28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Homa ya dengue yamlaza Mbowe, aiomba mahakama apumzike

Kulwa Mzee, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameiomba mahakama impe muda aweze kupumzika kutokana na afya yake, ambapo amesema anaumwa homa ya dengue, malaria na shinikizo la damu.

Mbowe kupitia Wakili wake Peter Kibatala aliifahamisha hayo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba leo Jumanne Novemba 26, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya mshtakiwa huyo kuhojiwa na mawakili wa Jamhuri.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka, Faraja Nchimbi amedai kesi imekuja kwa ajili ya kujibu maswali ya upande wa mashtaka baada ya kumaliza kujitetea na kwamba wako tayari kuendelea.

Wakili Kibatala amedai kuwa kama mawakili wako tayari kuendelea lakini shahidi (Mbowe) hali yake siyo nzuri hivyo aliomba apumzike.

Amedai kwa sababu kesi hiyo ni ya jinai pamoja na kuumwa kwake homa ya dengue, malaria na shinikizo la damu ameona ni muhimu kutii mahakama na kuja kusikiliza kesi hiyo.

“Mshtakiwa aliruhusiwa kutoka Hospitali ya Agha Khan alikokuwa amelazwa Novemba 22 mwaka huu, hivyo ameomba kupumzika kwa sababu hali yake si nzuri. Kwa sababu yeye ni shahidi na anatakiwa kujibu maswali, tunaomba ahirisho,” amedai Kibatala.

Akijibu hoja hiyo, Nchimbi amedai wiki iliyopita walipokea taarifa ya kuumwa kwa Mbowe iliyoambatanishwa na vyeti vya matibabu.

Amedai wanaamini kuwa tangu Novemba 22 mshitakiwa aliporuhusiwa na kwa kuwa hakuna maelekezo mengine ya daktari atakuwa amepumzika vya kutosha na amepona. Hata hivyo waliomba ahirisho kwa siku ya leo na kesi iendelee kama ilivyopangwa.

Hakimu Simba alisema kuwa afya ya mshtakiwa ni jambo la msingi hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28, 29 na Desemba 2, 3 na 4 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles