezo wetu wa ndani kujitegemea, tumieni watu wetu na ushirikiano katika ngazi mbalimbali fanyeni hivyo na muone utegemezi kuwa ni adui wa nchi”.

Akihutubia Mkutano wa hadhara pale Mkoa wa Katavi Rais Magufuli amesema Mtaji wa Msikini ni nguvu zake mwenyewe. Tunajitegemea kwa fedha zetu. Mradi wa Barabara wa Kaliuwa – Mpandafedha zetu, SGR, (reli ya kisasa),  fedha zetu, vituo vya afya na hospitali fedha zetu. Tembeeni kifua mbele.

“Fedha za elimu bure darasa la kwanza hadi kidato cha nne, Sh bilioni 23.6 kila mwezi fedha zetu, Hhta Ulaya hawawezi hili,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa mabeberu hawaoni raha kuiona Tanzania ikitekeleza miradi yake kwa fedha zake  ndio maana wanaizushia mabaya yakiwemo magonjwa hatari. 

Amesisitiza kwa kusema Mabeberu hawaoni raha kutuona tunafanya mambo makubwa ka fedha fedha zetu wenyewe . Ndio maana wanafanya mbinu zao wanadai kuna ugonjwa. Wapuuzeni!!!!!.

Utabiri na uhalisia wa maono na uwezo wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere umetimia. Hakika Tanzania inajitegemea kwa kutumia fedha zetu za ndani . Mwalimu tumeona utegemezi ni adui wa nchi.

Yapo mambo mengi sana mbayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alilazimishwa kuyafuata na hao mabeberu, mfano kuchaguliwa marafiki na kutakiwa kufata mrengo wa kushoto au kulia ili kupata misaada. Lakini Mwalimu alishinda vita hiyo kwa sababu wa msimamo wake na hoja alizokuwa anawasilisha mezani wakati akiongea na mabeberu hao na hakika walisalimu amri kwa Mwalimu.

Sio mara moja au mbili  kwa Mwalimu kufanyiwa hila na mabeberu hao Aidha, kwa kutumia Watanzania wenye fikira za kujineemesha wao wenyewe na familia zao kwa kudiriki kuwa wasaliti wa nchi yao. Hivyo Rais Magufuli hilo la hila limeanza kwa Mwalimu Nyerere usistajabu kutokea sasa.

Pia, Mwalimu Nyerere alipolazimishwa kufuata mpango wa Benki ya Dunia baada ya kutumia hila nyingi  ikiwemo vibaraka wao na mabeberu  kutumiwa kuvunja Jumuiya ya Afrika Mashariki, kumshabikia Rais wa Uganda Idi Amin Dadah kuichokoza Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa kukaa kimya bila kumkemea  ili kukuza mgogoro na Tanzania kusababisha vita.

Hali hiyo ilidhoofisha uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa ambapo Mabeberu wakafurahia hali hiyo wakidhani Mwalimu atasalim amri kwao. Kwa kuwa hali ya uchumi ilikuwa ngumu, Wahujumu uchumi wakapata kiburi cha kuficha mali  kuendlea kumdhoofisha uchumi wa nchi.

Serikali ya Awamu ya Tano ipokee  ushuzi wowote wanaouanzisha, kusema wazi na kuwaambia mabeberu hao kuwa tunajua njama zao  na kuelezea Jumuiya ya Kimataifa kuwa hizo ni njama. Hiyo, ndio silaha pekee ambayo Tanzania iendelee kuitumia kama alivyofanya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Mwalimu Nyerere ataendelea kukumbukwa na Watanzania katika maisha yao yote  kwa kuwa mambo aliyowafanyia ni ya kipekee ambayo hayawezi kufanywa na kiongozi yeyote yule ajaye. Tunasema hivyo kwa sababu kuna mambo yanafanyika mara moja katika historia ya nchi hayawezi kurejelewa tena . Mfano yeye ndiye aliyetuletea Uhuru tarehe 09 Desemba mwaka 1961, hivyo hakuna awezaye kutulletea tena Uhuru itabaki kuwa hivyo milele katika taifa hili.

Lakini Tukatae, tukubali  penye ukweli uongo hujitenga Uongozi wa Awamu ya Tano unavaa  ipasavyo viatu vya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kadiri siku zinavyosonga mbele ndivyo anavyozidi kumuenzi, wewe usiyekubali sio rahisi kuwashawishi watanzania wote wakubaliane na wewe kwa kuwa wanaona, wanasikia  na vitendo vinaonekana kwa macho.

Kwa kuwa Mwalimu Nyerere alitumia Elimu Bure kuwafunza na kuwaandaa Watumishi Mashujaa wa kuja kuitumikia Tanzania. Ni wajibu  wa  uongozi kuona alichokifanya  Baba wa Taifa kinaendelezwa ili kuzalisha Watumishi wengi watakaoitumikia nchi kwa moyo wao wote.

Mwalimu Baba wa Taifa la Tanzania hakika kazi uliyoifanya hapa Tanzania ni ya kutukuka ikiwemo ya kuwaandaa vijana wako ambao sasa wapo madarakani. Uliwafunza wakaelimika, na sasa wanatenda kwa vitendo na Tanzania inang’ara Mashasriki, Magharibi Kaskazini na Kusini mwa Dunia.  

PUMZIKA KWA AMANI MWALIMU. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles