24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hoja moja yaikomboa ndege iliyokamatwa Afrika Kusini

Kulwa Mzee -Dar es salaam

NDEGE ya Serikali aina ya Airbus A220-300 inayotumiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), iliyokuwa ikishikiliwa kwa amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng nchini Afrika Kusini tangu Agosti 21, mwaka huu, imeachiwa baada ya mahakama hiyo kukubaliana na hoja za mawakili wa Serikali ya Tanzania waliopinga hatua hiyo.

Hatua ya kushikiliwa ndege hiyo, ilikuja baada ya raia wa Afrika Kusini, Hermanus Steyn kufungua kesi ya fidia.

Steyn alikuwa anamiliki ardhi, mifugo na mali, ambazo zilitaifishwa na Serikali ya Tanzania miaka ya 1980 na pande zote mbili walikubaliana fidia atakayolipwa.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, Serikali ya Tanzania, kwa mujibu wa mkulima huyo imeacha kulipa deni hilo, na hatua ya kuomba ndege kushikiliwa ilikuwa moja ya harakati zake za kutaka kumaliziwa deni.

 Mara baada ya kushikiliwa ndege hiyo uwanja wa Oliver Tambo jijini Johannesburg kwa amri ya mahakama, Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi alisema; “kesi hii ni madai ya muda mrefu ya fidia ya ardhi iliyotwaliwa tangu miaka ya 1980 huko, hivyo si kesi kwamba ni ATCL ndiyo inadaiwa, Hapana. Tunaipambania ndege hii kwa masilahi ya taifa letu na tunaamini siku moja itarudi kuendelea na shughuli zake za kawaida.”

Maombi ya kupinga kushikiliwa kwa ndege hiyo yalisikilizwa Ijumaa ya wiki iliyopita.

Katika kesi hiyo mawakili kutoka ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, walishirikiana na mawakili wa Afrika Kusini katika maombi ya kupinga kushikiliwa kwa ndege hiyo.

Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa jana na mahakama hiyo ambayo gazeti hili imeiona, Agosti 30, mwaka huu Serikali iliwasilisha sababu tatu za kupinga kushikiliwa kwa ndege wakidai kwamba tuzo ya kulipa dola za Marekani milioni 36 ilikufa baada ya kufikia makubaliano ya kulipa dola milioni 30.

Walidai katika hoja zao, Steyn hawezi kutumia tuzo ya kwanza ya kumlipa dola milioni 36 kufungua kesi ya kushikilia mali nchi ya kigeni.

Pia Steyn hawezi kulazimisha kusaini makubaliano nchini Afrika Kusini.

Hoja ya pili ni kwamba kinga ya dola inazuia ukamataji wa mali za dola hata kama unaidai ikiwa suala lililowaleta mahakamani si la kibiashara.

Inadaiwa makubaliano kati ya Serikali na Steyn si zao la biashara kama wakili wake alivyodai mahakamani.

Hoja ya tatu ni uraia wa wahusika wa kesi hiyo, kwamba Tanzania na Steyn hawana uwezo kisheria kuzitumia mahakama za Afrika Kusini kwa kuwa wote si raia wa nchi hiyo.

Mahakama ilikubali hoja moja ambayo ni ya kwanza kati ya hoja tatu zilizowasilishwa na kuona kwamba haina mamlaka ya kushikilia mali hiyo, hivyo kuamuru iachiwe na Steyn alipe gharama za kesi pamoja na gharama za mawakili wawili wa upande wa Serikali.

Hoja nyingine mbili mahakama haikuzijadili katika kutoa uamuzi wake.

Jana baada ya mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro aliyekuwa nchini Afrika Kusini, alisema; “hoja zote walizowasilisha mawakili wetu zimekubaliwa, mahakama imeamuru ndege iachwe hivyo itaondoka wakati wowote.

“Amri iliyotolewa katika Mahakama ya Tanzania inatekelezwa na Mahakama za Tanzania.”

Alisema wanashangaa kuona mdai alikata rufaa siku moja kabla ya hukumu kutolewa na kushangaa alijuaje hukumu kabla haijatoka.

Inadaiwa kuwa juzi Steyn aliwasilisha maombi ya kukata rufaa kupinga uamuzi huo akidai kwamba hakutendewa haki, wakati hukumu ilisomwa jana.

Ndege hiyo ilishikiliwa kutokana na maombi namba 28/994/2019 yaliyowasilishwa na mwombaji Steyn kupitia ofisi ya uwakili ya Werksmans iliyopo nchini Afrika Kusini.

Maombi hayo ya kusikilizwa upande mmoja yaliwasilishwa Agosti 21, mwaka huu dhidi ya Serikali ya Tanzania, Uwanja Ndege wa Afrika Kusini, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Afrika Kusini, Kampuni ya Ndege Tanzania, Mr Sibusisi Nkabinde, Mr Kgomotso Molefi na Mr Patrick Sithole.

Katika maombi hayo, kuliambatanishwa na kiapo kilichoapwa na na Martin Richard Steyn na Bianka Pretorius wakisapoti maombi ya kushikilia ndege kwa sababu mdai anadai Serikali ya Tanzania dola za Marekani 36,375,672.81.

Mahakama ilisikiliza maombi hayo upande mmoja tarehe hiyo hiyo yaliyowasilishwa na kukubali hoja za mwombaji na kuamuru ndege ikamatwe.

Mwaka 2010 mbele ya Jaji mstaafu Josephat Manckanja, Steyn alikuwa anadai fidia ya shamba lake jumla ya dola za Marekani milioni 36.

Mahakama ilikataa, pande zote mbili wakaketi kwa makubaliano na walifikia makubaliano ya Serikali ya Tanzania kulipa dola za Marekani milioni 30.

Baada ya makubaliano hayo, Serikali ya Tanzania ilianza kulipa na ilishalipa kiasi kikubwa cha fedha.

Pamoja na kuwa tayari malipo yalishafanyika kwa kiasi kikubwa, mdai katika maombi yake anadai kiwango kile kile cha awali cha zaidi ya Dola za Marekani milioni 36 kilichokuwepo kabla ya makubaliano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles