24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hofu ya kubadilishana watoto Hospitali ya Meta

IMG_1628Na Pendo Fundisha, Mbeya

KWA miaka kadhaa sasa Hospitali ya Wazazi ya Meta iliyopo mkoani Mbeya imekuwa kimbilio la wajawazito wenye matatizo kwa kipindi chote cha ujauzito wao na hata nyakati za kujifungua.

Lakini kuna uwezekano wa hali hii kutoweka ikiwa hatua za haraka na za lazima za kuiongezea uwezo hospitali hiyo hazitachukuliwa.

Kihistoria, hospitali hiyo ilijengwa mwanzoni mwa miaka ya 1950 na wamisionari, lengo kuu likiwa ni kuifanya taasisi yenye kuhudumia wagonjwa wa Kifua Kikuu katika Mkoa wa Mbeya pamoja na maeneo ya jirani.

Wakati wa ujenzi wa taasisi hiyo, Mkoa wa Mbeya ulikuwa na wakazi wanaokadiriwa kufikia 200,000 tu.

Mwaka 1985, serikali iliichukua rasmi hospitali hiyo na kuifanya mahususi kwa ajili ya huduma za kinamama wajawazito.

Umuhimu wa hospitali hii kwa wakazi wa Mbeya pamoja na mikoa ya jirani ya Iringa, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Njombe na Songwe, umekuwa mkubwa na  wenye manufaa kwa mamia kama si maelfu ya kina mama katika ukanda huu.

Serikali kwa nyakati tofauti imejitahidi kuwekeza nguvu za kutosha kuhakikisha kuwa huduma zitolewazo hospitalini hapo zinakuwa ni za kiwango cha juu na hivyo kupunguza vifo vya kina mama vilivyokuwa vikitokana na matatizo ya uzazi, pamoja na watoto wachanga.

Hata hivyo eneo moja ambalo serikali imelisahau ni lile la kutanua miundombinu ya hospitali hii hususan upande wa majengo. Tangu serikali iichukue hospitali hii jambo kubwa ambalo limekuwa likifanyika kwa upande wa miundombinu yake ni ukarabati tu wa majengo yaliyokuwepo. Majengo pekee ambayo yameongezwa ni yale ya benki ya damu salama na kliniki ya watoto ambayo nayo bado ni ndogo.

Kwa ambaye anaweza kutembelea hospitali hii, jambo moja ambalo ni rahisi kwake kulishuhudia ni ubora na usafi wa eneo hilo, ingawa hili ni lenye kuonekana kwa mtu anayepita nje ya vyumba vya kutolea huduma hospitalini hapo. Kwa anayeingia ndani ya vyumba hivyo, hali ni tofauti sana.

Ni yenye kusikitisha na kuhuzunisha na zaidi ya yote inahatarisha si tu kina mama wanaokwenda kupata huduma hospitalini hapo bali hata watoto wanaozaliwa na wajawazito hao.

Ikiwa na wodi nne tu zilizo rasmi kulaza wagonjwa, hospitali hii haionekani kwa namna yoyote ile kuwa katika hali ya kuweza kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa wenye kuhitaji huduma zake. Idadi hii ya wodi, ilikuwa sawa kwa wakati ilipokuwa inajengwa, ambapo mkoa ulikuwa na wakazi takribani laki mbili tu.

Hivi sasa hospitali hii inatoa huduma kwenye eneo ambalo idadi ya wakazi wake inakadiriwa kuwa milioni nane.

Ongezeko hili la idadi ya watu, ni mara 40 ya idadi ya watu waliokuwepo wakati hospitali hii inajengwa, na kwa namna yoyote ile itakuwa ni kujidanganya kuwa ukarabati tu wa  majengo na miundombinu iliyopo, vinaweza kukidhi mahitaji ya idadi hii ya wahitaji huduma.

Wakati hospitali nyingi kubwa nchini zikiwa zinakabiliwa na tatizo sugu la wagonjwa kulundikana katika wodi moja huku wengi wakilala chini, hali ni mbaya zaidi katika hospitali hii ya Meta, kwani wapo wagonjwa ambao hata nafasi ya kujibana wakalala chini wanaikosa.

Hospitali hii ambayo ni kitengo cha Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, iliyoko jijini Mbeya, ina wodi nne tu zenye  vitanda 120 vya watu wazima sawa na vitanda 30 kwa kila chumba. Vitanda hivi vilitarajiwa kutumika kulaza wagonjwa 120 tu.

Hata hivyo, idadi kubwa ya wagonjwa ambayo imekuwa ikizidi uwezo wa hospitali hii, imelazimu kila wodi kuwa na wagonjwa kati ya 180-200.

Wapo ambao hulala wawili wawili katika kitanda kimoja na wanaolala chini.

Msimamizi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. John Francis, anasema tatizo limekuwa kubwa kwa sababu kina mama wanaotakiwa kujifungua na wale ambao mimba zao zinakuwa na matatizo wanaongezeka kwa wingi. Wengine ni wale wenye mtatizo ya saratani ya shingo ya kizazi, fistula na magonjwa mengine,” anasema Dk. Fransic.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, aliyetembelea hospitali hiyo hivi karibuni, ameutaka uongozi wa hospitali hiyo kuangalia njia mbadala itakayoweza kupunguza msongamano huo, huku akisisistiza kuwachaji fedha wagonjwa ambao hawana kesi za kiuchunguzi.

“Hospitali hii imejengwa kwa ajili ya wagonjwa ambao kesi zao zinahitaji kufanyiwa huchunguzi hasa masuala ya uzazi, lakini wananchi wengi wamekuwa wakikimbilia hapa kutokana na huduma bora zinazotolewa na kusababisha hospitali kulemewa.

“Hivyo kwa wale ambao hawana kesi yoyote ile ya kiuchunguzi wa kiafya ni vema wakatozwa kiasi cha fedha. Serikali haiwezi kumzuia mtu kufika kutibiwa lakini kutokana na msongamano huu ni vema kituo kikaanza kuwachaji wagonjwa ambao si walengwa hata kama ni wajawazito,” anasema Ummy.

Hospitali hiyo pia ina kitengo maalumu cha watoto wachanga, ambacho hakipo katika hospitali nyingi zilizomo katika kanda hii.

Katika kitengo hiki, watoto wachanga wa chini ya mwezi mmoja wanapozaliwa na matatizo mbalimbali kama yale ya kabla ya muda wa miezi tisa (njiti), hufika hapo kuhudumiwa.

Watoto hawa kwa kawaida ni lazima waambatane na wazazi wao, ambao kimsingi nao pia huhitaji sehemu ya kulala na hii yote huendelea kukuza ukubwa wa tatizo hili.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda, ambayo ndio hospitali mama kwa ile ya Meta, Dk. Godlove Mbwanji, licha ya kujivunia ubora wa huduma zitolewazo na taasisi hiyo hivi sasa, anasema bado hawaridhishwi na uwiano baina ya huduma hizo na miundombinu iliyopo.

“Huduma ni nzuri lakini changamoto ni mahala pa kujihifadhi wale wenye uhitaji wa kulazwa, kwa mfano wakati watoto wanatafutiwa sehemu ili walazwe, mama inampasa asimame na ieleweke kuwa hata watoto wenyewe huwa tunalazimika kuwalaza wawili hadi watatu katika kitanda kimoja.

“Hii ina hatari sana kwani kuna uwezekano wa wazazi kubadilishana watoto. Na ikumbukwe kwamba mama anayetoka kujifungua anakuwa amechoka sana, anahitaji mahala pa kupumzika anyonyeshe mtoto vizuri, jambo ambalo kwa Meta halipo kwani maeneo ni finyu hayatoshi.

“Magodoro ni mengi lakini hakuna sehemu ya kuyahifadhi, kuna vitanda lakini vitawekwa wapi. Shida kubwa ya hapa ni majengo, haya yaliyopo yamesha-bust,” anafafanua mkurugenzi huyu.

Kulingana na Mkurugenzi huyo, Meta inafanya upasuaji wa fistula, saratani ya mlango wa uzazi, upasuaji wa akina mama wanaojifungua ambazo zote hufanywa kwa wakati wote.

Uhaba wa vyumba hauko tu katika upande wa wagonjwa wenye kulazwa, bali pia hata katika upande wa utoaji huduma, hususan upande wa vyumba vya upasuaji.

Mkurugenzi huyo anasema idadi ya vyumba vya upasuaji kwa sasa ni viwili tu, huku idadi ya oparesheni zenye kuhitajika kufanywa kwa siku moja ikiwa ni kubwa zaidi ya uwezo wa vyumba hivyo.

“Oparesheni za kujifungua kwa siku ni kati ya 10 hadi 15, na kama unavyojua mama mjamzito wakati wa kujifungua ukifika hatakiwi kucheleweshwa. Oparesheni zingine zinazofanyika kwa siku ni kati ya 10 hadi 20. Kwahiyo ni wastani wa oparesheni 20-30 kwa siku,” anasema.

Ni mazingira haya ambayo wamekuwa wakikumbana nayo wagonjwa wanaofika hospitalini hapo, ambayo yamewafanya pia waungane na uongozi wa hospitali hiyo na kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuiwezesha hospitali hiyo kupata majengo mapya na ya kisasa.

Upatikanaji wa jengo jipya na la kisasa utaiwezesha hospitali hiyo kupanua wodi, kuongeza vyumba vya upasuaji, kuweka ofisi za watumishi, wodi ya watoto kwani iliyopo sasa ina uwezo wa kuchukua vitanda 40 huku watoto wanaopatikana kwa siku ni 80 -100.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles